The House of Favourite Newspapers

Eymael: Sisi Siyo Maroboti

0

LUC Eymael ambaye ni kocha mkuu wa Yanga, ameshangazwa na jinsi mwenendo wa ratiba yao ya ligi ambapo ameweka wazi kwamba hata Ulaya kwenye ligi zenye ushindani mkubwa hawachezi kama wao
wanavyocheza.

 

Kocha huyo amesema kwamba ratiba hiyo inawafanya wacheze mechi kila baada ya siku tatu ambapo ni ngumu kwake kwa sababu wachezaji wake siyo maroboti.

Yanga walicheza Alhamisi iliyopita kisha Jumamosi wakacheza tena na leo Jumanne watacheza na Mbeya City katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

 

Eymael, raia wa Ubelgiji, ameliambia Championi Jumatatu kuwa wana ratiba ambayo ni ngumu kwao kwa sababu wanacheza mechi zaidi ya tisa katika mwezi mmoja, kitu ambacho ni kigumu kwa sababu wachezaji wake ni binadamu na siyo maroboti.

 

“Sisi siyo maroboti, ni binadamu, kucheza mechi tisa katika mwezi mmoja siyo kitu chepesi, licha ya kwamba wengi wanaona tunaimarika kila baada ya mechi.

“Huwezi kucheza dakika 90 katika siku tatu tofauti tena katika uwanja wa bandia, hili siyo sawa japokuwa tunatakiwa kucheza kwa sababu ndiyo ratiba yetu, tunaendelea na mbio zetu kwenye ligi.

 

“Kama ukiwaambia Ulaya wacheze mechi namna hii watalia licha ya kwamba wao wana mazingira bora zaidi hata vyumba vya kuwafanyia masaji wachezaji na vitu vingine lakini hawawezi kufanya hivi. Mechi ijayo nitalazimika kubadili wachezaji kwa sababu ya kuwafanya baadhi yao wapumzike,” alisema Eymael.

Leave A Reply