The House of Favourite Newspapers

Fahamu Kwa Undani Ugonjwa Wa Pumu (Asthma)

0

LEO tutaangalia ugonjwa wa pumu au kitaalamu huitwa asthma. Ugonjwa wa pumu huathiri njia za hewa ambazo huingiza na kutoa hewa katika mapafu. Mtu mwenye ugonjwa huu kuta zake za ndani za njia ya hewa hupata maumivu ambayo kitaalamu huitwa inflammation na kuvimba.

 

Maumivu katika njia za hewa huzifanya njia hizo za hewa kujihami kwa kusinyaa na hivyo kupunguza kiasi cha hewa kinachopita kwenda kwenye mapafu. Hali hii husababisha mgonjwa kutoa mlio kama wa filimbi au mluzi wakati wa kupumua. Ugonjwa wa pumu unaweza kudhibitiwa kama vile ugonjwa wa kisukari na moyo unavyoweza kudhibitiwa.

 

AINA ZA PUMU

Kuna aina kuu mbili za pumu. Aina ya kwanza ni ile inayoanza mapema kitaalamu huitwa early onset asthma na aina ya pili ni ile inayochelewa kuanza yaani late onset asthma. Tuchambue kwa kifupi aina hizo za pumu. Pumu inayoanza mapema (early onset asthma) Aina hii ya pumu huanza kumkumba mtu akiwa mtoto ambapo miili yao hutengeneza kingamwili (antibodies) za IgE. Wagonjwa wa aina hii ya pumu hutambuliwa kwa vipimo maalum vya ngozi ambapo huonyesha kuathirika kwa asilimia kubwa ya vipimo hivyo vinapofanywa. Pia wagonjwa hawa huwa na matatizo mengine ya mzio (allergic disorders) kama mafua na ukurutu (eczema).

 

Pumu inayochelewa kuanza (late onset asthma) Aina hii ya pumu,tofauti na iliyopita, humkumba mtu akiwa mkubwa. Hakuna ushahidi wowote unaohusisha maradhi haya na mizio (allergens) vinavyotokana na mazingira na uwezo wa kusababisha aina hii ya pumu. Haifahamiki hasa ni sababu zipi zinazofanya njia za hewa kupata maumivu na hivyo kusababisha mtu kupata ugonjwa huu wa pumu. Vyanzo mbalimbali vinaonyesha kuwa ni kutokana na mseto wa vitu kama tumbaku, maradhi na baadhi ya vitu vinavyosababisha mzio.

 

Kuna vitu katika mazingira ambavyo vinaweza kusababisha mtu kushambuliwa na pumu. Vitu vinavyosababisha mzio ni kama vumbi, mende, chavua (pollen) kutoka kwenye miti na majani, viwasho (irritants) kama moshi wa sigara, uchafuzi wa hewa, harufu kali kutoka kwenye rangi au kitu chochote kitoacho harufu, au msongo wa mawazo na maradhi yatokanayo na virusi au manyoya au magamba ya wanyama.

Mtu anaweza kupata pumu kutokana na kuwa na mzio na madawa kama aspirin, ugonjwa wa kucheua, viwasho au vizio vitokanavyo na kemikali au kuwa na magonjwa ya njia ya hewa n.k Mtu anaweza kupata ugonjwa wa pumu kama anaishi katika miji mikubwa na kukumbana na vitu ambavyo kwake
humsababishia mzio, au kuvuta hewa iliyo na moshi, kemikali zitokanazo na kilimo,dawa za kutengeneza nywele, rangi, vyuma, plastiki au vifaa vya elektroniki. Mtoto anaweza kuwa na pumu kwa kurithi kwa mmoja wa wazazi wake mwenye pumu au baada ya kuathirika na maradhi ya mfumo wa hewa kama kikohozi na mafua wakati wa utoto au kutokana na kuwa na unene wa kupita kiasi (obesity), kuwa na ugonjwa wa kucheua na kiungulia (Gastro esophageal reflux disease).

