The House of Favourite Newspapers

Hadithi ya Shigongo: Dimbwi la Damu-12

Vumbi zito lilikuwa likitimka ilikuwa ni hali ya hatari, Nicholaus alijua kifo kimemfikia baada ya kukichenga kwa muda mrefu, lakini ghafla akili yake ilifanya kazi kama kompyuta akageuka kwa kasi ya umeme na kulala chali katikati ya reli, aliyashuhudia matairi ya treni yakipita kila upande wa mwili wake na treni likipita juu yake injini yake ikimuunguza vibaya mwilini mwake.

Yalikuwa ni maumivu makali sana yaliyompata, kwa sababu ya vumbi na joto la injini alifumba macho na muda mfupi baadae alipoteza fahamu na hakuelewa kilichoendelea.

Mbele kidogo treni lilisimama ghafla na abiria wote waliokuwemo ndani yake walishuka na kuanza kumwangalia mtu aliyemgonga, walirudi hadi nyuma wakiangalia chini ya reli hatimaye wakamkuta Nicholaus chini ya behewa moja akiwa ameungua vibaya.

Walimbeba na kumpeleka hadi mbele kwenye behewa la tajiri Mohamed akiwa hajitambui, Mohamed alimuonea huruma sana na alishindwa kuelewa ni kwa nini kijana mdogo   kama yeye alikuwa  katika pori lenye wanyama wakali kiasi kile.

Alijaribu kumwita ili kujua kama alikuwa hai lakini Nicholaus hakuitika sehemu kubwa ya mbele ya mwili wake ilikuwa imeungua vibaya mno hiyo ikiwa ni pamoja na uso.

“Mwambieni dereva aiondoe treni haraka tujaribu kuokoa maisha ya huyu kijana kwani tumebakiza kilometa ngapi kuingia Baghdad?”

“Mia mbili na hamsini”

“Haya tuondokeni na mwiteni daktari aanze kumshughulikia!” aliamuru tajiri Mohamed na baadae treni ilianza kuondoka kwa kasi kuliko mwanzo lengo likiwa ni kumuwahisha Nicholaus mjini Baghdad ambako angepatiwa matibabu, tajiri Mohamed alishangaa ni kwanini moyo wake uliingiwa  huruma kubwa kiasi hicho juu ya Nicholaus, alitaka kufanya chochote kilichowezekana ili kuokoa maisha yake.

Waliingia Baghdad dakika arobaini na tano baadae na kilichofanyika ni kumkimbiza haraka iwezekanavyo kwenda hospitali ya jamii ya Kiislam iliyoitwa Al-Quaba, ilikuwa ni hospitali maarufu sana katika mji wa Baghdad ndio iliyotumika kuwatibu majeruhi wa vita vya Ghuba wakati Marekani ilipoishambulia Iraq.

“Amepatwa na nini huyu?”

“Ajali ya treni!”

“Ajali ya treni?”

“Mbona yuko hivi?”

“Ulitegemea aweje binti?” Mzee Mohamed aliuliza.

“Tumezoea kuwaona majeruhi wa ajali za treni wakiwa nyang’anyang’a!”

“Ilikuwa bahati kabla hatujamgonga alilala kifudifudi katikati ya reli hivyo treni likapita juu yake!”

“Sasa kwanini ameungua kiasi hiki?”

“Nafikiri joto la injini lililomuunguza lakini treni haikumgonga!”

“Kuna watu wengine pia walioumia?”

“Majeraha madogo madogo tu hawa wametibiana wenyewe tatizo ni huyu mtoto naomba mumsaidie na kama kuna uwezekano atibiwe katika daraja la kwanza mimi nitalipa!” alisema mzee Mohamed akionyesha huzuni kubwa.

“Anaitwa nani?”

“Anaitwa Abdallah Hussein!” Mzee Mohamed alilazimika kudanganya jina la mgonjwa ili kuepusha hali ya kutonekana hakuwa na uhusiano wowote na Nicholaus.

Kauli hiyo mzee Mohamed iliongeza kasi ya matibabu, haikuchukua hata sekunde tano daktari akawa ameshafika na kumuandikia Nicholaus dripu za maji ili kuyarudisha maji yaliyopotea kutokana na moto pia alimuandikia dawa za maumivu ili kumpunguzia mateso.

Mgongo na makalio yote ya Nicholaus yalikuwa yameungua vibaya kiasi cha kushindwa kuelewa ni kwa namna gani dawa ingeweza kuwekwa katika vidonda vyake, alichofanya daktari ni kuagiza Nicholaus alazwe kifudifudi na dawa imwagwe moja kwa moja kwenye vidonda.

“Put a bed cradle to prevent body and sheets contact!” (Wekeni kifaa cha kuzuia mwili na mashuka yasinatane!)

