The House of Favourite Newspapers

Global Publishers Yazindua Jipange na Pepa Kwa Kishindo

Mitihani ni miongoni mwa mambo yanayoogopwa na wanafunzi wote, wa ngazi zote! Kuanzia wanafunzi wa shule za msingi, sekondari mpaka vyuo, wanaposikia kuna mitihani, huchanganyikiwa, hujawa na hofu na wengi hukata tamaa!

 

Wakati mwingine mwanafunzi anaingia kwenye chumba cha mitihani akiwa amejiandaa vya kutosha lakini ile ‘homa’ ya mtihani, inamfanya achanganyikiwe na kukosa hata yale maswali ambayo alikuwa anayajua vizuri.

 

Kwa wanafunzi wa shule za kata na nyingine zilizopo vijijini, wao changamoto inakuwa kubwa zaidi kwa sababu hawapati majaribio ya kutosha kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani wa mwisho kutokana na uhaba wa walimu na vifaa vingine vya kujifunzia.

 

Kwa kuzingatia hilo, Kampuni ya Global Publishers inayochapisha magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani, Championi na Spoti Xtra, imekuja na ‘project’ mpya iitwayo Jipange na Pepa ambayo itakuwa ni maalum kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi (hasa wa sekondari) kuelekea kwenye mitihani yao ya mwisho na kupunguza ile ‘homa’ ya mitihani.

 

Project ya Jipange na Pepa imeanza rasmi leo Jumatatu ya Noemba 4, 2019 kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda ambako kutakuwa na mtihani wa kwanza na itaendelea kila siku ambapo Jumanne utafanyika uzinduzi rasmi kwenye ofisi za Global Group zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

 

Jopo la walimu wazoefu, wenye mbinu bora za ufundishaji na utungaji wa mitihani, watakuwa wakitunga mitihani ya masomo mbalimbali kwa kuzingatia ‘format’ ya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne (NECTA), na maswali yatakuwa yanachapishwa kwenye Magazeti Pendwa kuanzia Jumatatu mpaka Jumamosi, huku majibu ya kila mtihani yakitolewa kwenye toleo linalofuatia la gazeti husika.

 

Hii itawasaidia wanafunzi kuizoea mitihani, kuelewa namna maswali yanavyoweza kutungwa kutokana na ‘topic’ walizozisoma na kuelewa maeneo ambayo maswali huwa yanatoka zaidi. Lakini pia itawasaidia walimu, hasa kwenye zile shule zenye walimu wachache ambapo kwa kutumia mitihani itakayokuwa inachapishwa, watakuwa na uwezo wa kuwapima wanafunzi wao kwa urahisi na kuangalia maeneo ambayo yana udhaifu.

 

Hata kwa wale wanafunzi ambao kwa sababu ya uhaba wa walimu hujikuta wakishindwa kumaliza topic zote kama mtaala unavyotaka, watakuwa na uwezo wa kuelewa namna ya kujibu maswali hata yale ambayo hawajafundishwa kwa kusubiri kuona namna majibu ya swali husika yanavyotakiwa kuwa.

 

Si hivyo tu, itawasaidia hata wazazi wanaozingatia maendeleo ya watoto wao ambapo kwa kutumia mitihani itakayokuwa inachapishwa, watakuwa na uwezo wa kuwasimamia watoto wao waifanye, kisha baada ya hapo wanasubiri toleo linalofuata kutazama majibu na kupima uelewa wa watoto wao.

 

Kwa kuanzia, masomo yatakayoangaziwa na majina ya magazeti husika ni kama ifuatavyo: BIOLOGY (Ijumaa Wikienda linalotoka siku ya Jumatatu), GEOGRAPHY (Uwazi, Jumanne), MATHEMATICS (Risasi Mchanganyiko, Jumatano), ENGLISH, KISWAHILI (Amani, Alhamisi), HISTORY, CIVICS (Ijumaa) na PHYSICS, CHEMISTRY (Risasi Jumamosi).

 

Kwa siku ambazo zina masomo mawili, walimu watakuwa wakitunga mitihani ya masomo hayo kwa kubadilishana kwa lengo la kuhakikisha kila somo linapata nafasi ya kutosha.

 

Kwa ufafanuzi zaidi, endelea kusoma magazeti ya Global Publishers, tembelea mtandao wa Global Publishers au unaweza kupiga simu namba 0719401968 kwa maelezo zaidi! Jipange na Pepa!

Comments are closed.