The House of Favourite Newspapers

Fei Toto Aleta Mkali Zaidi ya Makambo

ZIKIWA zimesalia wiki nne kabla ya usajili wa dirisha dogo msimu huu, kiungo wa Yanga anayekuja kwa kasi hivi sasa, Fei Toto amependekeza kusajiliwa beki wa kati na mshambuliaji tu. Kiungo huyo Mzanzibar, ameshauri usajili huo baada ya kukiangalia kikosi chao hicho katika michezo sita ya ligi ambayo wameicheza wakishinda mitano huku wakitoa sare mmoja na Simba.

 

Yanga hivi sasa inawategemea Kelvin Yondani na Andrew Vicent ‘Dante’ pekee kwenye safu ya ulinzi ya kati huku ya ushambuliaji Mkongomani, Heritier Makambo ambaye kama akibanwa hakuna mwingine wa kufurukuta.

 

Akizungumza na Spoti Xtra , Fei Toto ambaye shughuli yake Taifa Stars imemfanya kukubalika na mashabiki wengi wa soka, alisema matokeo ya michezo sita ya ligi ndiyo inatoa tathmini ya timu yao kwa maana wana kikosi imara cha kutwaa ubingwa.

 

Fei Toto alisema, nafasi ya kiungo siyo mbaya, ipo vizuri inayoongozwa na Papy Tshishimbi, Raphael Daudi na Pius Buswita ambayo anaamini kama ikitokea akiongezwa mwingine mmoja itakuwa vizuri zaidi.

 

Aliongeza kuwa, kama wakifanikiwa kuzifanyia maboresho nafasi hizo katika dirisha dogo kwa kununua ndani au nje, basi hakutakuwa na timu itakayowazuia kutwaa ubingwa huo wa ligi unaotetewa na watani wao Simba.

 

“Yanga ina kikosi imara kitakachochukua ubingwa wa ligi na hilo lipo wazi kabisa, mfano matokeo ya uwanjani kwenye michezo sita tuliyocheza ya ligi utaweza kufanya tathmini ya kikosi chetu, kizuri au kibaya.

 

“Tumelithibitisha hilo baada ya kucheza michezo sita ya ligi bila ya kufungwa zaidi ya kutoa sare na Simba pekee huku tukishinda mechi tano, hivyo ninajisikia faraja katika hilo.

 

“Ni furaha yangu kuona timu ikiendelea kupata matokeo mazuri ya ushindi katika michezo inayofuata ya ligi katika mzunguko huu wa kwanza kabla ya mzunguko wa pili ambao tutarudi tukiwa tumefanya usajili kwa kuziboresha baadhi ya sehemu, safu ya beki wa kati na mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kama Makambo,” alisema Fei Toto.

 

Fei Toto aliongeza kuwa “Nimefurahia sapoti kubwa ya mashabiki ya Stars waliofika kwenye mchezo wa kufuzu Afcon na kunipongeza kwa kiwango changu nilichokionyesha kwa dakika chache nikitokea benchi.”

 

“Ni matarajio yangu kuona nikiendelee kucheza kwa kiwango kikubwa nikiwa na Stars, pia nashukuru kwa kocha kwa kuniamini na kucheza mechi hiyo kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake,” alisema Fei Toto.

Comments are closed.