GHOROFA ANALOJENGA HARMONIZE LASHTUA

Rajab Abdul ‘Harmonize’

DAR: Ghorofa analojenga Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ limeshtua wengi ni baada ya kuonekana katika hatua za awali huku wengi wao wakidai kuwa litakapomalizika litakuwa ni la kifahari.  

 

Gazeti hili la Amani limefanikiwa kulinasa ghorofa hilo ambalo ni mjengo wa maana maeneo ya Madale Jijini Dar es salaam. Baada ya kulinasa waandishi walifanikiwa kulithaminisha ghorofa hilo kwa kulitembelea na kulandalanda ndani na nje ili kubaini ukubwa wa jengo hilo ambalo halijaisha.

 

AMANI NDANI YA MJENGO

Baada ya Amani kutinga katika eneo la tukio na kushuhudia ghorofa hilo, lilifanikiwa kuzungumza na mmoja wa majirani wa eneo hilo ambapo alikiri kumuona kila mara mama mzazi wa Harmonize akisimamia ujenzi wa mjengo huo.

 

“Hii nyumba kweli ni ya Harmonize kwa sababu mara nyingi hapa tunamuona mama yake anakuja kuangalia maendeleo yakoje na Harmonize huwa anakuja mara mojamoja nadhani ni kwa sababu ya ubize alionao.

“Tunampongeza kwa sababu jambo analolifanya ni la maana sana ni wasanii wachache wenye akili kama yake wengi wao huishia kununua magari na kubadilisha tu wanawake, wanasahau kwamba kuna siku unaweza ukapata na siku nyingine ukakosa,” alisema jirani huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

 

MLINZI ACHARUKA

Wakati Amani likiwa eneo hilo huku likipata picha za mjengo ghafla alitokea baba aliyejitambulisha kuwa ni mlinzi na kucharuka kwa nini picha zinapigwa eneo hilo bila ruhusa yake. “Nyie ni wakina nani na kwa nini mnapiga picha bila ruhusa yangu? Kama ni waandishi wa habari kwa nini hamjampigia simu Harmonize badala yake mnavamia tu.

 

“Msione naongea kwa ukali ni vile tu hamumjui huyu Harmonize ni mkali balaa, mmtanisababishia matatizo akijua anaweza kunifukuza kazi, ebu ngoja nimpigie kwanza mama yake ili ajue kwamba mpo hapa,” alisema mlinzi huyo na kupiga simu.

Baada ya kumpigia mama huyo alimtaka mlinzi kuwapa waandishi simu na kuzungumza nao ambapo alibaki akilalalama kwa nini wamefika eneo hilo. Kutokana na kulalamika huko mama huyo alimpigia simu Harmonize na kumweleza ambapo mwanamuziki huyo naye alimpigia mlinzi na kutaka kuongea na waandishi.

 

Harmonize baada ya kupewa simu aliongea na waandishi kwa ukali kisha akakata simu. “Ehh! nyie ni kina nani na mmefuata nini kwenye nyumba yangu nani kawaruhusu kuingia na kuanza kupiga picha…,” alimaliza Harmonize.

Stori: Memorise Richard na Neema Adrian, Amani.

Toa comment