The House of Favourite Newspapers

MY GOD KUNA NINI JAMANI?

DAR ES SALAAM: My God (Mungu wangu) kuna nini? Ndivyo walivyozungumza kwa uchungu baadhi ya wakazi wa Mbeya baada ya kutokea kwa ajali nyingine iliyosababisha vifo vya Wanajeshi zaidi ya 10.

Wanajeshi hao wa Jeshi la Kulinda Taifa (JKT) walipata ajali hiyo katika eneo la Igodima jijini Mbeya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi wa Chuo cha Kikuuu cha Dar es Salaam wakiwa kwenye maombolezo ya manafunzi wenzao pamoja na wafanyakazi wa chuo hicho

waliofariki kwa ajali.

“Mungu wangu, kuna nini jamani? Juzi tu tumetoka kusikia ajali ya wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, leo (juzi) tena ajali nyingine imetokea, yaani kwa kweli ni huzuni mpya katika sikukuu hii ya Idd, familia zao ndugu jamaa na marafiki watakuwa kwenye wakati mgumu sana sikukuu hii,” alisema Mwakipesile Mkuu, mkazi wa Igodima jijini Mbeya.

Aidha, Risasi Jumamosi lilizungumza na mshuhuda mbalimbali wa ajali hiyo ambao walisema hakuna sababu ya kumtafuta mchawi kwani dereva wa gari hilo ndiyo chanzo cha ajali.

“Hakuna sababu ya kutafuta mchawi. Huu ni uzembe wa dereva, alikuwa spidi sana halafu hakuwa na tahadhari yoyote,” alisema mmoja wa mashahuda.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Mkoa wa Mbeya, ACP Musa Athuman alisema ajali hiyo ilitokana na uzembe wa dereva pamoja na ubovu wa gari.

Licha ya kutotaja idadi kamili ya vifo vilivyotokea katika ajali hiyo, kamanda Musa alisema vifo hivyo vinatazamiwa kuwa zaidi ya kumi.

MAJONZI CHUO KIKUU

Wakati ajali hiyo ikitokea juzi majira ya mchana, upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam machozi, huzuni na simanzi vilitawala kwa takriban siku nne (saa 96) wakiomboleza msiba wa wanafunzi wenzao hao pamoja na wafanyakazi wa chuo hicho waliofariki kwa ajali.

Wanafunzi wa chuo hicho; Maria Godian Soko na Steven Sango wakiwa na muuguzi Jonathan Bashuba Lung’ando pamoja na dereva James Josephat Kagwebe, walipoteza maisha usiku wa Juni 11, mwaka huu baada ya gari la wagonjwa la chuo hicho kupata ajali majira ya saa tatu usiku katika eneo la Riverside, Ubungo jijini Dar.

Mara baada ya taarifa hizo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii usiku wa tukio, wanachuo pamoja na walimu wao walijawa na huzuni kutokana na jinsi walivyokuwa wakishirikiana kwa pamoja na wapendwa wao hao.

“Ni zaidi ya simazi. Kwa kweli kuanzia ile siku ya kwanza tulipopata tarifa, hadi leo (juzi) tunapoaga hakuna mtu aliyekuwa katika hali ya kawaida.

“Unajua wote hawa ni watu ambao tunaishi nao kwa ukaribu, wanachuo wenzetu pamoja na dereva wetu na hata muuguzi ni watu ambao tulikuwa tukiishi nao kwa upendo,” alisema mwanachuo mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ally.

Risasi Jumamosi lililokuwepo chuoni hapo wakati wa shughuli

ya kuaga wanafunzi pamoja na wafanyakazi wa chuo hicho, lilishuhudia umati mkubwa wa watu katika Ukumbi wa Nkrumah wakiwa kwenye hali ya majonzi.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuwaaga wapendwa hao, mshereheshaji wa tukio hilo, Prof. Aldin Mutembei alisema

msiba huo umewagusa wengi na pia alitoa salamu za rambirambi kutoka kwa Mkuu wa Chuo, Dk Jakaya Kikwete na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof Joyce Ndalichako.

Aidha, wakati umati wa watu ukiwa unaomboleza, mapya yaliibuka katika ajali hiyo yakihusisha eneo lililotokea ajali kwa kudaiwa kuwa ni hatari na zimekuwa zikitokea ajali nyingi.

“Lile eneo ni hatari sana, inabidi kwa kweli vyombo vinavyohusika vilitazame lile eneo ili kuhakikisha ajali zinakuwa hazitokei,” alisema John Kigoa, mkazi wa Riverside jijini Dar.

Aidha, mkazi mwingine wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Shaban Ngoa, alilihusisha eneo hilo na imani za kishirikina akidai pamekuwa pakitokea ajali nyingi ambazo nyingine huwa haziripotiwi na vyombo vya habari.

“Yani hapa kuna Noah iliwahi kuua dereva mmoja, kuna mwandishi Adolf Balingilaki naye aligongwa na gari, kuna fuso liliwahi kugonga msingi yani kwa kweli ni matukio mengi mimi nahisi kuna mambo ya Kiswahili pale,” alisema

 

Comments are closed.