FAHAMU MAMBO MUHIMU KUJADILIANA KABLA YA KUOANA-2

MAMBO vipi marafiki? Naamini mpo wazima kabisa. Basi tuendelee na mada yetu tuliyoanza nayo wiki iliyopita, ambapo tunaangalia mambo ya muhimu kuzingatia kabla ya kuingia kwenye ndoa na mpenzi wako.  Wiki iliyopita tulianza kuona kuhusu imani za dini na changamoto zake wakati wa kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa. Sasa tuendelee…

NI SAHIHI KUOANA DINI MBILI TOFAUTI?

Siku hizi kuna utaratibu wa ndoa za mseto; baadhi ya madhehebu yanaruhusu maharusi waoane chini ya msimamo wa imani yao hata kama kila mmoja anaabudu kwake. Kisheria halina tatizo hasa kwa kuwa suala la ndoa ni la kisheria zaidi. Tunaporudi katika utaratibu wa maisha ya kawaida ndipo tunapokutana na matatizo. Yapo matatizo kadhaa yanayoweza kutokea kwa kuishi wanandoa wawili huku kila mmoja na imani yake.

Kama nilivyotangulia kusema kwamba imani ndiyo msingi, hivyo hata katika uhusiano na ndoa migogoro ikizidi, njia salama na za siri zaidi kumaliza ukiondoa kwa wanasaikolojia ni katika imani za dini.

Tafiti zinaonesha kwamba, kesi nyingi zinazopelekwa kwa viongozi wa dini huisha kwa amani kuliko zile za kisheria. Kuwa na imani tofauti, maana yake wanandoa wanakosa mahali sahihi pa kupeleka matatizo yao. Upo ushahidi mwingi wa wazi juu ya matatizo haya. Nitakupa mfano mmoja kutoka kwa msomaji mmoja niliyepata kuzungumza naye akiomba ushauri.

“Nimeolewa miaka 28 iliyopita, kwanza niliishi na mume wangu mwaka mzima bila ndoa, maana tulikuwa tunavutana kuhusu suala la dini (naomba kuficha imani zao). Mume wangu alinisisitiza nimfuate kwenye dini yake ili aweze kunioa, nikakubali.

“Mwanzoni ndoa ilikuwa tamu sana lakini baadaye mambo yakabadilika. Mume wangu amekuwa mkorofi na ana wanawake wengine nje. Amani niliyoifuata kwenye ndoa yangu kwa kuamua kubadili dini siipati tena.

“Mbaya zaidi mume wangu hanifundishi namna ya kuabudu kwa utaratibu mpya wa imani yake, imefikia mahali nimeona najitesa tu nafsi yangu, siku hizi kwa kujiiba huwa nakwenda kwenye imani yangu ya zamani na ninaabudu huko.” Kupitia kisa hicho unaweza kuona namna unavyoweza kupata usumbufu kwa kutokuwa makini na jambo hili. Wakati ukifikiria moyo wako, mapenzi yako kwa mwenzako, fikiria pia kuhusu watoto wenu wajao.

Je, watafuata madhehebu gani ikiwa mnaoana mkiwa mpo tofauti? Hakika ni jambo la kutafakari kabla ya kuchukua uamuzi wa kuingia kwenye ndoa. Epuka mijadala ndani ya ndoa ambayo mnaweza kuijadili kabla hamjaingia kwenye ndoa.

Wakati mwingine ukweli unaweza kuwa unauma lakini ni vizuri kuuchukua kama changamoto. Haraka ya ndoa na kufanya uamuzi wa haraka wa kubadili imani au ndoa ya mseto, kunaweza kukusababishia matatizo.

Uamuzi wa nani awe mke/ mume wa ndoa unatakiwa kuchukua kwa umakini mkubwa sana. Ukikosea kuchagua mwenzi sahihi wa maisha ni dhahiri kwamba huko mbele maisha yako yanaweza kubadilika na kuwa machungu. Jifunze kupitia kwa wengine.

WEKENI MJADALA

Ili uwe salama na usiingie kwenye mtego huu ni vyema mkalizungumza jambo hili mapema sana. Unapokutana na mwenzako na ukahisi kuna dalili za kufika mbali katika uhusiano wenu ni vyema mkazungumzia kuhusu imani zenu. Usisubiri tatizo likue, lazima ujue mwenzako ni imani gani ili baadaye mkifikia kwenye suala la ndoa isiwe tatizo kwako.

VIPI MAKABILA?

Wazee wanajua zaidi kuhusu hili ndiyo maana kijana akipata mchumba swali la kwanza kuuliza ni juu ya dini na kabila. Kuna makabila yana mila potofu; sasa huwezi kusubiri mpaka mtakapofikia kwenye mipango ya ndoa ndiyo unaanza kuchunguza.

Unaingia kwenye ndoa unakutana na tabia za ovyo, kumbe ni kosa lako hukuchunguza. Sitaki kuhukumu kabila fulani hapa, ila unapaswa kuwasilikiza wazee kuhusu mila na desturi za kabila unalotarajia kuoa kabla ya kufanya uamuzi. Naamini kuna kitu mmepata, siyo? Basi hadi wiki ijayo.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Toa comment