The House of Favourite Newspapers

Hadithi: Insane (Mwendawazimu -2)

Ilipoishia sehemu ya 1

Kila mtu alibaki akimwangalia, alimuonea huruma kwani kwa jinsi alivyokuwa akilia, alionekana kuwa mtu mwenye maumivu makali moyoni mwake. Alikaa hapo kwenye benchi kwa saa nne ndipo madaktari wakamtoa mumewe katika chumba kile na kumpeleka katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa ajili ya mapumziko.

“Mungu! Naomba umpiganie mume wangu! Naomba umpe uzima, najua madaktari wanahangaika kwa ajili yake. Wao si chochote kile, wewe ndiye daktari wa mwisho mwenye nguvu ya kumponya mume wangu! Naomba ufanye muujiza, naomba umuinue tena kitandani pale alipolala,” alisema mwanamke huyo huku machozi yakiendelea kutiririka mashavuni mwake.

Kila alichokiomba, aliomba akiwa na maumivu makali mno moyoni mwake.

****

 

Waandishi wa habari wakakusanyika katika hospitali hiyo, walitaka kufahamu kile kilichokuwa kimetokea. Taarifa kwamba bilionea Edson alipata ajali akiwa na muigizaji Stela ilisambaa kwa kasi sana kiasi kwamba hata wale waliokuwa vijijini nao wakajua kile kilichokuwa kimetokea.

Hakukuwa na daktari aliyependa waandishi hao wawepo ndani ya hospitali hiyo lakini lilikuwa jambo gumu kuwafukuza kwani walitaka kupata habari juu ya kila kitu kilichotokea lakini kubwa zaidi lilikuwa ni kutaka kujua kama bilionea huyo alikuwa hai au alifariki katika ajali hiyo.

Walimfuata mke wake, Rachel na kuanza kumuuliza juu ya kilichokuwa kikiendelea. Mwanamke huyo hakuzungumza kitu chochote kile, aliuinamisha uso wake na kuendelea kulia. Muda huo alihitaji nguvu za Mungu kuupoza moyo wake kwani ulichanganyikiwa na mbaya zaidi alikuwa na maumivu makali.

Aliuzuia moyo wake kumchukia Stela, alijua kwamba alimchukulia mumewe lakini hilo hakutaka kuliweka moyoni kwani alikumbuka vizuri maneno yaliyoandikwa kwenye Biblia kwamba alitakiwa kusamehe saba mara sabini.

“Mungu nipe nguvu, siwezi, chuki inaninyemelea, nashindwa kujua nini cha kufanya,” alisema Rachel huku akichukua kitambaa chake cha jasho na kuyafuta machozi yake.

Madaktari walikuwa bize, hawakutaka kutoka ndani ya chumba kile, watu walioletwa walikuwa kwenye hali mbaya sana, wakati mwingine walihisi kwamba tayari walikwishafariki kwani tangu wapoteze fahamu kwenye ajali ile, hawakuwa wamerudiwa na fahamu kabisa.

Mashine za oksijeni zilikuwa puani mwao, madaktari hao walikuwa wakijitahidi kuyaokoa maisha yao kwa kuamini kwamba kama wasingefanya jitihada zote kuyaokoa maisha yao basi wangeweza kufa kitandani walipokuwa wamelala.

“Hali inaendeleaje?” aliuliza Dk. Kimario.

“Mapigo ya moyo yapo chini sana, ila tumewawekea Propafenone IV kwa ajili ya kuyarudisha mapigo yake ya moyo katika hali ya kawaida,” alijibu nesi Maria.

“Safi sana. Kama hiyo dripu itakwisha, chomekeni nyingine mbili, zote ziwe na Propafenone IV. Mmenielewa?”

“Ndiyo mkuu!”

Hawakutaka kutulia, uhai wa watu hao ulikuwa kitu cha muhimu kwa kipindi hicho, walifuata maelekezo ya daktari na hata dripu zile zilipokwisha, wakaweka nyingine na kuendelea kuwasikilizia.

Baada ya saa mbili, mapigo yao ya moyo yakaanza kurudi katika hali ya kawaida. Kwa Edson, kidogo hali yake ilikuwa ikiridhisha lakini kwa msichana Stela, mambo yalikuwa mabaya zaidi kwani kadiri muda ulivyozidi kuongezeka ndivyo hali yake kitandani pale ilivyoonekana kuzorota.

“Huyu msichana hali yake ni mbaya sana, cha msingi ni kumuomba Mungu,” alisema Dk. Kimario.

“Atakufa?”

“Bado sijajua. Nimejaribu kukiangalia kichwa chake, kina majeraha sana cha msingi tumuombe Mungu tu,” alisema daktari huyo.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa, msichana Stela alikuwa kwenye hali mbaya, kitandani pale alipokuwa alionekana kama mfu, kichwani aliwekewa bandeji kubwa ambazo kadiri dakika zilivyokuwa zikienda mbele ndivyo zilivyojaa damu kutokana na kichwa chake kupata majeraha makubwa.

Madaktari hawakukata tamaa, bado walijitahidi kumhudumia msichanahuyo lakini juhudi zao ziligonga mwamba kwani siku tatu tangu afikishwe hospitalini hapo, Stela akafariki kitandani hapo.

“Amekwishafariki…tusingeweza kumuokoa,” alisema Dk. Kimario huku uso wake ukiwa kwenye majonzi mazito kana kwamba alifiwa yeye.

Hiyo ilikuwa taarifa kubwa iliyomtingisha kila mtu aliyekuwa akifuatilia filamu za Bongo Muvi. Stela alifahamika, alikuwa staa mkubwa nchi Tanzania, tena aliyependwa kila kona na ndiyo maana kifo chake kiliwashtua watu wote waliosikia taarifa hiyo.
Watu wakaanza kujazana nyumbani kwao Magomeni Mapipa, wengi hawakuamini kama kweli msichana huyo alifariki dunia kwani tayari alikwishaipigia promo filamu yake mpya ya Penzi Penzini na ilitarajiwa kutoka siku chache mbeleni.

“Hivi kweli Stela amekufa?” aliuliza msichana mmoja huku akionekana kutokuamini.

“Ndiyo! Yaani siamini kabisa..kweli Stela amekufa…” alisema msichana mwingine.

Taarifa iliendelea kusambaa zaidi, hospitalini, watu wakajazana, wengi wao hawakuwa wakiamini kile kilichokuwa kimesambaa sana katika mitandao hivyo walitaka kushuhudia wenyewe au kusikia chochote kile kutoka wa daktari wa hospitali hiyo.

Kwa kuwa Dk. Kimario hakuwa msemaji, akamuachia msemaji wa hospitali hiyo ambaye alithibitisha kwa waandishi wa habari na watu wengine kwamba kweli msichana huyo alikuwa amefariki dunia.

“Na vipi kuhusu bilionea Edson?” aliuliza mwandishi mmoja.

“Bado tunaendelea kumuhudumia,” alijibu daktari.

“Atapona?”
“Wote tunaamini hilo, ila maombi yenu ni muhimu zaidi,” alijibu daktari huyo na kuingia ndani.

Matibabu yaliendelea, hali ya Edson haikutengemaa pale kitandani, bado alionekana kuwa na tatizo kubwa katika mifupa yake hivyo mwisho wa siku madaktari wakakubaliana kwamba ni lazima mwanaume huyo asafirishwe na kupelekwa nchini India kwa matibabu zaidi.

Hicho ndicho kilichofanyika, siku mbili mbele, yeye, mkewe na madaktari wawili walikuwa njiani kuelekea katika Hospitali ya Ganga nchini India. Ndani ya ndege Rachel alikuwa na mawazo tele, hakuamini kilichokuwa kikiendelea kwamba mumewe alilala kitandani huku akiwa kimya, hakutingisha kiungo chochote kile mwilini mwake.