 

DALILI ZA PUMU Baadhi ya dalili za kawaida za ugonjwa wa pumu ni kama zifuatazo: Mgonjwa kushikwa na kikohozi: Mara nyingi kikohozi cha pumu huwa kikali nyakati za usiku au alfajiri na hivyo kumfanya mgonjwa kutolala vizuri usiku. Mgonjwa kutoa sauti ya mfano wa mtu anayepiga mluzi au filimbi wakati wa kupumua, kifua kubana ambapo mgonjwa husikia kama kitu kinakandamiza kifuani au wakati mwingine husikia kama mtu amemkalia kifuani. Dalili nyingine ni mgonjwa kukosa hewa na kujikuta kama hawawezi kupumua kwa hewa inayoingia na kutoka kwenye mapafu. Kutokana na hilo mgonjwa huyo atakuwa anapumua harakaharaka. Dalili hizo zinaweza kuwa mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha. Wengine hupata dalili hizo mara moja tu kwa mwezi, wengine kila wiki na wengine hupata dalili kila siku.

 

UCHUNGUZI Mgonjwa ni lazima afanyiwe kipimo kwa kuangalia jinsi mapafu yanavyofanya kazi. Kipimo hicho hujulikana kitaalamu spirometry na hutumika kwa watu kuanzia miaka
mitano na kuendelea na hutathmini kiasi cha hewa mtu awezacho kukitoa baada ya kuvuta hewa kwa nguvu na kwa haraka. Kipimo hiki cah spirometry pia hutumika kutathmini jinsi mgonjwa wa pumu anavyoendelea, kupata nafuu au tatizo kuongezeka. Mgonjwa pia anaweza kufanyiwa kipimo cha mzio (Allergy Test). Kipimo cha ugonjwa wa kucheua na kiungulia pia hufanyiwa mgonjwa.

 

Mgonjwa pia ni lazima apimwe mapafu kwa X-ray ili kuona iwapo kuna kitu chochote kilichoziba njia ya hewa au kama kuna maradhi yoyote katika mapafu au moyo. TIBA Kuna aina mbili za matibabu ya pumu, moja ni ile ya dharura ili kutoa msaada au nafuu ya haraka. Dawa hizi ni zile zinazosaidia kutanua njia za hewa ambazo zimesinyaa yaani bronchopdilators ambazo pia husaidia kuilainisha misuli ya njia za hewa iliyosinyaa ili iweze kutanuka na kuruhusu hewa ya kutosha kuingia kwenye mapafu. Aina nyingine ya dawa ni zile za muda mrefu. Aina hizi za dawa hutumiwa mara kwa mara kwa kipindi kirefu kuzuia dalili za pumu na mashambulizi. Watu wenye pumu isiyoisha wanahitaji matumizi ya dawa ya muda mrefu.Kotikosteroidi za kuvuta (inhaled corticosteroids) ni nzuri kwa aina hii ya pumu.

 

TIBA KWA WATOTO Watoto wenye pumu kama ilivyo kwa watu wazima wanapaswa kumwona daktari wale walio na umri mdogo wanahitaji uangalizi wa wazazi/ walezi ili kudhibiti pumu. Watu wazima wanaweza kutakiwa kupunguza au kuongeza matumizi ya dawa za pumu kutokana na maradhi mengine waliyonayo. Madawa kama ya kutibu shinikizo la juu la damu, ugonjwa unaotanua mboni ya jicho na kutatiza kuona (glaucoma),aspirini na dawa za maumivu (non steroidal anti inflammatory drugs) huingiliana na utendaji wa dawa za pumu au zenyewe kusababisha pumu, hivyo matumizi yake yanahitaji ushauri wa daktari.

 

Wajawazito wenye pumu wanahitaji ushauri wa karibu wa daktari kwa kuwa ikiwa pumu itasababisha kusinyaa kwa njia ya hewa basi wanaweza kusababisha upungufu wa hewa ya oksijeni kwa mtoto hali ambayo ni hatari kwa mtoto tumboni. Dawa nyingi za pumu hazina madhara kwa mtoto aliye tumboni, hivyo ni muhimu kuendelea na matibabu wakati wa mimba kwa ushauri wa daktari kuliko kuacha.

 

KINGA Njia pekee ya kujikinga na pumu ni kuepuka mzio au vitu vinavyoweza kusababisha ugonjwa huo kwa kusafisha nyumba kila wiki kupunguza vumbi, kuwaepusha watoto na baridi au kukumbatia paka au wanyama, kuepuka kufanya mazoezi kwenye baridi, kuepuka moshi wa sigara, kudhibiti ugonjwa wa kucheua na kiungulia na kadhalika.

Na Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta. Simu: 0713 252 394

Leave A Reply