The House of Favourite Newspapers

FEDHA ZAMCHANGANYA BEN POL AACHA CHUO

Mwanamuziki Bernard Paul ‘Ben Pol’ akiongea na mashabiki wake Dar Live.

WIKI iliyopita, tuliishia pale Majuto Mnyang’anga au kwa mliozoea kumuita Bernard Paul ‘Ben Pol’, akizungumzia baadhi ya biashara zake nje ya muziki. Lakini baadaye alianza mazungumzo mapya ambayo yalitufungulia ukurasa mpya, akijutia kujikita katika muziki huku akitupilia mbali kabisa masomo yake ya chuo kikuu tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wasanii wenzake anaowajua ambao wao waliweza kufanya muziki wao bila kukikacha chuo.


Baada ya dokezo hilo, sasa tusonge pamoja kujua sababu zilizomfanya aachane na chuo na kudili na muziki tu. ENDELEA HAPA anaanza kwa kusema:

 

“Katika harakati zangu zote ambazo nilielezea huko nyuma na kunionyesha nimemaliza form six na kujikita katika muziki, kuna jambo hapo ambalo sijalielezea kabisa kuwa pamoja na harakati za kuingia THT na baadaye kuja kutoa ngoma na kushaini katikati ya 2012, hapo niliamua kurudi Chuo cha Institute of Finance Management (IFM), kilichopo Posta jijini Dar es Salaam, lakini pamoja na hayo niliona bado muziki unanihitaji na una majukumu mengi kwangu.

Akicheza na mrembo mmoja kati shoo.

“Hivyo niliamua kujikita chuo kwa mwaka mmoja tu, ambao nao niliusoma mzima kama ulivyo bila kukosa hata siku moja ambapo nilikuwa nafanya vizuri ila niliamua kuachana na chuo kwa sababu wakati huo tayari nilikuwa nimeshapata tuzo na nina jina kubwa, hivyo simu za kazi zilikuwa nyingi sana kiasi kwamba nikasitisha,” anaeleza Ben Pol.

 

Ben Pol anafafanua kwamba, kilichomfanya aache chuo ni kujulikana, kwani ilikuwa kila anapopita kwa wanafunzi wenzake zile Ben Pol zilikuwa nyingi sana, hivyo akaacha chuo, na kuamua kuendelea na muziki pekee. Mkali huyu wa muziki anasema kuwa sasa anaona kwamba alifanya jambo la ajabu sana kwani muda umeshaondoka.

 

“Naamini kabisa kilichonichanganya zaidi ni mambo ya shoo za Fiesta na tuzo zile ambazo nilizipata wakati tumefunga chuo, kwani pale ndiyo nilibahatika kushinda tuzo ya Mtunzi Bora, Wimbo Bora wa RNB, lakini pia zile ziara za Kilimanjaro nadhani nazo zilinipagawisha kwani nilipiga fedha nyingi sana kipindi hicho kiasi kwamba mtu yeyote, angeweza kusitisha masomo kirahisi tu kama hasa aliingia katika muziki kibiashara zaidi.

 

“Lakini mbali na hivyo, utaona najuta kuachana na chuo kifaida sana maana maendeleo niliyonayo leo sina uhakika sana kama ningeyapata kwa muda huo kama ningeendelea na chuo kwani nahisi muda ambao ningetumia kusoma hadi kumaliza chuo gepu hilo kwa vyovyote lilikuwa kubwa sana kwangu kujiimarisha kimuziki lakini hata kimaendeleo yangu ya kimaisha,” anafunguka. Ben anasema tuzo alizopata tu kwa muda wote ule alioacha chuo, ni nyingi sana kiasi kwamba kuna watu wapo kwenye tasnia ya muziki zaidi ya miaka 10 hawajawahi kuzipata.

 

“Hata pesa ambazo nimeshapiga kupitia heshima ya kupata tuzo ni nyingi sana na bado napata shoo lukuki kupitia heshima hiyohiyo ya tuzo zangu. “Natambua kuwa kuna wengi hawajui kama muda huo wote nilioacha chuo kuna ‘tour’ nyingi sana za nje ya nchi nilipata, hasa baada ya kupata tuzo na kitendo cha kupewa tuzo kwa msanii mimi naona ndiyo jambo la haraka zaidi linalomtambulisha msanii ukubwa wake hasa nje ya nchi, kwani watu wa nchi za wenzetu huwa wanamfuatilia zaidi msanii kupitia tuzo alizopata na hata kukupa shoo zao huwa wengi wanajiridhisha kupitia tuzo ulizopata nchini kwenu na hata nje ya nchi.

 

“Huwa najuta tu kuachana na chuo ninapowaona baadhi ya wasanii wenzangu walioweza kufanya muziki wakisoma kama vile kaka yangu Mwana FA na wengine wengi ambao kwa pamoja waliamua kukomaa na muziki wakati huohuo wakisoma, nadhani kwa uwezo niliokuwa nikiuonyesha chuo kama nisingekata tamaa basi leo hii nafikiri tungekuwa tunazungumza na wewe haya labda nikimalizia kabisa mwaka mmoja niwe na PHD.

 

“Kwani ndoto zangu, mbali na muziki nilitamani sana siku moja nisome ili niweze kufikia kuitwa msomi mwenye hadhi ya Daktari au Profesa kabisa ila kwa sasa ni jambo ambalo naona kama limeshakuwa gumu kwani maisha yananidai mambo mengi sana, hivyo kusema nitapata tena muda kama ule niweze kurejea chuo itakuwa ngumu mno ila kama ikitokea nikaweza kufanya hivyo tena kwa kipindi hiki nitafurahi sana.” Je, maisha yanamdai kitu kipi kwa sasa Ben Pol? Tukutane kwenye toleo lijalo.
NA MUSA MATEJA

Comments are closed.