The House of Favourite Newspapers

Hadithi ya Eric Shigongo: Dimbwi la Damu-07

“Shabir hebu  mwache   mimi nitaongea naye!” Alisema Leah  alipomwangalia Victoria na kushikwa na huruma ! Aligundua kitu  walichokuwa wakikifanya yeye na mume wake hakikuwa sahihi  ukizingatia  wema  ambao   wazazi wa Victoria walimfanyia yeye.

“Jamani msiniache nitaishije mimi?”

Leah alimnyanyua Victoria kutoka chini alipokuwa amekaa    akamsimamisha wima na kumshika mkono kisha kuanza kutembea nae kuelekea nje ya nyumba ambako wote walikaa chini kwenye msingi wa nyumba!

“Victoria!”

‘Naam dada!”

“Si Mungu ni mmoja au? Na ni nini kitatufikisha mbinguni je madhehebu yetu au matendo yetu?”

“Matendo yetu dada!”

“Unafikiri Uislamu au Ukristo wetu ndio utatufikisha mbinguni?”

“Hapana dada!”

“Sasa kuna ubaya gani wewe ukiingia katika Uislamu  na ukaendelea kumwabudu Mungu  wako na matendo yako yakaendelea kuwa mema mbele za Mungu?”

Victoria aliinamisha kichwa chake kwa kama dakika kama tano hivi akiwaza bila kumjibu Leah kitu chochote! Kwa harakaharaka kichwani mwake alizichambua dini  moja baada ya nyingine na kuona zote zilimwambudu Mungu! Aligundua mtu anaweza kuwa Mkristo lakini  bado akawa na dhambi nyingi na  kuishia  jehanamu na mtu mwingine anaweza kuwa Mwislam lakini akawa na matendo yasiyofaa akaenda jehanamu vilevile! Kwake tofauti ya madhehebu au dini ilionekana  kukosa maana!

“Cha muhimu ni matendo yangu, dhehebu  langu halitanifikisha mbinguni! Dada nimekubali kubadili dini tena  kwa hiari yangu kwani Mungu ni mmoja!”

Leah alimkumbatia Victoria na baadaye wote walisimama wima na kuanza kutembea kurudi tena ndani ambako walimkuta Shabir amekaa kitini akiwasubiri, Leah alimpa taarifa hizo mumewe  nae hakuamini alichokisikia alinyanyuka na kumbusu Victoria usoni.

“Victoria umekubali sababu ya kukulazimisha au?”

“Hapana shemeji maneno aliyonieleza dada kule nje yamenifanya nigundue hakuna tofauti yoyote, sote tunamwabudu Mungu   mmoja na yatakayotufikisha  mbinguni ni matendo yetu wala si madhehebu!”

Mzee Shabir alishangazwa sana na maneno ya Victoria aligundua  kumbe haikuwepo  sababu ya kutumia nguvu   kumghasi alimshukuru  mkewe kwa diplomasia aliyoitumia.

Siku tatu baadaye taratibu za dini ya Kiislam zilifanyika  Victoria akawa amebadilisha dini na jina lake tangu siku hiyo likawa Fatma! Hali ilibadilika sana ndani  ya nyumba yao hapakuwa tena na chuki  kila mtu alionekana kuwa na furaha.

Siku kumi na sita  baadaye mipango ya safari ilikuwa imekamilika  ingawa ilifanyika kwa siri kubwa   mzee Shabir hakutaka   watu wafahamu  alikuwa akiihama  Tanzania  sababu kubwa ya kufanya jambo hilo ilikuwa ni kukimbia na pesa nyingi alizokuwa akidaiwa kama kodi.

“Nitafikiria  kitu cha kufanya ili kuudanganya ulimwengu kuwa tumekufa!” Alimwambia mkewe wakiwa wamelala na siku mbili baadaye alikuwa na mpango kamili kichwani mwake.

