The House of Favourite Newspapers

GGML yabeba tuzo kampuni bora ya madini 2021

0

 

Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia miradi endelevu kwa upande wa Ghana & Tanzania, Simon Shayo (katikati) akipokea moja kati ya tuzo kadhaa zilizotolewa kwa GGML kutoka kwa Rais wa mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete (kushoto) na Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko (kulia) katika Mkutano wa nne wa kimataifa wa Uwekezaji kwenye sekta ya madini uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya dhahabu Geita (GGML) imetunukiwa tuzo ya kuwa kampuni bora inayoendesha shughuli za uchimbaji wa madini nchini kwa mwaka 2021.

Kampuni hiyo imetunukiwa tuzo hiyo hivi karibuni katika Mkutano wa nne wa Kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini uliofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliofunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango na kufungwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ulikuwa na kauli mbiu isemayo; ‘Mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya madini’

Kauli mbiu hiyo inaakisi azma dhabiti ya serikali ya awamu ya sita ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha kuvutia mitaji ya wawekezaji katika fursa zilizopo kwenye sekta za madini na nyingine uchumi.

Akizungumzia katika mkutano huo, Makamu Rais wa Kampuni ya Anglogold inayomiliki na kuendesha mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML), Simon Shayo alisema kampuni hiyo inaona fahari kubwa ya kuendelea kuwa sehemu ya musktakabali wa maendeleo ya Tanzania kwa miaka 20.

Alisema GGML imekuwapo hapa tangu mwaka 2000 ikizalisha dhahabu, ni mgodi ambao kwa sehemu kubwa ya miaka ambayo umekuwa ukifanya kazi umekuwa kinara kwa yale maeneo ya msingi hasa kwenye uchangiaji wa mapato ya serikali.

“Kwa mara nyingi ikiwemo mwaka wa fedha uliopita tulitambuliwa kama mlipa kodi mkubwa kwa sekta ya madini, lakini mlipa kodi wa pili kwa sekta zote,” alisema.

Kampuni hiyo ambayo ilitoa zaidi ya Sh milioni 90 kufadhili wa mkutano huo, imeajiri zaidi ya wafanyakazi 5,600 na asilimia 97 ya hao ni watanzania na asilimia 80 ya menejimenti yote ya GGML ni Watanzania.

“Pia asilimia 85 ya fedha ambayo tunatumia kwa manunuzi inabaki hapa Tanzania, kwamba inanunua bidhaa zilizotengenezwa hapa Tanzania au lah ni jambo lambalo wote tuna fursa ya kufanyia kazi lakini kwa vyovyote hatuwezi kukata tamaa kwa sababu tupo mahala pazuri.

“Niendelee kushukuru kwa kampuni yetu kupewa fursa ya mshiriki lakini pia mmoja wa wadhamini wakubwa kwenye maonesho haya.

“Niahidi wakati wote ambao kampuni itakuwa hapa Tanzania, tutakuwa si wadau na wabia wa serikali kwenye maendeleo kama ambavyo tumeonesha kwa uwekezaji wetu kwenye maeneo yanayozunguka mgodi wetu ambapo kwa kila mwaka tunatumia kati ya Sh bilioni 9 hadi 10 kwa uwekezaji kwenye jamii ambayo inajulikana kama CSR,” alisema.

Mbali na tuzo hiyo, GGML pia ilipata tuzo ya kampuni inayoimarisha ushiriki wa nchi na wananchi katika mnyororo wa uchumi wa madini nchini, tuzo ya kampuni bora inayowajibika vema kwa jamii (CSR), tuzo ya kuwa kampuni inayozingatia masuala ya mazingira na usalama na mshindi wa pili katika kipengele cha mchango wa kampuni kwa mapato ya Serikali kwenye sekta ya madini.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wageni zaidi ya 1200 kutoka ndani na nje ya nchi.

 

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply