The House of Favourite Newspapers

GUARDIOLA: TUNACHUKUA UBINGWA MBELE YA MOURINHO LEO

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola.

KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema atapambana kuhakikisha timu yake leo inatangaza ubingwa wa Ligi Kuu England mbele ya Manchester United inayonolewa na Jose Mourinho.

Leo Jumamosi saa 1:30 usiku kwa saa Afrika Mashariki, Man City itacheza na Man United nyumbani kwenye Uwanja wa Etihad, na wakishinda watatangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu England.

 

Hadi sasa Man City ipo kileleni mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 84 huku Man United ikiwa nafasi ya pili na pointi 68 na endapo Man City ikishinda itafikisha pointi 87 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

 

Man City na Man United zimecheza mechi 31 hadi sasa na zimebakisha mechi saba lakini baada ya mechi ya leo, zote zitabakisha mechi sita na kama Man City ikishinda itafikisha pointi 87, Man United itabaki na pointi 68 na ikishinda mechi zitakazobaki itafikisha pointi 86 tu.

Guardiola akizungumzia mchezo huo alisema; “Tutapambana nyumbani tushinde na kutwaa ubingwa mbele ya wapinzani wetu, najua ni mechi ngumu kwani wapinzani wetu tunawaheshimu wao ni timu bora. “Wikiendi iliyopita tulicheza mechi, baada ya siku tatu tukacheza na Liverpool mechi ya Ligi ya Mabingwa na sasa tunacheza na Man United baada ya siku tatu, halafu tunacheza tena na Liverpool. “Ratiba yetu ni ngumu lakini tutapambana, hivyo ni tofauti na wenzetu ambao wamejiandaa kwa siku saba kuelekea mchezo huu.” Kwa upande wake, Mourinho alisema: “Mechi ya watani? Halafu iweje? Sifikirii sana kuhusu mechi hii.

“Man City siyo muhimu kwangu. “Kitu muhimu kwangu ni kubaki katika nafasi ya pili hadi mwisho wa ligi na tunakidhi kuwa katika nafasi hiyo msimu huu kwani tupo hapo kwa muda mrefu. “Hatutafurahi endapo Man City watatangaza ubingwa mbele yetu, tutapambana na wenzetu hii ndiyo raha ya soka.”

 

Man City inacheza na Man United ikiwa imetoka kufungwa mabao 3-0 na Liverpool katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano wiki hii.

Comments are closed.