The House of Favourite Newspapers

Hadithi: Insane (Mwendawazimu -4)

Ilipoishia Sehemu ya 3

“Ni lazima nizae na Miriam, haiwezekani hata kidogo nimuache,” alisema Boniface huku akionekana kumaanisha. Hakutaka kutoa macho yake kwa msichana huyo. Kila alipomwangalia, ndivyo alivyompenda zaidi.

SONGA NAYO…………..

Rachel hakuwa na furaha, moyo wake ulikosa amani, kila alipoyakumbuka maneno ya daktari kwamba mumewe asingekuwa na uwezo wa kufanya mapenzi moyo wake ulimuuma mno.

Kila wakati alionekana kuwa na majonzi, wakati mwingine alikuwa akikaa peke yake na kutulia tu kwenye benchi huku akiyafikiria maneno hayo ambayo yaliingia mpaka moyoni mwake, ndani kabisa na kumganda.

Hakukuwa na kitu alichokuwa akikitamani kipindi hicho kama mtoto. Alikuwa radhi kukosa kila kitu katika maisha yake lakini si mtoto. Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kufanikisha hilo, kama ingewezekana, basi kipindi hicho angelala na mwanaume kisha kupewa mimba na pindi mumewe atakapopona amwambie kwamba kabla ya kupata ajali, mimba ilikuwa imeingia.

Hilo lilimuingia kichwani mwake na lilimsumbua mno lakini hakuwa na jinsi, hakutaka kufanya mchezo huo mchafu kwani bado alikuwa na penzi la dhati kwa mume wake huyo.

Siku zikaendelea kukatika huku madaktari wakifanya kazi yao kwa nguvu kubwa. Baada ya miezi miwili ya matibabu makubwa hospitalini hapo ndipo Edson akarudiwa na fahamu.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuangalia kila upande katika chumba alichokuwepo. Alikumbuka kwamba mara ya mwisho alikuwa ndani ya gari lake akiwa na mchepuko wake, Stela, walikuwa wakibadilishana mate, na baada ya hapo hakujua ni kitu gani kilichotokea.

Mara baada ya nesi kumuona Edson akiwa amefumbua macho, harakaharaka akatoka ndani ya chumba hicho na kwenda katika ofisi ya daktari na kumuita. Huo ulikuwa muujiza mkubwa kwani kwa kipindi kirefu mwanaume huyo alikuwa hapo hospitalini akiteseka.

“Hatimaye umerudiwa na fahamu,” alisema Dk. Mantesh huku akimwangalia Edson.

“Dokta! Nipo wapi?”
“Upo India.”
“Imekuwaje tena? Nakumbuka mara ya mwisho nilikuwa ndani ya gari. Imekuwaje?” aliuliza Edson huku akimshangaa Dk. Mantesh.

Daktari huyo akamtaka apumzike kwanza kwani kama kujua kilichokuwa kimetokea, angekifahamu lakini si kwa muda huo. Akamuwekea dripu nyingine na kisha kutoka ndani ya chumba hicho.

Kwa sababu ilikuwa usiku na Rachel alikuwa hotelini, akachukua simu yake na kumpigia mwanamke huyo na kumpa taarifa njema, harakaharaka Rachel akarudi hospitalini hapo.

“Nataka nimuone mume wangu!” alisema Rachel mara baada ya kufika hospitalini hapo.

“Nifuate!”
Wakaondoka mpaka katika chumba kile. Kitendo cha kumuona mumewe kitandani, kumbukumbu za maneno ya daktari kwamba mwanaume huyo hakuwa na uwezo wa kufanya mapenzi na mwanamke zikaanza kurudi kichwani mwake. Hapohapo machozi yakaanza kumtoka. Akasimama, akabaki akimwangalia mume wake.

“Mke wangu! Nini kimetokea?” aliuliza Edson, kiukweli hakukumbuka kitu gani kilitokea mara baada ya kuwa na msichana Stela kwenye gari.

“Ulipata ajali!”
“Ajali! Ilikuwaje?”

Hapo ndipo Rachel akaanza kusimulia kila kitu kilichotokea. Moyo wa Edson ulihuzunika mno, aliyakumbuka maneno ya mkewe kila siku alipokuwa akizungumza naye kuhusu msichana huyo na kumwambia kwamba hakuwa akitembea naye bali zilikuwa mbinu za magazeti kutaka kumchafua.

Hakukuwa na siri tena, kila kitu kilijulikana, mkewe alijua kila kitu kilichotokea hali iliyompa wakati mgumu mno moyoni mwake. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kumuomba msamaha mke wake.

“Naomba unisamehe mke wangu!” alisema Edson huku akimwangalia mkewe usoni.

“Usijali mume wangu! Nimekusamehe hata kabla hujaniomba msamaha,” alisema Rachel pasipo kumwambia mumewe kwamba huyo Stela alikuwa amefariki dunia. Kama yeye alikuwa hivyo, vipi kuhusu Stela? Alitamani kuuliza lakini akaona bora kunyamaza kwa kuona kwamba angemuumiza mke wake.

Comments are closed.