The House of Favourite Newspapers

Flora Lauwo: Dada wa Kazi Hagusi Nguo za Mume Wangu


STORI: IMELDA MTEMA | RISASI JUMAMOSI| MPAKA HOME

ANAITWA Flora Godwin Lauwo. Kwa wale wanaomsoma leo kwa mara ya kwanza, Flora ni mtangazaji maarufu wa Kipindi cha Flora Shoo kinachoshughulika na watu maarufu na kutangaza urembo.

Pia ni mtangazaji wa Kipindi cha Nitetee Sauti ya Mnyonge ambacho kinashughulika na watu wenye matatizo katika jamii. Vipindi vyote hivyo vinarushwa kupitia runinga ya Channel Ten lakini mwenyewe makazi yake ni jijini Mwanza.

Kutokana na msaada wake katika jamii, hivi karibuni, Flora alitangazwa kuwa miongoni mwa wanawake waliochaguliwa kuwa Malkia wa Nguvu walioandaliwa na Kituo cha Runinga cha Clouds cha jijini Dar.

Safu ya Mpaka Home ambayo imeondokea kupendwa na wasomaji kutoka pande mbalimbali za nchi, iliona ni vyema kumtafuta mwanadada huyu ili kuyajua maisha yake ya familia. Akiwa nyumbani anaishije,  anafanyaje, anawezaje…

Mpaka Home: (baada ya salamu) Flora, kwanza hongera sana kwa jitihada zako za kuisaidia jamii ya Watanzania. Kupitia wewe, watu wenye matatizo mbalimbali wamekuwa wakipata misaada.

Flora: Ni kweli, nashukuru sana kwa kulitambua hilo.

Mpaka Home: Flora, watu wamekuwa wakikuona katika runinga kupitia vipindi vyako viwili ambavyo ni maarufu sana. Lakini wengi wangependa kujua maisha yako ya nyumbani…eee…kwanza kabisa umeolewa, una watoto au  mtoto?

Flora: Nimeolewa na nina watoto wawili, mmoja mwanamke…

Mpaka Home: Oke! Maisha yako ya nyumbani kwa ujumla yapoje? Unadeka, unafanyiwa kila kitu kwa sababu wewe ni maarufu au vipi?

Flora: No! Maisha yangu nyumbani ni ya kawaida sana. Mimi nikiwa nyumbani nakuwa mama kama wamama wengine unaowajue wewe.

Mpaka Home: Ina maana na wewe huwa unavaa kanga, unaosha vyombo, unafua nguo, unapika chakula?

Flora: Kila kitu. Ukinikuta nyumbani nakuwa si Flora yule wa Flora Shoo au Nitetee Sauti ya Mnyonge. Nakuwa ni Flora mama wa familia.

Mpaka Home: Eee…majukumu yako ukiamka asubuhi ni yapi kama mama wa familia?

ANAFANYA NINI ANAPOAMKA ASUBUHI?

Flora: Kwanza ni kuwaandaa watoto waende shuleni kwa kuhakikisha wameoga, wamekunywa chai, nguo zao safi na madaftari yako sawa. Lakini pia ni kuhakikisha mume wangu naye anapata mahitaji yote kabla hajaondoka kwenda kibaruani.

Mpaka Home: Ni chakula gani haipiti siku ndani kwako bila kukipika?

Flora: Mimi napenda sana ndizi na nyama au kitu kingine.

Mpaka Home: Kwa kawaida nani anatangulia kulala kati yako na mume wako? Maana unaonekana uko bize sana wewe.


Flora:
Mume wangu ndiye anayetangulia kwenda kulala na pia yeye huchelewa kuamka. Si unajua mimi mama wa familia. Kwa kawaida mimi naamka saa kumi na mbili asubuhi.

Mpaka Home: Ukiwa kama mke wa mtu ni jambo gani ambalo limekuwa likiwatofautisha kimtazamo wewe na mume wako?

Flora: Mh! Ni chakula. Yeye anapenda sana ugali, mimi napenda sanasana ndizi.

KUHUSU DADA WA KAZI

Flora: Una dada wa kazi?

Flora: Ndiyo ninao. Unajua pia naishi na watoto wengine 12 ambao nawasaidia kimaisha. Kwa hiyo lazima dada wa kazi kuwepo.

Mpaka Home: Dada wa kazi unamtegemea kwa kiasi gani ndani ya nyumba? Ni msaidizi wa kazi za ndani au ndiyo mama mwenye nyumba?

Flora: (kicheko) kwangu dada wa kazi ni msaidizi tu. Hana nafasi ya kutawala.

NGUO ZA FAMILIA

Mpaka Home: Huwa anafua nguo za familia?

Flora: Mara mojamoja.

Mpaka Home: Hizo mara mojamoja, huwa anafua nguo zote za mista mpaka ‘kufuli’?

Flora: (kicheko) hilo haliwezi kutokea. Ninaposema anafua mara moja ni nguo zangu tu. Mimi nguo zote za mume wangu hazina uhusiano wowote na dada wa kazi na sitaki aziguse.

NANI ANAPIKA CHAKULA?

Mpaka Home: Je, vipi kuhusu chakula cha familia, huwa kinapikwa na nani nyumbani kwako?

Flora: Huwa napika mwenyewe, ikitokea kuna shughuli ambayo itanichelewesha kurudi nyumbani nasaidiwa na wadada.

Mpaka Home: Kuna akina mama wakiwa majumbani wanapenda kuangalia tamthiliya, filamu na kusoma magazeti. Wewe siku ukishinda nyumbani unapenda kufanya nini?

Flora: Huwa napenda sana kuangalia mambo yote ya nyumbani, wapi kuna jambo la kurekebisha, wapi kuna jambo la kuweka sawa. Yaani nadili zaidi na maisha ya familia na matatizo yake, hasa usafi. Mimi napenda sana usafi, yaani napenda sana.

Mpaka Home: Mtandao ya kijamii je, huangalii?

Flora: Naingia kama sehemu ya kazi na si kutafuta nani leo kafanya nini na itakuaje! Hiyo kwangu hapana!

U-MALKIA WA NGUVU WAMCHANGANYA

Mpaka Home: Kituo cha Runinga cha Clouds kimekutangaza wewe kuwa miongoni mwa wanawake Malkia wa Nguvu kwa mwaka 2017-18, ulijisikiaje?

Flora: Kwanza nilichanganyikiwa nilipoambiwa maana nilikuwa msibani. Lakini pia  nilifurahi sana kuona kumbe mchango wangu ni mkubwa katika jamii kiasi cha kuonekana nafaa kuwa Malkia wa Nguvu… Da! Namshukuru sana Mungu lakini pia nawashukuru sana waandaaji maana nilipokea meseji nyingi sana.

Mpaka Home: Dada Flora usituchoke tena siku nyingine tukije, sawa?

Flora: Karibuni sana, hapa ni kama kwenu jamani.

Comments are closed.