“Nitatega shoti hapa ndani siku ya kuondoka ambayo itasababisha moto utakaoichoma na kuiteketeza kabisa nyumba yetu kila mtu ataamini sote tumeteketea ndani ya moto! Sitaki kutafutwa sababu nitatoroka na pesa za serikali!” Aliendelea kusema mzee Shabir na wote   walikubaliana  juu ya jambo hilo bila Victoria kufahamu!

****************

Ulikuwa ni  usiku wa manane gari lilikuwa  nje ya nyumba yao  likiwa limejazwa mafuta  tayari kwa safari, Vicky alivalishwa  nguo nzuri na safi  na hata Man`0jit mtoto wao naye alipendeza.

Ilikuwa ni safari ya kuiacha Tanzania nchi aliyozaliwa na kwenda ugenini ambako Victoria hakumfahamu mtu yeyote, woga ulimwingia moyoni lakini hakuwa na chaguo jingine zaidi ya kukubali kusafiri!  Kila kitu alichokuwa nacho alikuwa anakiacha, mdoli aliyenunuliwa na mama yake akiwa mdogo  na kumtunza mpaka wakati huo alikuwa anamwacha pia.

Alikuwa tayari kuacha vitu vyote lakini si kipande cha noti alichoachiwa na kaka yake Nicholaus, hicho alikuwa nacho mkononi! Aliamini ndio kitu pekee kilichomkumbusha juu ya pacha wake kwake kilikuwa ni   sawa na Nicholaus mwenyewe.

Leah akiwa amembeba Manjit  alimshika mkono Victoria na kumuongoza hadi  nje ya nyumba ambako  walipanda ndani ya gari, walimwacha Mzee Shabir  ndani ya nyumba akikamilisha kazi yake maalum na dakika kama kumi hivi baadaye alitoka na kuungana nao  ndani ya gari.

“Tayari!” Alimwambia mke wake aliyekuwa amembeba Manjit mkononi  aliyekuwa akilia sababu ya baridi kali iliyokuwepo mjini Arusha siku hiyo.

“Kwa hiyo?”Leah aliuliza.

“Itawaka baada ya saa nzima hivi!” Alijibu kwa sauti ya chini chini mzee Shabir na kuanza kuliondoa gari lake kwa kasi.

Alichofahamu Victoria ni kuwa kutoka Tanzania kwenda Canada ilikuwa ni lazima kutumia usafiri wa ndege lakini alishangaa   kuona wanaondoka kwa gari, alitamani  kuuliza lakini moyo wake ulisita na kuamua kuvuta subira.

Safari ilikuwa ndefu na gari lilikimbia kwa kasi, kulipokucha   walikuwa  jijini Nairobi ambako mzee Shabir alishughulikia mipango ya usafiri na kuikamilisha. Walikuwa na uhakika hakuna mtu aliyefahamu  walikuwa nchini Kenya kwa wakati huo, waliamini    watu wote mjini Arusha walijua Shabir na familia yake waliteketea kwa moto.

“Au inawezekana moto  haukuwaka?”

“Kwani hukutega vizuri shoti?”

“Niliitega vizuri sana na kama haitawaka basi nina uhakika  watanitafuta na nitarudishwa tena Tanzania kushtakiwa kwa kukwepa kodi!”

“Siyo rahisi!”  Alisema Leah huku akimpigapiga mzee Shabir begani.

Walifanya maongezi yao  taratibu wakihakikisha   Victoria hasikii kitu lakini muda mfupi baadaye Leah alionyesha mshtuko alipotupa macho kwenye luninga iliyokuwepo ndani ya hoteli waliyokuwa wakila chakula  kabla ya kwenda uwanja wa ndege.

“Baba Manjit hebu ona kule kwenye luninga, ona! Ona! Ona!” Alizidi kumpigapiga mumewe begani ili aangalie.

