The House of Favourite Newspapers

Fei Toto, Makambo, Aucho Watupwa Nje Yanga

0

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Yanga, wanatarajiwa kuwakosa mastaa wake sita katika mchezo wa Kombe la FA watakaocheza dhidi ya Mbao FC ya mkoani Mwanza.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya FA ambao umepangwa kuchezwa leo Jumamosi saa 10:00 Jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

 

Yanga ambao ni vinara wa ligi, wataingia uwanjani wakiwa vifua mbele wakiongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 35 katika msimamo.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, Iitawakosa wachezaji hao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeraha.

 

Mtoa taarifa huyo aliwataja wachezaji hao kuwa ni Shaaban Djuma na Yannick Bangala wataukosa mchezo huo kutokana na kuwepo katika majukumu ya timu ya taifa ya DR Congo, Heritier Makambo ambaye amerejea kwao kutokana na matatizo ya kifamilia.

 

Alimtaja kiungo mkabaji Mganda, Khalid Aucho ana kadi tatu za njano, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Denis Nkane (majeraha).

 

“Kwetu hatutaidharau timu yoyote tutakayokutana nayo mbele, katika kuelekea mchezo wetu wa FA dhidi ya Mbao tunatarajia kuwakosa wachezaji wetu sita kutokana na sababu mbalimbali, siyo kwa makusudi.

 

“Hivyo tumeelekea Mwanza kwa kazi moja pekee ambayo ni ushindi na siyo kitu kingine, kama yalivyokuwa malengo yetu ni kuchukua makombe yote tutakayoshindania,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Hata hivyo, jana asubuhi Nkane alipata nafuu na alionekana Uwanja wa Ndege akikatiwa tiketi kisha akaingia kwenye ‘pipa’ kuelekea jijini Mwanza kuungana na wenzake.

 

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alithibitisha hilo kwa kusema: “Ni kweli tutawaacha wachezaji hao sita kutokana na sababu mbalimbali kati ya hizo ni majeraha na kadi za njano, lakini tunaamini kuwa tunao tayari wachezaji watakaoziba mapengo yao.”

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply