The House of Favourite Newspapers

Hadithi ya Shigongo: Dimbwi la Damu-16

Ghafla tajiri Abdulwakil 
alirejea na fahamu zake 
tofauti na walivyofikiri madaktari,  baada ya kufungua macho yake aliangaza  huku na huku chumbani, mwanzoni hakuelewa mahali alikokuwa lakini alipoziona chupa za maji zikining’inia juu ya kitanda chake  alijua  mahali  alipokuwa ni hospitali.

Alimwangalia Patrick chumbani hapo lakini  hakumwona badala yake alimwona mkewe  akiwa amesimama pembeni  mwa kitanda chake uso wake ukiwa umejaa mshangao mkubwa!

“Ma…ma!”Abdulwakil alimwita.

“Pole sana mume wangu!”

“Ahsante!”

“Kilitokea nini?”

“Nili…mwo….na da…da ya…ngu!”

“Dada yako?”

“Nd…i….ooo!”

“Nani?”

“Vict….,hicho ndicho kilinishtua!”

“Unamuongelea Victoria yule pacha wako! Ambaye umekuwa ukinieleza habari zake?”

“Ndiyo!”

“Yuko wapi?”

“Alikuja nyumbani!”

“Unamaanisha ndiye  alikuja na yule kijana unayemdai?”

“ Haswa! Yuko wapi?” Tajiri Abdulwakil aliuliza.

Kwa bahati nzuri mama yake Manjit aliyasikia maongezi ya wafanyakazi pamoja  na Patrick kabla hawajaondoka hospitali kwenda nyumbani, waliondoka eneo hilo na kwenda kumuua  Victoria ambaye kila mtu kati yao aliamini  alihusika na matatizo yaliyompata tajiri yao! 

Wasiwasi  mwingi ulimwingia moyoni mwake akijua ni lazima wakati huo  Victoria alikuwa marehemu kama wafanyakazi walifanikiwa kumpata, ilikuwa ni lazima afanye kila alichoweza kuzuia tukio hilo kutokea! Alijua wazi mume wake asingefurahi kusikia Victoria kauawa, kwa jinsi Abdulwakil alivyomuongelea dada yake karibu kila siku  alielewa ni kiasi gani  alimpenda.

Bila hata kupoteza muda  alifungua mkoba wake na kutoa simu yake ya mkononi, akatoka nayo hadi nje ambako  alibonyeza namba fulani fulani na  kumpigia Patrick, lengo lake likiwa ni kumzuia asifanye kitu chochote kibaya kumdhuru  Victoria.

           **************

Jiwe la kwanza lililorushwa na mmoja wa  wafanyakazi lilitua moja kwa moja  kichwani kwa Victoria  likampasua na kumtoa damu nyingi! Ni wakati huo huo simu ya Patrick ilianza kuita!  Kwanza alitaka kuidharau lakini alipousikiza vizuri   mlio wa simu aligundua ulikuwa ni mlio wa  mama yake! Kwani  aliseti milio tofauti ya simu  za wazazi wake na watu mbalimbali maarufu.

“Patrick! Patrick! Patrick!” Alisikia sauti  ya mama yake ikimwita.

“Ndio mama!”

“Uko wapi?”

“Tulikuwa tunamtafuta huyu mchawi porini, tumempata na hivi sasa ninavyoongea na wewe vijana wanamshughulikia kisawasawa, muda si mrefu atakuwa amekufa hawezi kumpiga baba yangu na jini halafu yeye akabaki hai!”

“Mama yangu! Usifanye hivyo Patrick!”

“Kwanini mama?”

“Unamuua shangazi yako Victoria!”

“Shangazi yangu Victoria???” Aliuliza Patrick kwa mshangao mkubwa.

“Tafahdali  usimuue! Baba yako amerejewa na fahamu zake na kusema kilichomshtua ni furaha aliyoipata baada ya kumwona dada yake waliyepotezana naye miaka mingi!”

Patrick hakusema kitu tena maneno ya  mama yake yalimwingia moyoni, palepale alikata simu na kuanza kukimbia haraka kuelekea mahali alipolala Victoria akipigwa na wafanyakazi wake.

“Jamani msiniue!” Alilia Victoria lakini hakuna mtu aliyejali

“STOOOOOP!”  Patrick alipiga kelele  alipowafikia  wafanyakazi wake , Victoria alilala chini akilia machozi na kuomba asiendelee kupigwa, damu nyingi zilikuwa zikitoka.

“Vipi bosi!” Mmoja wa wafanyakazi alimuuliza Patrick.

“Mbebeni! Mbebeni!”

“Tumpeleke wapi?”

“Hospitali haraka”

Wafanyakazi wote walishangazwa na kauli hiyo lakini kwa sababu alisema  bosi wao, hakuna mtu aliyepinga maneno yake, Victoria akanyanyuliwa chini na kuanza kukimbizwa hadi nyumbani ambako alipakiwa ndani ya gari na kwa haraka alikimbizwa hadi hospitali! Madaktari walipomuona katika hali hiyo walikataa kumpokea wakihitaji karatasi ya polisi, lakini baada ya Patrick kuongea nao vizuri na kumpa kitu kidogo daktari wa zamu pesa kidogo, Victoria alipokelewa akiwa katika maumivu makali na kupelekwa  chumba cha upasuaji na kushonwa sehemu zote zilizochanika, alipotolewa chumba cha upasuaji  alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi  ambako alilazwa hali yake ilikuwa mbaya mno! Hakuna  mtu aliyekuwa na uhakika kuwa  Victoria angepona.

******************

“Baba! Nisamehe baba! Sikujua kama ni shangazi!” Patrick aliongea akiwa amepiga magoti  pembeni mwa kitanda cha baba yake ilikuwa siku tatu tu tangu Victoria ashambuliwe kwa mawe kufuatia amri aliyoitoa kwa wafanyakazi..

“Kwanini ulichukua uamuzi wa kuua?”

“Baba ni kwa sababu ninakupenda na sikuwa tayari kuona mtu amekufanyia kitu kibaya wakati mimi nipo!”

“Ndio uue?  Sasa akifa je?”

“Mungu atamsaidia baba, nisamehe kwa kitendo nilichokifanya!”

“Nimekusamehe Patrick lakini hakikisha shangazi yako anapata matibabu ya uhakika ili apone, sipo tayari kumpoteza Victoria ni pacha wangu  na ninampenda sana,  siamini hata kidogo kuwa nimekutana  naye tena baada ya miaka mingi! Lolote lifanyike  na kwa gharama zozote lakini Victoria apone”

“Sawa baba nitafanya kama unavyoagiza!”

“Na si yeye tu pia hakikisha   kijana aliyeko mahabusu anatolewa  inawezekana ni mtoto wa dada yangu!”

“Nani Manjit?”

“Ndiyo!”

“Leo hii hii atatoka baba!”

Siku hiyo haikuwezekana kumtoa Manjit mahabusu lakini siku  iliyofuata  alitolewa  na kukaribishwa nyumbani kwa tajiri Abdul Wakil,  Patrick  alionekana kuwa  rafiki  zaidi kuliko siku nyingine zote, kitu cha kwanza alichofanya baada ya kutoka mahabusu ni kuuliza  mahali Victoria alikokuwa!

“Victoria anaumwa sana!” Patrick alimjibu.

“Anaumwa nini?”

Patrick alikaa kimya  kwani hakuwa na jibu la kumpa Manjit kuhusiana na  swali lake, alionyesha masikitiko makubwa sana usoni, hali hiyo ilimtia wasiwasi  Manjit, hisia zake zikamfanya aanze kufikiria labda Victoria hakuwa hai.

“Umesema anaumwa kitu gani?”

“Alipatwa na ajali!”

“Ajali?”

“Ndiyo!”

“Ajali ya nini?”

“Aligongwa na gari!” Patrick alidanganya

“Kwa hiyo yupo wapi?”

“Hospitali!”

“Nipeleke!”

“Pumzika kwanza!”

“Haiwezekani nipeleke hospitali kwanza!”

Patrick alipoiangalia saa yake ya mkononi  ilikuwa saa saba na nusu mchana, aligeuza gari na kuondoka kwa haraka  kuelekea hospitalini, ambako yeye na Manjit walikwenda moja kwa moja hadi chumba cha  wagonjwa mahututi alikolazwa Victoria, waliruhusiwa na muuguzi na  kuingia hadi chumbani kwa mgonjwa, Manjit alilia machozi alipomwona Victoria kitandani, uso wake ulikuwa umevimba kupita kiasi na kichwa kizima kilifunikwa na bandeji.

“Anti Vicky! Anti Vicky! Anti Vicky!” Alianza kumwita akimtingisha lakini Victoria hakuzinduka, muuguzi aliyekuwa karibu alikuja na kumshika Manjit mkono akimzuia kumtingisha.

“Jamani mlimfanya nini mama yangu mdogo?” Aliuliza Manjit huku akilia machozi na  Patrick alimshika mkono na kuanza kumtembeza hadi nje ambako alikaa kitini na kuendelea kulia, Patrick alimwekea mkono begani na kuanza kumbembeleza.

