The House of Favourite Newspapers

FIGISU NZITO MAPOKEZI YA LISSU!! KUTUA NA DEREVA WAKE

0
Tundu Lissu

WAKATI akiwa amekaa hospitalini kwa siku 82, tangu alipojeruhiwa kwa risasi Septemba 7, mwaka huu, mapokezi ya Tundu Lissu kutua Bongo yamegubikwa na figisu nzito. Lissu anapatiwa matibabu Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana. Alikumbana na mkasa huo akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma na hadi sasa amefanyiwa operesheni kadhaa.

 

MAPOKEZI

Baada ya kuimarika kiafya kutokana na matibabu anayopata, imedaiwa kuna vikao vya siri vya maandalizi ya kumpokea mbunge huyo wa Singida Mashariki pindi atakaporejea nchini. Mmoja wa viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema, maandalizi yameanza, lakini hawataki suala hilo lifahamike. “Maandalizi ni kweli yameanza lakini hiyo ni siri yetu kwa sababu tukio lililomkuta mbunge ni kubwa, hivyo ni lazima mapokezi yake yaratibiwe kwa umakini,” alisema kiongozi huyo.

Kiongozi huyo ambaye hakupenda kuweka bayana jina lake wazi kutokana na unyeti wa suala lenyewe, aliongeza kuwa: “Siku Lissu akitua atasema mwenyewe kile alichofanyiwa, na atakuwa ameongozana na dereva Simon Mohamed Bakari huyu naye ana mengi ya kusema, lakini kwa sasa vuteni kwanza subira.” Alisema kwa sasa hawawezi kuweka bayana gharama za mapokezi wala picha halisi ya mapokezi hayo itakavyokuwa kwa kuhofia kukwamishwa na watu wasiopenda suala hilo lifanikiwe.

 

MAKENE, MBOWE WATAFUTWA

Uwazi lilifanya jitihada za kuwatafuta, msemaji wa Chadema, Tumaini Makene na Mwenyekiti Freeman Mbowe kwa nyakati tofauti lakini simu zao ziliita bila kupokelewa.

 

MDOGO WA LISSU ANENA…

Mdogo wa Lissu, Vincent Mughwai, alipoulizwa na Gazeti la Uwazi kama ana taarifa yoyote kuhusu maandalizi hayo, alisema hana. Alisema licha ya kuwa hali ya kaka yake inazidi kuimarika siku hadi siku, bado hawezi kusema anarudi hivi karibuni. “Hayo maneno watu wanaongea tu mimi nakanusha hilo, ameumizwa ndiyo maana nasema hadi apone na kurejea kwenye hali yake ya kawaida itachukua muda.

 

“Lissu bado yupo Nairobi kwa matibabu jambo la kumshukuru Mungu kila siku afya yake inazidi kuimarika, japo kutembea bado itachukua muda kidogo,” alisema.

 

MPANGO WA KUMHAMISHA

Alipoulizwa kuhusu mpango wa kaka yake kuhamishiwa nje ya Nairobi kwa matibabu zaidi kama bado upo, Vincent alisema bado upo pale pale. “Mpango wa kumpeleka nje ya nchi uko palepale ila Nairobi hawajamaliza matibabu, hivyo hatuwezi kuwanyang’anya, matibabu anayopata Nairobi yakikamilika ataenda sehemu nyingine kupata rehab kwa ajili ya kunyoosha viungo ili arejee kwenye hali yake ya kawaida,”.

 

KUPONA KABISA

Katika mazungumzo yake na Uwazi, Vincent alisema kutokana na tatizo lililompata kaka yake, ni mchakato wa muda mrefu hadi arudi kwenye hali ya kawaida. “Kutembea mwenyewe bado hatua hiyo hajaifikia ila wana imani matibabu yakienda vizuri atakuwa sawa,” alisisitiza.

 

KUPUNGUA MWILI

Aliongeza kuwa kutokana na watu kuibua mjadala kuhusu kupungua mwili wakihisi labda ni msongo wa mawazo, alisema hali hiyo imetokana na tatizo alilopata. Vincent alisema ilifikia hatua
hata chakula analishwa kwa mirija ukichanganya na matibabu anayofanyiwa, haoni cha ajabu afya yake kutetereka. “Ukweli ndugu yetu ameumia sana, unadhani tatizo kama hilo kumpata mtu ni jambo dogo…ni lazima akonde, mfano ndiyo wewe umepatwa na tukio hilo lazima liathiri hata afya yako, ila sioni cha ajabu, muhimu ni kumuombea Mungu apone,”aliongeza.

 

ATOA NENO KWA SERIKALI

Alitoa dukuduku kuwa serikali ilitangaza italipia gharama za matibabu iwe ndani au nje ya nchi, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika zaidi ya michango ya awali iliyotoka bungeni. “Tunaona kama danganya toto sababu hadi sasa hivi serikali haijachukua hilo jukumu, huyu ni mbunge bosi wake ni spika… sisi kama familia tunashangaa kwa nini hilo halijafanyika na waliahidi, pia ukiacha hilo, sheria ya viongozi wote kwa muda ambao yuko pale kwenye matibabu inatakiwa kila siku awe analipwa posho yeye na mtu anayemuuguza, lakini hakuna. “Cha ajabu viongozi wanaoenda kumuona wengi ni Chadema. Kwa nini hatembelewi na watu wote? Kwa nini hapewi haki kama wengine?,” alihoji. Aliongeza kuwa, “tumezoea kuona watu wakipata matatizo viongozi wakubwa wanaenda kumuona wakiwemo mawaziri, rais lakini sivyo Lissu.”

FULL Stori ipo hapa

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leave A Reply