The House of Favourite Newspapers

Watanzania 27 Wasio na Vibali Wakamatwa Mombasa

Kamanda wa polisi wa Mombasa,  Johston Ipara

MAMLAKA ya usalama huko Mombasa, Kenya,  inaendelea na mipango ya kuwarejesha nchini Watanzania 27 wanaoshikiliwa na polisi katika kituo cha Likoni, Mombasa, wakiwa hawana vibali vya kuishi nchini huo.

Kamanda wa polisi wa Mombasa, Johston Ipara, ameeleza kwamba Watanzania hao ni miongoni mwa wahamiaji wengine kutoka Congo, Somalia, Eritrea na Ethiopia ambao walikamatwa kwa kutokuwa na vibali vya kusafiria.

Ingawa watu wa Afrika Mashariki huwa wanaweza kutumia kitambulisho cha taifa  kuingia na kutoka katika nchi zote tano za Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Kenya, Burundi, Rwanda, Tanzania na Uganda, Ipara alisema watu hao hawakuwa hata na vitambulisho vya taifa.

Raia hao walikamatwa katika ukaguzi ambao umekuwa ukifanyika  nchi nzima. Hata hivyo,  ilionekana kuwa hapakuwa na mwongozo mzuri katika ukaguzi huo kuhusu hatua zilizochukuliwa na polisi na utawala.

Jumatano iliyopita, baadhi ya watu hao walipelekwa mahakamani lakini kesi yao ikafutiliwa mbali. Wakili wa serikali,  Henry Nyakweba, aliiambia mahakama kuwa watapitia upya mashtaka ya watu hao kuwepo nchini Kenya bila kibali.

Tangu mwezi Mei mwaka huu, serikali ya Kenya ilianza udhibiti kwa wageni wasiokuwa na vibali hasa wale wanaofanya kazi nchini humo.

Comments are closed.