Hivyo ndivyo wauguzi walivyofanya, matibabu yalikuwa ya hali ya juu! Kilifanyika kila kitu kuhakikisha Nicholaus anapona tena kwa gharama ya mzee Mohamed mwenyewe, alihamishwa katika wodi ya kawaida na kupelekwa katika wodi ya daraja la kwanza ambako matibabu yaliendelea.

*****************

Nicholaus alizinduka baada ya siku mbili na kujikuta yu katika maumivu makali kupita kiasi,kwanza alifikiri yuko  Tanzania  lakini alipoangaza macho yake huku na kule chumbani alishangazwa na watu aliowaona, badala ya kuona watu weusi aliona Waarabu wakikizunguka kitanda chake.

Alishtuka sana na kushindwa kuelewa ni wapi alikokuwa! Lakini ghafla kumbukumbu zilimjia kichwani mwake na kuliona treni likija kumgonga. Aliruka kitandani na kusimama wima, dripu zote zilichomoka na hata bendeji zilidondoka! Chuma kilichokuwa juu yake kuzuia mashuka yasigusane na mwili wake kiliruka na kuanguka pembeni.

Manesi walikimbia haraka kuelekea kitandani kwakena kumshika, walimrudisha kitandani haraka na kumuomba atulie lakini hakufanya hivyo, aliendelea kupiga kelele akiomba msaada!  Daktari alipoitwa alielewa kilichotokea na kuamua kumpa Nicholaus dawa ya usingizi ili apumzike.

“Ni kumbukumbu ndizo zimemsumbua hakuna kitu kingine!”

“Kweli daktari?”

“Ndiyo! Hii hutokea mara nyingi sana hasa kwa watu waliopatwa na ajali”

Alipozinduka baadae Nicholaus alikuwa ametulia kabisa na alielewa kila kitu kilichotokea, pia kumbukumbu za Tehran zilimiminika kichwani mwake, alikumbuka alipofungwa kamba na kusubiri kupigwa risasi sababu ya kuingiza madawa ya kulevya nchini humo, lakini akaokolewa na tetemeko la ardhi!

Alimkumbuka pia Neema, msichana aliyejitolea kumuokoa lakini wote wawili wakagandamizwa na udongo, Neema akafa lakini Nicholaus akaokoka.

Mwisho kabisa alipomkumbuka dada yake Victoria roho ilimuuma zaidi na kujikuta akilia machozi yaliyomtonesha vidonda vyake! Alishindwa kuelewa kama mpaka wakati huo alikuwa bado yuko hai  ingawa ndani ya nafsi yake alilazimika kuamini hivyo.

Kumbukumbu ya kipande cha noti walichogawana na dada yake ilipomwijia alijikuta akipiga kelele tena na kuomba apewe suruali yake, mwanzoni alipoongea kiswahili manesi hawakumuelewa akaamua kubadilisha lugha na kuongea Kiingereza, hapo ndipo wote walimuewa na kumsogezea suruali yake karibu ingawa hakuelewa aliihitaji ya kazi gani.

Alinyoosha mkono wake wa kuume na kuudumbukiza ndani ya mfuko wa kulia wa suruali yake akijaribu kukitafuta kipande cha noti alichokiweka! Furaha aliyoipata ilikuwa ya ajabu pale  mkono wake ulipokigusa kipande hicho ndani, hakutaka kukitoa nje bali aliikunja suruali yake na kuiweka chini ya godoro la kitanda chake.

Ghafla mlango ulifunguliwa akaingia mzee wa kiarabu mfupi na mwenye ndevu nyingi, alifanana kabisa na watu wa Iran wenye majina ya Khomein! Alikuwa na kilemba kichwani, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Nicholaus kumuona mzee huyo!  Alishindwa kuelewa ni nani lakini alionekana mwenye furaha nyingi na alikumbatiana na wauguzi na madaktari waliokuwepo chumbani.

Nicholaus alishindwa kuelewa ni kwanini na baada ya salamu na madaktari mzee huyo alimsogelea Nicholaus kitandani na kumshika kichwani.

“How are you my son?” (Vipi hali yako mwanangu?)

“ I thank God am a little  bit fine now!” (Namshukuru Mungu hali yangu ni nzuri kidogo)

“Do you know me?” (Unanitambua mimi?)

“No, thank you” (Hapana)

“I’m Mohamed Mashreef” (Ninaitwa Mohamed Mashreef)

“ Nice to meet you but what is your concern in me?” (Ninafurahi kukutana na wewe lakini nini haja yako kwangu?)

Mzee Mohamed alimueleza Nicholaus kila kitu kilichotokea na ni kwanini aliamua kumsaidia, haikuwa rahisi kwa Nicholaus kuamini kulikuwa na binadamu mwenye roho nzuri kama mzee huyo, alimpa shukrani zisizo na idadi na alimuomba  aendelee kumpa msaada.