“Nisamehe sana!” Patrick alisema.

“Kwa kosa gani?”

“Siwezi kukueleza hivi sasa, ila wewe ni ndugu yangu!”

“ Ndiyo binadamu wote ni ndugu lakini nahitaji kufahamu nini mlimfanyia mama yangu mdogo  sababu ya kunidai ndio  mkaamua kumuua? Sawa tu!”

“Hapana siyo hivyo! Hebu kwanza twende huku!” Patrick alisema akimsaidia Manjit kunyanyuka kitini na  kumwongoza hadi katika chumba alicholazwa tajiri Abdulwakili, wote wawili waliingia, hali ya Abdulwakili tayari ilikuwa nzuri alikuwa ameketi kitandani akinyweshwa uji na mke wake, walipoingia  mama yake Patrick alishtuka hasa alipomwona Manjit akilia.

“Vipi tena?”

“…nimemleta huyu kijana nimtambulishe kwenu!”

Manjit aliwasabahi wote huku machozi yakiendelea kumtoka! Alionyesha wazi kulikuwa na jambo lililomtatiza, hali hiyo ilishtua wazazi wote wa Patrick.

“Vipi mbona  mwenzako analia?”

“Huyu ndiye Manjit!”

“Manjiti???? Ndiye huyu????” Abdul Wakili aliuliza kwa mshangao”

“Usilie mwanangu, madeni yako yote nimeyafuta!” Abdul Wakil alisema  akiamini kilichomliza Manjit ni wasiwasi wa kulipa! Alinyanyuka kitandani na kwenda  moja kwa moja hadi  kwenye kiti alichokalia Manjit na kukaa naye.

“Nashukuru sana  kwa kunifuatia deni lakini bado nataka kujua ni  nini  mmemfanyia mama yangu mdogo wakati alikuwa mzima?”

“Hilo nitakueleza baadae lakini napenda kuongea  maneno machache na wewe kwanza!”

“Maneno gani?”

“Ulishawahi kumsikia mtu aliyeitwa Nicholaus?”

“Ndiyo mama mdogo alimtaja mara kwa mara!”

“Basi ni mimi!”

“Ni wewe? Wewe si ni Abdulwakil?”

Tajiri Abdulwakil alianza kumsalimia Manjit historia nzima ya maisha yake, kuanzia Arusha mpaka Baghdad!  Alipomweleza kuwa yeye na Victoria walikuwa mapacha Manjit alishangaa  sana, alimweleza wazi kuwa miaka yote alikuwa akimtafuta  dada yake na alimshukuru sana Manjit kwa kumleta hadi kwake!

“Umefanya jambo kubwa mno na sijui jinsi ya kukushukuru!”

“Kwa hiyo wewe ndiyo Nicholaus?”

“Ndiyo, wewe ulizaliwa wapi Tanzania au Canada?”

“Nilizaliwa Tanzania lakini  baadaye tukahamia Canada!”

“Baba yako ndiye Shabir siyo?”

“Ndiyo!”

“Na mama yako ni Leah!”

“Ndiyo!”

“Leah alikuwa yaya katika nyumba yetu  mimi na Victoria tukiwa watoto wadogo, wazazi wetu walimchukua akiwa yatima na kuishi nae, hivi sasa wako wapi?”

“Wote ni marehemu! Baba alifariki miaka mingi iliyopita na mama amefariki wiki iliyopita!”

“Masikini waliugua nini?”

“Baba alijinyonga na nilipotoka tu huku kukopa mafuta nilikuta  mama yangu akiteketea katika moto! Nyumba yetu iliungua”

“Kweli?”

“Ndiyo!”

“Pole sana mwanangu, tangu sasa niite mjomba si Abdulwakil tena!”

“Sawa lakini ilikuwaje ukabadili  jina?”

Swali hilo lilimfanya Abdulwakil asimulie kila kitu kilichotokea maishani mwake ikiwa ni pamoja na namna alivyoupata utajiri wote aliokuwa nao katika biashara ya mafuta, muda wote   akisimulia Manjit alibaki mdomo wazi,  hakuamini  binadamu anaweza kuteseka kiasi hicho kabla ya kufikia mafanikio yake. Baadae wote walinyanyuka na kukumbatiana hapakuwa na uadui tena, kulichokuwa mbele yao kilikuwa ni kuhakikisha Victoria anapona na maisha yanaanza upya.