Moyo wake uliuma, muda mwingi alikuwa akimuomba Mungu amponye mumewe kwani hakuwa na tegemeo jingine, bila Mungu, aliona kila kitu kuwa kigumu mbele yake.

Baada ya saa kumi na tano, ndege ikafika nchini India ambapo moja kwa moja Edson akashushwa na kisha kupandishwa kwenye machela iliyosukumwa mpaka katika garoi la wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Ganga na safari ya kuelekea huko kuanza.

“Mungu! Naomba umponye mume wangu! Naomba usimpe adhabu hii kubwa, Mungu! Hata kama hutosikia maombi yake, naomba usikie maombi yangu Mungu,” alisema Rachel huku gari likiendelea na safari kama kawaida.

Mara baada ya kufika hospitali, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuchukua ripoti kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuanza kuipitia, walitaka kuangalia tatizo lililokuwa nini mpaka mtu huyo kuuwa hivyo.

Jopo la madaktari watano likakusanyika katika chumba kimoja cha mkutano na kisha kuanza kuiptia ripoti hiyo ambapo wakagundua kwamba mara baada ya kupata ajali, mifupa yake mikubwa ya miguu na mikono ilivunjika lakini mbali na hiyo, pia mshipa wake mkubwa wa urethra ulikuwa umeharibiwa vibaya.

“Mshipa wake wa urethra umeharibika vibaya,” alisema Dk. Mantesh.

“Unasemaje?”
“Ndivyo ripoti inavyosema! Hii hapa.”

Akawagawia wenzake ripoti ile na kuanza kuiangalia. Kila mmoja akashtuka, ilikuwa vigumu sana kumpata mtu ambaye aliharibiwa vibaya na mshipa huo ambao ndiyo uliokuwa ukimfanya kiungo cha mwanaume kufanya kazi inapotakiwa pindi anapokutana na mwanamke.

Suala la mshipa huo kuharibiwa vibaya ilionyesha kwamba kiungo chake kisingeweza kufanya kazi tena, mbali na hiyo, pia hata wakati wa kukojoa, katika siku za kwanza atakuwa akipata maumivu makali mpaka pale ambapo mshipa huo ungerekeshwa sehemu ambazo zilikuwa na tatizo, ila la kiungo kutokufanya kazi lingeendelea katika maisha yake yote.

Hawakutaka kumficha mkewe, walichokifanya ni kumuita na kumwambia ukweli kile kilichokuwa kimetokea. Rachel hakuamini, alibaki akilia kwa maumivu makali moyoni mwake, hakuamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wa yeye kufanya mapenzi na mumewe, alilia kama mtoto mdogo.

“Pole sana…” alisema daktari huku akimbembeleza.

“Sina mtoto daktari…sina mtoto..” alisema Rachel huku akilia. Dk. Mantesh akamkumbatia na kuanza kumfariji.

Hilo ndilo lililotokea, Rachel hakuwa na jinsi, alitakiwa kukubaliana na matokea kwamba mumewe asingeweza kushiriki naye mapenzi kitandani kutokana na ajali iliyomtokea.

Moyo wake ulimuuma mno, muda mwingi alionekana kuwa na mawazo, hakuamini kama Mungu aliruhusu yeye kupitia katika maisha aliyotakiwa kupitia kipindi hicho. Hakuacha kuomba, hospitalini hapo, kila alipokuwa kwenye benchi, alimuomba Mungu kwa kuamini kwamba kupitia Yeye, hakukuwa na kitu ambacho kingeshindikana.

“Mungu! Najua unajua ni jaribu kubwa kiasi gani napitia. Sijui nifanye nini, ila naomba unipe nguvu ya kusonga mbele,” alisema Rachel huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.

Serikali Yaingilia Kati Suala la Parking

 

Comments are closed.