Shabir alipogeuka kuangalia alikuta ni taarifa ya habari ya shirika la CNN! Nyumba ilikuwa ikiteketea kwa moto, kwa hakika ilikuwa nyumba yao! Watu wengi walionekana wamekusanyika kushangaa tukio hilo, magari ya zimamoto yalikuwa yakiendelea kuuzima moto huo  kwa bidii.

Leah na mumewe walikaa kimya wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa na mtangazaji wa televisheni aliyekuwa akiwasiliana na makao makuu kutoka  eneo hilo la tukio.

“Inaaminika watu wanne wamefia ndani ya moto huu! Mwanaume mmoja na mkewe pamoja na watoto wao wawili!”

“Hakuna njia yoyote ya kuwaokoa?”

“Inavyoonekana hakuna!”

“Chanzo cha moto ni nini?”

“Hakijajulikana bado ingawa kuna habari kuwa chanzo ni shoti ya umeme!”

Aliposikia maneno hayo mzee Shabir aliruka juu na kushangilia kwa furaha  kwani mpango wake wa kudanganya ulikuwa umefanikiwa! Watu wote ndani ya hoteli hiyo walishangazwa na kitendo cha kushangilia ajali, hawakuelewa nini ilikuwa sababu ya mzee Shabir kufanya hivyo.

Muda mfupi baadaye waliondoka kwenda uwanja wa ndege ambako walipanda ndege kwenda zao Ottawa!

“Hawatakuja kufahamu siri hii, nipongeze basi mke wangu!”

“Hongera sana darling!”

“Hivi wewe una kitu ulichosahau Tanzania?”

“Hata kimoja, sina baba wala mama, nini cha kufuata tena  bongo!” Alisema Leah,  sababu alikuwa yatima aliamini asingerudi tena Tanzania.

**************

Nicholaus, Tehran:

Uwanja wa ndege wa Al- Akiri ulijaa mamia ya wakazi wa jiji la Tehran, haukuwa mkusanyiko wa kawaida bali watu wote walikuwa pale kushuhudia kifo cha muuza madawa ya kulevya, biashara iliyochukiwa na karibu kila mtu nchini humo.

Watu walishangilia kifo cha binadamu mwenzao! Nicholaus alikuwa amefungwa kwenye mti mkubwa  macho yake yakiwa yamefunikwa kwa kitambaa cheusi!Alikuwa amekata tamaa kabisa ya maisha na mwili wake wote ulikuwa umekufa ganzi! Picha ya dada yake Victoria iliendelea kumwijia kichwani mara kwa mara.

Machozi yalizidi kumbubujika Nicholaus, alisikitika kufa ugenini na kumwacha dada yake aliyempenda Victoria! Alijilaumu  kwa kitendo chake cha kukubali kuongozana na wauza madawa ya kulevya!

“Sina hatia jamani! Sina hatia hata kidogo!” Aliendelea kulia Nicholaus wakati mkuu wa jeshi akihesabu maaskari walitegemea akifikisha tatu wafyatue bunduki zao na kummaliza Nicholaus aliyekuwa amefunika macho yake  akisubiri kifo.

Ghafla kabla mkuu wa jeshi hajafikisha tatu katika kuhesabu tatu!  Ardhi ilianza kupasuka, kutikisika na kudidimia! Maghorofa marefu yalianza kuanguka lilikuwa ni tetemeko la ardhi baya kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini Iran.

Watu walisahau kilichowapeleka uwanjani  na kuanza kukimbia huku na kule kuokoa maisha yao hata maaskari walizitupa bunduki zao na kuanza kukimbia mbio, hakuna aliyekumbuka kumuua Nicholaus tena. Alibaki peke yake akiwa amefungwa kwenye  mti

Nicholaus aligeuza kichwa chake na kuanza kukisugua kitambaa alichofunguwa nacho usoni kwenye mti ili aweze kuona  vizuri, ilikuwa kazi ngumu lakini alifanikiwa kukishusha hadi mashavuni na kuanza kuona mbele!