“Nitafanya sherehe kubwa sana dada yangu akipona, nafikiri  nchi ya Iraq hawajawahi kuona sherehe kubwa kama hiyo tangu  iwepo juu ya nchi!” Alisema tajiri Abdulwakil huku akitabasamu, kila siku alikwenda wodini kwa Victoria kumwangalia, hali ilimsikitisha sana lakini bado alimwombea dada yake kwa Mungu ili apone na wafurahie tena maisha pamoja baada ya mateso ya muda mrefu! Wiki moja baadae Abdulwakil aliruhusiwa kutoka wodini na kurejea nyumbani ambako aliendelea kupona taratibu, lakini hali ya Victoria bado iliendelea kuwa mbaya.

         ******************

“Patrick!”

“Naam daktari!”

“Kwa kweli tumejitahidi sana kumsaidia shangazi yako bila mafanikio na sasa  tunaelekea   kukata tamaa  ingawa  bado tunayo matumaini kuwa  akifikishwa nchini Marekani katika hospitali ya Boston  Medical Institute anaweza kupona  kwa sababu huko kuna mabingwa  wa kufanya operesheni za ubongo  kuliko sisi hapa Baghdad, mimi nilisoma katika hospitali hiyo nina imani  na madaktari wa hospitali hiyo.

“Kwa hiyo unashauri tumpeleke huko?”

“Kuna njia mbili  za kufanya, ya kwanza ni kusafiri hadi huko lakini ya pili ni kuwaleta wataalam hapa kwa gharama zako mwenyewe!”

“Ni hayo tu?”

“Ndiyo!”

“Hakuna shida anachotaka baba ni shangazi kupona  hata kama ni kwa gharama  gani! Nafikiri hakuna haja ya kusafiri waagize hao madaktari waje wafanyie hapa hapa mimi nitaongea na baba!”

“Basi subiri kwanza!” Daktari alisema na kunyanyua simu, alipiga moja kwa moja hadi hospitali ya Boston  Insitute na kuongea na Dr. William Knight,  mkuu wa kitengo kilichoitwa NeuroSurgery Department kilichojishughulisha na operesheni za ubongo na mishipa ya fahamu! Na madaktari  wawili walikubali kuondoka Marekani kwenda Baghdad kumshughulikia Victoria..

 ****

Furaha ya tajiri Nicholaus 
ama Abdulwakil kama 
alivyojulikana na wengi katika nchi za Kiarabu kukutana na dada yake Victoria waliyepotezana miaka mingi wakiwa watoto wadogo iliingia dosari baada ya hali ya Victoria kuwa mbaya kufuatia kipigo alichopigwa na wafanyakazi wa kwenye visima vyake vya mafuta kwa amri ya mtoto wake Patrick, wakimhusisha Victoria na uchawi, kuwa alihusika na kuugua ghafla kwa Abdulwakil baada ya kukutana naye.

Abdulwakil hakuwa tayari hata kidogo kuona Victoria anakufa mbele ya macho yake  kwani kwa  siku nyingi mno alikuwa amemtafuta  Victoria bila mafanikio, halikuwa jambo rahisi kwake kukubali mara moja dada yake afe bila juhudi zozote kufanyika!Alikuwa tayari kutumia chochote alichokuwa nacho kuokoa maisha  ya Victoria!

“Atapona kweli?”

“Atapona tu wale madaktari ni mabingwa!”

“Kwani tatizo lake kwenye ubongo ni nini hasa?”

“Nafikiri alipigwa na kitu kizito kichwani, fuvu likapasuka kwa ndani na damu ikavuja na sasa damu  hiyo inaugandamiza ubongo kwa ndani!”

“Kwa hiyo madaktari hao watafanya nini ili kuokoa maisha yake?”

“Watafanya upasuaji wa kichwa kisha watatoa bonge la damu lililoganda ndani, ni operesheni ngumu kidogo kufanyika lakini kwa madaktari wanaokuja nina hakika wataweza!”

Majira ya  saa tatu na nusu usiku wa siku hiyo  madaktari kutoka marekani waliwasili  katika jiji la Baghdad kwa ndege maalum ya kukodi, iliyokodiwa kwa gharama za Abdulwakil  na kwenda moja kwa moja hadi hospitali alikolazwa Victoria, walionana na madaktari na kufanya kikao cha karibu dakika arobaini na tano wakielezwa kuhusu hali halisi ya mgonjwa na kilichokuwa kikimsumbua.

“She was involved in a mob justice act, hit hard by angry civillians! They broke her skull and caused internal bleeding which resulted into a contussion!”(Alipigwa na wananchi wenye hasira wakavunja fuvu lake na kusababisha damu ivuje kwa ndani ambayo iliganda na  kuanza kuugandamiza ubongo!)

