The House of Favourite Newspapers

Fei Toto, Kamusoko Wavuruga Mipango Yanga

Feisal Salum ‘Fei Toto’.

MSAFARA wa wachezaji wa Yanga jana alfajiri ulisafiri kwenda Mkoani Arusha kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya African Lyon huku ukiwaacha wachezaji wake nyota wanne.

 

Yanga wanaoongoza ligi watashuka kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wakiwa na pointi 44 wakicheza michezo 16 wakifuatiwa na Azam FC wenye 40 wakicheza 16.

 

Katika mchezo huo, Yanga watashuka uwanjani bila ya kocha wao mkuu Mkongomani, Mwinyi Zahera aliyesafiri juzi kwenda nchini Ufaransa.

Akizungumza na Championi Jumatano, Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema timu hiyo imeondoka bila ya wachezaji wake Thabani Kamusoko, Raphael Daud, Andrew Vicent ‘Dante’ wote wenye majeraha ya goti.

 

Saleh alimtaja kiungo wao mkabaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye yeye ataukosa mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano alizozipata kwenye michezo iliyopita ya ligi.

 

Aliongeza kuwa, wakati wachezaji hao wakiukosa mchezo huo, beki wao mkongwe, Kelvin Yondani atakuwepo kwenye orodha ya kikosi hicho kitakachoivaa Lyon baada ya kumaliza adhabu ya kadi tatu za njano alizozipata kwenye michezo iliyopita ya ligi.

 

“Morali ipo juu ya wachezaji wetu na timu leo (jana) alfajiri ilisafiri kwenda Arusha kwa ajili ya mchezo wa ligi dhidi ya Lyon.

 

“Maandalizi yapo vizuri ya timu kwa maana ya kikosi chetu, wachezaji wetu wanne tumewaacha Dar tofauti na Ngassa (Mrisho) anayemalizia adhabu ya kadi nyekundu ambaye tayari amekosa michezo miwili bado mmoja pekee.

 

“Wengine wapya tuliowaacha ambao ni Kamusoko, Dante na Raphael wenye majeraha ya goti na Fei Toto anayetumikia adhabu ya kadi tatu za njano, lakini wengine wote wapo fiti,”alisema Saleh.

Stori: Wilbert Molandi | Championi Ijumaa

Comments are closed.