Hakuyaamini macho yake alipojikuta yu  peke yake eneo hilo!  Na alishuhudia maghorofa makubwa na marefu yakidondoka na kusambaa ardhini, watu wengi walirushwa na kutupwa mbali na  mawe makubwa yaliviringika hadi eneo alilokuwa amefungwa mengi yalitaka kumponda  na mengi yalipita pembeni! Hakuwa na uhakika wa kuokoka.

Pembeni yake kulikuwa na majengo marefu yaliyokuwa yakiyumba na kuashiria  yangeanguka wakati wowote na kumpondaponda kabisa Nicholaus! Kwa mara nyingine tena aliiona sura ya dada yake Victoria na kulia  kwa uchungu.

Aliendelea kujaribu kuzikata kamba zilizomfunga mikononi   mwake kwa meno lakini alishindwa  kwani zilikuwa  kamba nene na ngumu! Kwa mbali aliona kisu lakini alishindwa kukifuata sababu alikuwa amefungwa.

“Mungu wangu ninusuru mie mwanao, nilifanya makosa makubwa kumkimbia ndugu yangu Victoria! Najua baba Mungu unaniadhibu  kwa kosa hilo, napenda kusema nampenda Victoria hata wewe unajua! Nisingemwacha ila ni kwa sababu ya shida  nilizokuwa nazo  na kama nitakufa basi Mungu nisamehe makosa yangu!” Alisali Nicholaus na baadaye kuendeleza sala ya ‘baba yetu uliye mbinguni’

Alipofungua macho  yake kuangalia mbele baada ya sala hiyo, alishangaa kumwona msichana wa Kitanzania aliyekutana naye uwanja wa ndege  akija mbio kuelekea mahali alipokuwa, Nicholaus akajua alikuwa amempata Mwokozi wa maisha yake, aliamini Mungu amejibu maombi yake.

“Njoo unisaidie dada!”

“Nakuja usiwe na wasiwasi!” Alijibu msichana huyo huku akikimbia na alipomfikia alimfungua kamba  zote mikono na baadaye miguuni.

“Haiwezekani Mtanzania mwenzangu ufe  hapa peke yako ni heri nikuokoe kaka yangu! Nilikuwepo tangu  mwanzo lakini nilishindwa kukusaidia, tetemeko lilipoanza nilikimbia lakini mbele zaidi nikakukumbuka nikaamua kurudi kuja kukusaidia!” Alisema msichana huyo baada ya kumfungua Nicholaus kutoka mtini.

“Sijui nikushukuru vipi dada? Kwa kweli sijui jinsi ya kukushukuru ila Mungu atakulipa kwanza unaitwa nani”

“Ninaitwa Neema Lucas ila hayo yaache kwanza tutaongea baadaye cha muhimu tujiokoe  hebu nifuate!” Msichana huyo alisema huku akimvuta Nicholaus   na wakaanza kukimbia kwenda upande wa pili kulikokuwa na  maghorofa mafupi kidogo.

“Tukifika kwenye mnara wa Khomein tutakuwa tumeokoka!” Alisema msichana huyo.

Mnara wa Khomein ulikuwa ni  mnara wa kiongozi wa nchi hiyo, uliheshimiwa na kila mtu na ulijengwa katika eneo la wazi ambalo halikuwa na ghorofa hata moja, kila lilipotokea tetemeko nchini humo watu walikimbilia kwenye mnara huo! Ulikuwa umbali wa kama  mita mia tano kutoka maeneo hayo lakini kulionekana mbali kwa jinsi hali ilivyokuwa.

Walizidi kukimbia lakini ghafla kilitokea kitu ambacho hawakukitegemea! Ardhi mbele yao ilipasuka na ghorofa kubwa na refu lilikuwa likiporomoka juu yao, kila mtu alijua lingewaponda lakini kabla  halijatua chini, ardhi iliyopasuka iliwameza wakawa wameingia ndani ya shimo likawa sawa na kaburi! Ghorofa lilianguka juu yao, pande kubwa  kama jiwe la udongo lilitua juu yao lakini halikuwafikia baada ya kuzuiliwa na vipande vya ardhi. Walikaa humo kwa takribani masaa mawili bila kupata msaada wowote.

