The House of Favourite Newspapers

GHETTO KIDS: KUTOKA MATOPENI MPAKA MAMTONI!

0
Ghetto Kids wakiweka pozi.

 

Moyo wa subira, juhudi na ubunifu ndiyo kila kitu katika maisha ya mtu mwenye shauku ya mafanikio. Hicho ndicho kilichowafikisha watoto wa Ghetto Kids kwenye kilele cha mafanikio barani Afrika na duniani. Kwa sasa watoto hawa wameula, wanaogelea kwenye fedha. Dunia inawajua na wana mvuto wa kipekee wanapokabidhiwa jukwaa kufanya mambo.

 

Ghetto Kids, hatari.

 

KAMA UTANI VILE

Ghetto Kids walianza kuonekana kama utani vile kwenye mitandao ya kijamii wakicheza muziki kwa staili ya aina yake kwa kutumia Wimbo wa Maria Rosa wa mwanamuziki, Eddy Kenzo wa Uganda, tena kwa staili ya kuchekesha na kivituko zaidi.

Walikuwa wakicheza muziki wa video kali zilizotoka na zilizoonekana kuwashika mashabiki wengi duniani, hasa kwa kuzingatia jina la mwanamuziki husika aliyeachia ngoma yake.

 

Ghetto Kids wakiwa na French Montana.

 

COVERS ZA NGOMA KALI

Mbali na kufanya covers (kurudia video za nyimbo kwa staili tofauti) za video za Kenzo pia walifanya za ngoma kali za mastaa wakubwa duniani kama Sorry ya Justin Bieber, Make Am ya Patoranking na nyingine kibao huku wakitamaniwa na mastaa wengi kama Nicki Minaj na French Montana aliyediriki kusema kuwa wanajua kucheza zaidi ya Chris Brown.

Nikiri kuwa, nilipoona video zao kwa mara ya kwanza kwenye mitandao ya kijamii, nilivutiwa na staili yao hiyo ya kucheza muziki mitaani kwa mpangilio wa aina yake, wakionekana wachafu kwa kujigaragaza kwenye mavumbi na matope.

 

Ghetto Kids.

 

MAISHA HALISI

Kilichonivutiwa zaidi kwa watoto hawa ni namna walivyoakisi mazingira ya Kiafrika na maisha halisi ya sehemu kubwa ya bara hilo. Mavazi yao yanayowaonesha kama vile wanatoka familia zisizokuwa na uwezo kiasi cha kuvaa mavazi yaliyochanika na kuwekewa viraka kuonesha maisha ya familia nyingi ambazo hazina uwezo wa kuwanunulia watoto wao nguo mpya.

Ghetto Kids wakiwa katika picha ya pamoja.

 

GETTO KIDS NI AKINA NANI?

Kadiri siku zilivyosonga ndivyo walivyozidi kuwa gumzo mitandaoni. Hapo ndipo nilipopata shauku ya kutaka kujua Getto Kids ni akina nani?

Jina kamili la kundi lao ni Triplets Ghetto Kids kutoka nchini Uganda. Kundi hilo linaundwa na watoto ambao wote wamezaliwa baada ya mwaka 2000 (yupo aliyezaliwa 2010). Baadhi yao ni pamoja na Ada, Patricia, Ashley, Man King, Ronnie, Isaac, Fredy, Nyangoma, Kokode na wengineo. Mwaka 2014 walipata pigo la kufiwa na mwenzao kwenye ajali ya baiskeli aliyeitwa Alex.

 

Patricia.

 

 

WANAMILIKIWA NA EDDY KENZO

Kwa mujibu wa mwanamuziki wa Uganda anayelimiliki kundi hilo, Eddy Kenzo, watoto hao aliwakusanya mitaani wakiwa hawajuani.

Wengi wao ni watoto waliokulia maisha magumu ya mitaani kutokana na familia zao kutokuwa na uwezo wa kuwapeleka shuleni au kuwapa malezi bora. Pia baadhi yao ni yatima.

Kenzo anasema kuwa, tangu kuanza kwa safari yao ya ku-dance mavumbini na kwenye matope, walionekana watoto wa mitaani wasiokuwa na mwelekeo wa kimaisha.

Eddy Kenzo.

 

KENZO AONA TOBO

Ilibidi kutumia staili hiyo baada ya kubaini kuwa, kuna tobo au mwanya ambao wengi hawauoni. Kwamba, staili hiyo inaakisi uhalisia wa familia zilizo nyingi za Kiafrika na kwamba ingepata mvuto kwa sababu ni staili ya kipekee.

Kenzo ni mwanamuziki mkubwa nchini Uganda hivyo anasema si kweli kwamba alishindwa kuwapiga sopusopu na pamba kali za kisanii, lakini alitaka waonekane hivyo kuleta utofauti na ndiyo maana wakiwa nje ya steji au kazi yao hiyo wanaonekana ni watoto wa matajiri f’lan.

WAPENYA ULAYA, MAREKANI

Mdogomdogo, Ghetto Kids walianza kuiteka Uganda, Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla. Baadaye walivuka mipaka ya Bara la Afrika. Wakaanza kulamba shoo mabara mengine, wakialikwa kwenye matamasha makubwa ya Ulaya na Amerika (Marekani).

Sasa maisha ni bomba. Wanatamba hadi Hollywood, Marekani. Mwaka huu walipafomu kwenye moja ya steji kubwa za kimataifa na kutumbuiza mbele ya umati mzito wenye macho ya wasanii wakubwa na watu mashuhuri duniani kwenye tuzo kubwa za BET za Marekani.

French Montana.

 

FRENCH MONTANA AWAONA

Katika harakati zao hizo, walionekana na staa mkubwa wa muziki wa Marekani, French Montana. Staa huyo alipowaona watoto hao, aliamua kuwatumia katika tour (ziara za kimuziki) sehemu mbalimbali duniani.

Mbali na hilo, pia wamekuwa wakipata coverage (kuandikwa) kwenye majarida makubwa ya burudani kama Vibe la Marekani.

French Montana amewatumia pia kwenye video ya ngoma yake kali ya Unforgettable aliyomshirikisha Rapa Swae Lee ambayo imetazamwa na zaidi ya watu milioni 170 kwenye Mtandao wa YouTube.

DOLA LAKI 1 KUWASAFIRISHA

Kupitia Jarida la Vibe, French Montana anasema kuwa, baada ya kuwaona watoto hao kwenye mitandao ya kijamii, alitumia kiasi cha dola laki moja (zaidi ya Sh. milioni 220) kuwasafirisha kutoka Uganda hadi Marekani kwa ajili ya kuwatumia kwenye kazi zake za kisanaa.

“Stori yao ni ya aina yake, jinsi walivyokutanishwa na namna wanavyoishi pamoja,” anasema French mwenye asili ya Morocco na kuongeza;.

 “Unforgettable (ngoma yake) haikuwa ngoma yangu pekee. Nilipenda kuwaona watoto hawa wakiwa na furaha. Ukweli ninapenda kuwaona sasa wana furaha.”

 

Na Sifael Paul | GAZETI LA IJUMAA

 

VIDEP: Mama Aliyekutwa Uchi Azua Balaa

Leave A Reply