The House of Favourite Newspapers

Frank Mwakajoka Awaomba CCM, CUF Kumpigia Kura

0

MGOMBEA ubunge jimbo la Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema) amewaomba wananchi wa mji huo uliopo mkoani Songwe kumpigia kura za kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, bila kujali itikadi zao za kisiasa.

 

Mwakajoka ambaye pia ni Mbunge aliyemaliza muda wake, alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi wa Maporomoko mjini humo na kuwasisitiza kulinda amani.

 

Alisema licha ya kwamba yupo Chadema, anawatumikia wananchi wa Tunduma ambao ni wanachama wa CCM na vyama vingine.

 

“Nataka niwaambie mama wa Chadema akikosa maji vilevile wa CCM anakosa maji kwa sababu wanaishi eneo moja la Tunduma, vivyo hivyo mtoto wa kada wa Chadema akikosa dawati shuleni pia mtoto wa kada wa CCM anakosa dawati, kwa maana hiyo maendeleo hayana vyama,” alisema.

 

Aidha, alitoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kudumisha amani ili kuondoa hofu iliyosheheni kwa wananchi wa jimbo hilo.

 

Alisema ili kuondoa hofu hiyo ambayo imesababisha wananchi kuogopa kuhudhuria mikutano ya kampeni, ni vyema vyombo vya dola kukaa pamoja na wanasiasa na kuzungumza namna ya kuboresha amani katika mji huo.

 

“Tukae tuzungumze kwa pamoja kwa sababu CCM na Chadema wote tunalia matatizo yetu pamoja, uchaguzi huu usiwe uchaguzi wa kutugawa, uwe uchaguzi wa amani na wenye kujenga umoja wetu.

 

“Kama mnakumbuka wananchi, nikiwa diwani tumefanya kazi pamoja na hata nilipokuwa mbunge tumepata maendeleo pamoja na matatizo yetu tumeyatatua pamoja, huu sio wakati kutugawa ni wakati wa kuzungumza juu ya amani yetu,” alisema.

 

 Alisema wananchi wengi wamekuwa wakikimbilia maporini na wengine kuogopa kuhudhuria mikutano ya kampeni kwa kuogopa kukamatwa na polisi kutokana na madai ya mauaji ya kijana aliyekuwa kada wa CCM mkoani humo.

NA MWANDISHI WETU, TUNDUMA

Leave A Reply