“Dada Neema samahani   kwa kukusababishia matatizo ninajua nia yako ilikuwa ni kuokoa maisha yangu lakini kwa bahati mbaya imeshindikana na sasa hata wewe maisha yako  yapo hatarini, thawabu yako utaikuta mbinguni!” Alisema Nicholaus huku akitokwa na machozi.

“Usijali Nicholaus yote ni mipango ya Mungu!”

“Heri ningebaki tu na Vicky wangu!” Aliwaza Nicholaus huku Neema akiwa amemkumbatia juu yake wote wawili walikuwa wakilia machozi.

“Dada wewe kwenu   ni mkoa gani nchini Tanzania?”

“Kagera kijiji cha Kanyigo!”

*************

Pande kubwa la udongo lililokuwa juu yao lilizidi kushuka kadri ardhi ilivyozidi kutingishwa na tetemeko hatimaye liliteremka kwa kasi na kumponda Neema kiuno, alijaribu kujinasua lakini alishindwa! Akaanza kulia kwa maumivu akimwomba Nicholaus amuokoe.

“Niokoe Nicholaus, nisaidie Nicholaus nakufa!”

NIcholaus alijaribu kuchimba kwa chini ili amtoe lakini pia ilishindikana,roho ilimuuma sana kushindwa kumsaidia mtu aliyejitoa ili kuokoa maisha yake. Machozi ya uchungu yalimtoka, kuumia kwa Neema ilikuwa ni sawa kuumia kwa Victoria dada yake.

Baadaye jiwe lilizidi kumgandamiza na hewa ilizidi kuwa nzito na hawakujua nini kingewaokoa kutoka katika mlango wa kaburi,   kitu walichokuwa na uhakika nacho kwa wakati huo ni  kifo  sababu ya kukosa hewa safi.

“Nicholaus nisaidie nakufa!” Neema alizidi kulia.

“Sawa nifanye kitu gani dada?”

“Nivute!”

Nicholaus alijaribu kumvuta kwa nguvu zake zote lakini pia haikuwezekana  Neema alizidi kulia hatimaye alinyamaza kimya kwa muda wa dakika kama kumi, aliporejea ni neno moja tu alilosema.

“Nisalimie Tanzania kama  ukiokolewa!” Alisema  Neema kisha akakaa kimya! Nicholaus alilia machozi ya uchungu na huruma!

********************

Ndege iliingia katika uwanja wa ndege wa  Ottawa masaa kumi na  mawili baadaye, kila mtu alikuwa amechoka vibaya mno na safari lakini  Victoria alichoka zaidi, pamoja na hali hiyo bado kipande cha noti alichoachiwa na kaka yake kilikuwa mkononi mwake! Mawazo yote yalikuwa kwa Nicholaus, alishindwa kuelewa yeye na kaka yake wangekuja kukutana vipi maishani mwao kwa umbali aliokuwa amekwenda! Lakini bado aliamini ipo siku wangeonana.

“Hapa ndio Ottawa, Canada! Tutaishi hapa maisha yetu yote!” Mzee Shabir alimwambia Leah baada ya kufika kwenye nyumba aliyonunua kwa pesa aliyopaa kwa ukwepaji wa kodi, alioufanya nchini Tanzania.

 

 Je, nini kitaendelea?
Endelea kufuatilia Jumatano hapahapa

 

Tu-Follow kwenye mitandao ya kijamii;

Facebook @Globalpublishers

Twitter @GlobalHabari

Instagram @GlobalPublishers

YouTube @GlobalTVTZ

Endelea kutembelea website ya Global Publishers kila siku, tutaendelea kukusogezea kila news inayotokea mahali popote duniani.

Comments are closed.