The House of Favourite Newspapers

Familia ya Nesi Aliyeaga Dunia Akiogelea na Kujirekodi, Yashindwa Kuurejesha Mwili Nchini

0
Hellen Nyabuto “Wendy”

FAMILIA ya muuguzi raia wa Kenya aliyeaga dunia nchini Canada wakati akiogelea katika swimming pool huku akijirekodi live kwenye ukurasa wake wa Facebook inasema kuwa imeshindwa kuurejesha mwili wake nchini kwa hafla ya mazishi.

 

Ikiongozwa na babake John Nyabuto, familia ya Hellen ‘Wendy’ Nyabuto imezungumza kuhusu kumpoteza mwanao ikisema kuwa bado inang’ang’ana kukubali kifo chake.

 

Kwa mujibu wa babake, bado wanawaza jinsi ya kuurejesha mwili wake nchini ili kuupa maziko yanayostahili.

 

“Nimelia tangu nilipopata hii taarifa. Rafiki zake wamekuwa wakipiga simu na kufafanua kilichotokea. Ninashindwa jinsi gani nitauleta mwili wake nchini.

 

“Nimepoteza binti yangu na hakuna kitu ambacho ninaweza kufanya. Sijui gharama ya kuusafirisha mwili wake kuja nchini, uchungu ni mwingi. Ninaomba msaada. Yeye ndio alikuwa mwanga wangu. Nilimsomesha kwa shida nyingi sana,” mzee Nyabuto aliambia gazeti la the Standard.

John Nyabuto, Baba wa Hellen ‘Wendy’

Kwa sasa mwili wake umepelekwa katika makafani moja jijini Toronto ukisubiri kufanyiwa upasuaji.

 

Wendy alikuwa akijirekodi moja kwa moja kwenye Facebook alipokuwa akiogelea Alhamisi majira ya saa nane adhuhuri, saa za Afrika Mashariki.

 

Wakati akifanya hivyo, Wendy alionekana mchangamfu na alijirekodi akijivinjari kwenye swimming pool hiyo. Hakuna mtu mwingine yeyote aliyeonekana karibu na eneo hilo.

 

“Haya mkoje mliko. Ni saa nane hapa… Nimetoka kazini, niko kwenye bwawa, naburudika tu,” anasikika akisema.

 

Mwanzoni mwa tukio hilo, Wendy alionekana kuchangamka sana na alionekana kufurahia kuogelea. Alikuwa akiogelea kidogo na kisha kurudi kwenye simu yake na kuangalia watu waliokuwa wakitazama video hiyo.

 

Wendy aliendelea kujivinjari na kwa bahati mbaya alizama na kufariki dunia. Kamera iliendelea kurekodi kwa takriban saa tatu kabla ya mtu kujitokeza kumsaidia.

Leave A Reply