The House of Favourite Newspapers

FAHAMU AINA ZA FANGASI WA KWENYE NGOZI

FANGASI wapo kila mahali, kwenye miti, mimea, mchanga, ndani majumbani mwetu na hata kwenye ngozi ya binadamu.  

 

Kuna aina milioni moja na nusu za wadudu aina ya fangasi wanaotambulika duniani, kati yao ni fangasi 300 tu wanaojulikana kusababisha maambukizi kwa binadamu. Uvutaji wa hewa iliyochanganyika na mazalia ya fangasi yanayojulikana kama fungal spores pamoja na uwepo wa uvamizi au ukuaji wa fangasi kwenye ngozi ya binadamu husababisha maambukizi ya fangasi, hivyo basi maambukizi mengi ya fangasi huanzia kwenye mapafu au kwenye ngozi ya mtu.

 

Tuangalie maradhi ya ngozi yanayosababishwa na fangasi hasa wale wanaoshambulia sehemu za wazi za mwili, yaani Tinea corporis. Kuna fangasi wa ngozi ya mwili. Aina hii ya fangasi huathiri sehemu zisizojificha kama vile, katikati ya vidole au chini ya kucha.

 

Aina hii ya fangasi huathiri sehemu za mwili ambazo ziko wazi kwa mfano tumboni au mgongoni. Fangasi wa aina hii huwa na uwezo wa kushambulia sehemu kubwa zaidi ya mwili kama mikono, miguu, uso na kiwiliwili na huonekana kwenye mwili wakiwa na muundo wa duara mfano wa sarafu na ngozi ikiwa imevimba kwenye uzio wa eneo ambalo fangasi amevamia, yaani ukiangalia eneo lenye athari utaona kuna kaduara, mfano wa sarafu.

Eneo lenye maradhi pia hubadilika rangi na kuwa na rangi tofauti kidogo na ngozi ya eneo ambalo halijaathirika na maambukizi. Mfano, mtu ambaye ana ngozi ya maji ya kunde, eneo ambalo limeathirika linaweza kuwa na rangi nyeusi zaidi au likawa na rangi nyaupe zaidi.

 

DALILI ZA MAAMBUKIZI

Aina hii ya fangasi huwa na dalili chache sana na kubwa ni muonekano wake kama nilivyouelezea hapo juu. Ila vifuatavyo huonekana:

 

Kubadilika kwa rangi ya ngozi ya eneo lenye maambukizi, eneo la ngozi lenye maambukizi huwa lina muundo wa duara mfano wa sarafu ya fedha. Ngozi kubanduka kwenye eneo lenye maambukizi pia kukauka kwenye eneo lenye maambukizi. Inawezekana kabisa kupata muwasho kwenye eneo lililo na maradhi ingawa si sehemu zote za mwili zenye maambukizi zinaonyesha dalili hii.

AINA ZA MAAMBUKIZI  YA FANGASI

Maambukizi ya fangasi nje ya mwili (Superficial mycoses): Ni fangasi ambao husababisha maambukizi kwenye ngozi, nywele, kucha na hawaishi kwenye tishu mwilini. Fangasi aina hii hujulikana kama Dermatophytes. Fangasi hawa hushambulia sehemu tajwa hapo juu kwa kutoa vimeng’enyo (Extracellular enzymes) vinavyolainisha protini aina ya keratin inayopatikana katika maeneo hayo.

 

Maambukizi haya ya fangasi yamegawanyika kama ifuatavyo:

Tinea Corporis – Maambukizi ya fangasi yanayopatikana katika sehemu yoyote ile mwilini.

Tinea Pedis (Athlete’s foot)– Maambukizi ya fangasi katikati ya vidole vya miguuni na kwenye nyao za miguu.

Tinea Unguium (Onchomycosis) – Maambukizi haya yanapatikana kwenye kucha za vidole vya miguuni na vya mikononi.

 

Tinea Capitis – Huonekana kwenye kichwa hasa kwa watoto wadogo. Husababisha mapunye kwenye kichwa, nywele kunyofoka, mabaka meusi kwenye kichwa yaliyoambatana na mcharuko (Inflammation), kutokwa na magamba kichwani, kuwashwa na kuvimbavimba kwenye kichwa.

Tinea Cruris – Maambukizi ya fangasi sehemu za siri.

 

inea Barbae – Huonekana maeneo yenye ndevu, kwenye uso na shingoni.

Tinea Vesicolor – Maambukizi ya fangasi kwenye ngozi ya watu wazima. Maambukizi haya hayaonekani kwenye uso ila husababisha ngozi kuwa na mabaka yenye rangi ya kahawia iliyochanganyika na rangi nyekundu (reddish brown).

Tinea vesicolor huonekana sana kwenye ngozi ya watu wanaoishi sehemu zenye joto kali au wenye matatizo kwenye vichocheo vya miili yao (hormonal abnormalities) ingawa wote wanaopata maambukizi haya huwa ni watu wenye afya njema.

 

HUSAMBAA VIPI?

Maradhi haya huambukizwa kwa njia zifuatazo:Kugusana na mtu mwenye maambukizi ya fangasi hawa, kugusa vitu vilivyobeba fangasi wa aina hii kama vile nguo ikiwemo nguo za ndani, chanuo la nywele, mikufu, vifaa vya kuogea, viatu na soksi. Unaweza kupata maambukizi pia kwa kugusa sehemu ambazo mwenye maradhi amegusa kama ukuta, viti, makochi na vitu vingine.

NANI YUPO HATARINI?

Watu ambao huweza kupata maambukizi ya fangasi wa aina hii ni kama wafuatao: Wale wanaofanya kazi zinazohusisha kugusana na watu wenye maambukizi ya fangasi, wanaolala kitanda kimoja na wenye maambukizi ya fangasi wa aina hii, wanaoshiriki mapenzi na wenza wenye maambukizi ya fangasi hao.

 

TIBA NA USHAURI

Tiba ipo baada ya kuonana na daktari. Anaweza kukupa dawa ya kupaka au ya kumeza, itategemea atakavyouona ugonjwa. Ni vema kuwahi kuonana na daktari ukiona dalili kabla ugonjwa haujasambaa.

Na Dk. Marise Richard

 

Comments are closed.