The House of Favourite Newspapers

Gari la Waziri Nusura Liue Mwendesha Baiskeli

MKAZI wa Kata ya Ngogwa, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Marco Charles (48), amenusurika kifo baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili STL 2777 lililokuwa limembeba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  wakati akitokea mkoani Kagera kutekeleza majukumu yake ya kikazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 27 majira ya saa 10.30 jioni, eneo la Ngogwa barabara ya Masumbwe kuelekea Kahama na kwamba gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Jumanne Ally (45), lilimgonga mwendesha baiskeli huyo na kumsababishia majeraha kichwani, mkono wa kulia na shingoni.
Haule aliongeza kuwa, kutokana na ajali hiyo, majeruhi huyo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama na anaendelea na matibabu.
Wakati huohuo, Kamanada Haule alisema Agosti 26 majira ya saa 9.53 usiku mtaa wa Nyasubi katika baa ya Chillar Kahama mjini, Emmanuel Philimon (39), mlinzi wa baa hiyo, alijeruhiwa kwa kupigwa na risasi katika mapaja yote mawili na George Nyamhanga (41), ambaye ni mhasibu wa baa hiyo.
Ilielezwa kuwa alifanya hivyo wakati akisaidia kuwazuia watuhumiwa watatu waliokuwa wamekamatwa kwa tuhuma za kumjeruhi mlinzi mwingine wa baa hiyo, Baharia Athumani (25), mkazi wa Nyasubi aliyepigwa na chupa.
Kamanda alisema chanzo cha tukio hilo ni uzembe wa mtumiaji wa bastola hiyo yenye namba za usajili 785819 CAR Na. 00104206 aina ya Browning, kutochukua tahadhari za kutosha wakati akifyatua risasi hewani ili kuwatuliza watuhumiwa watatu wasitoroke. Watuhumiwa hao walikuwa wamekamatwa kwa kumpiga chupa mlinzi huyo.
Kamanda alisema mtuhumiwa alikamatwa na silaha hiyo kwa uchunguzi zaidi na kwamba majeruhi wamelazwa katika hospitali ya mji wa Kahama na hali zao zinaendelea vizuri.

Comments are closed.