Habari za kunusurika kifo kwa Nicholaus katika ajali mbaya ya treni ziliandikwa na kutangazwa na vyombo mbalimbali vya habari katika nchi za Ghuba, ni gazeti la Baghdad Times lililoingia nchini Iran na kusomwa na viongozi wa kikosi cha kudhibiti madawa ya kulevya nchini humo. Wengi walimfananisha kijana aliyepata ajali hiyo na Nicholaus lakini kwa alivyoungua usoni na jina lake kuwa tofauti walishindwa kuwa na uhakika ikabidi maaskari  watano watumwe kwenda nchini humo kufanya uchunguzi.

*********************

Fahamu zilimreja baada kama ya dakika kumi na tano na kukuta Maji na damu nyingi yakiendelea  kumtoka ukeni, alikuwa katika maumivu makali mno lakini hakuwa na la kufanya kwa sababu alishaamua kumuua mtoto wake ili kujiepusha na ugomvi kati yake na mlezi wake Leah kwani maisha bila yeye  yasingekuwa maisha tena!

Hasira aliyokuwa nayo juu ya Shabir ilimfanya anyanyuke na kuutoa mrija uliokuwa ndani yake, alitaka kuuingiza tena lakini alishindwa sababu ya maumivu! Kwa shida kubwa alinyanyuka na kuanza kujikongoja kuelekea chumbani ambako alijifunika na blanketi lake kuanzia kichwani hadi miguuni! Aliendelea kulia chini ya blanketi hilo na hakunyanyuka tena mpaka saa tatu usiku alipozinduliwa na Shabir.

“Victoria! Nini kimetokea humu ndani mbona zulia limechafuliwa na damu?” Aliuliza Shabir lakini Victoria hakujibu kitu ikabidi aulize tena mara ya pili.

“Nilikuwa nakunywa juisi ya Zabibu bahati mbaya ikamwagika, nisamehe baba!”

“Nilishakuambia usiniite baba bali kila siku niite Darling wewe hivi sasa ni mama wa mtoto wangu au siyo?”

“Hapana, hiyo haiwezekani!”

“Utafanyaje sasa wakati tayari mimba unayo? Na siku nikisikia umeitoa nitakuua!”

“Siwezi kuitoa ila namuogopa sana Leah!”

“Kwani atafanya nini? Kama hataki si arudi Tanzania?” Alisema Shabir kwa dharau wala hakuelewa kilichotokea.

******************

Kwa siku tatu mfululizo Victoria aliishi bila maumivu yoyote zaidi ya maumivu aliyoyapata wakati wa kujitoboa mfuko kwa mrija wa kunywea soda na hakuna kitu  kilichotoka zaidi ya maji yaliyomwagika! Kwa kutokuelewa kwake aliamini maji yaliyotoka ndiyo iliyokuwa mimba iliyokuwa ndani ya mfuko wake lakini siku ya nne  asubuhi Shabir akiwa kazini Victoria alipatwa na maumivu makali ya ajabu ya tumbo.

Tumbo lilimnyonga kupita kiasi na aligalagala kitandani kwa maumivu, hayakuwa maumivu ya kawaida! Yalinyonga tumbo la chini mpaka kiuno chake, alipapasa kabatini na kutoa vidonge viwili vya maginiziamu akatafuna lakini bado havikumsaidia, aliendelea kuteseka namna hiyo mpaka saa nane za mchana alipojisikia kwenda kujisaidia haja kubwa.

Hakujua kama maumivu yaliyokuwa yakimsumbua ni uchungu, alipapasa ukuta hadi kwenda mpaka chooni ambako alichuchumaa kwa lengo la kujisaidia, badala ya kutoka kinyesi alishtukia kitu kikidondoka  kutoka  ukeni!  Baada ya kitu hicho kutoka maumivu yalitulia ghafla.

Alirudi chumbani ambako aliendelea kulala, aliamini mimba yake sasa ilikuwa imetoka!  Hakunyanyuka kitandani wala kula chochote mpaka  alipousikia mlango wa chumba ukifunguliwa, alikuwa ni Shabir na badala ya kwenda kitandani Victoria alisikia hatua zake akikimbia kuelekea chooni, ilionyesha alikuwa amebanwa sana na haja ndogo.

Dakika kama moja baadae alishtukia akinyanyuliwa kitandani na kuanza kupigwa kwa ngumi na mateke hadi akatupwa chini! Victori alilia kwa uchungu akiuliza ni kwanini alikuwa akipigwa.

“Yaani weee kenge umemuua mtoto wangu na wewe ni lazima ufe!”

 

 Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano hapahapa

Comments are closed.