“Oh! My God  did you do a CT-Scan?”(Mungu wangu mlimpiga picha ya  CT-Scan kichwani?) Dk. Knight aliuliza, mmoja wa madaktari kutoka Marekani.

“Yes!” (Ndiyo!)

“Can I see it?”(Naweza nikaiona picha hiyo?)

“Ndiyo!” Aliitikia Dk. Khalfa,  bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo, madaktari wote walikuwa ofisini kwake wakifanya kikao chao, alinyanyuka na kufungua kabati iliyokuwa nyuma yake na kutoa bahasha kubwa, ndani yake akatoa karatasi nyeupe ndogondogo mbili na kumkabidhi Dk. Knight ambaye alizitupia macho na kuanza kuzikagua.

Madaktari wengine wote walikaa kimya wakisubiri majibu ya Dk. Knight baada ya kuzikagua picha hizo.

“Its gonna be a tough task!”(Itakuwa kazi ngumu!)

“Why?”(Kwanini?)

“The clot is so huge and about to compress the carotid artery! We have to do this operation right now if we’re serious about this patient’s life! Are you ready?”(Bonge la damu lililoganda ni kubwa mno na karibu linaungandamiza mshipa wa damu unaopeleka damu kwenye ubongo, hivyo kama tunataka kuokoa maisha ya huyo mgonjwa ni lazima tuifanye hii operesheni sasa hivi! Mpo tayari?)

“Ready we are!”(Tupo tayari!)

Maandalizi yalifanyika haraka iwezekanavyo, Victoria akakimbizwa chumba cha upasuaji ambako madaktari waliotoka Marekani kwa kushirikiana na madaktari  wawili  wenyeji walimfanyia Victoria operesheni ya kufanikiwa kulitoa bonge la damu lililoganda  chini ya fuvu lake na kuiziba mishipa  ya damu iliyopasuka  ili kuzuia damu kuendelea kuvuja zaidi.

Ilikuwa operesheni ngumu   walifanikiwa kuikamilisha baada ya  masaa sita! Kila mtu kati yao alikuwa amechoka lakini walifurahi kuona operesheni imefikia mwisho ingawa hakuna mtu kati yao aliyekuwa na uhakika kuwa Victoria angepona.

Manjit, Patrick, tajiri Abdulwakil na mkewe walikuwa nje ya chumba cha upasuaji wakisubiri operesheni ikamilike, muda wote huo wa masaa sita machozi yaliendelea kumtoka Manjit, hakuwa tayari Victoria afe, ni mtu pekee aliyekuwa amebakiza duniani! Hakuwa na  baba, mama, bibi wala shangazi!

Kumpoteza Victoria kungemaanisha yeye kubaki peke yake duniani kitu ambacho hakuwa tayari hata kidogo kupambana nacho, pamoja na wema wote aliofanyiwa na familia ya Abdulwakil, pia msamaha alioombwa bado hakuwa tayari kumsamehe Patrick kwa kitendo chake cha kuamrisha watu wampige kwa mawe Victoria, mara nyingi alimwangalia kwa jicho la chuki! Jambo hilo hata Patrick mwenyewe aliligundua.

Wote watatu walimzunguka Manjit wakijaribu kumbembeleza lakini haikutosha, Patrick aliendelea kulia! Lakini  maneno ya tajiri Abdulwakil kuwa maumivu aliyokuwa nayo moyoni mwake kwa matatizo yaliyompata dada yake mpendwa yalimtia nguvu kidogo ingawa bado  moyoni mwake alikuwa haamini kama kweli Abdulwakil ndiye Nicholaus aliyeongelewa na Victoria kila mara.

“Pole na kazi daktari!” Abdulwakil alimwambia Dk.Knight baada ya operesheni hiyo, aliongea katika lugha ya Kiingereza.

“Ahsante sana!”

“Kuna matumaini kidogo?”

“Mungu atasaidia ingawa operesheni ilikuwa ngumu!”

Maneno hayo ya daktari  hayakumpa Abdulwakil uhakika wa Victoria kupona lakini hakutaka kuonyesha wasiwasi zaidi,  aliyaacha mambo yote mikononi mwa Mungu! Baadaye waliiona machela ikipitishwa kutoka chumba cha upasuaji na kupelekwa moja kwa moja chumba cha wagonjwa mahututi ambako Victoria alilazwa, hawakuruhusiwa kumwona mpaka siku iliyofuata asubuhi walipoingia wodini na kukuta bado Victoria hajitambui.

Alibaki katika hali hiyo kwa karibu siku saba, kila siku alipewa madawa makali ya usingizi yaliyomfanya alale kwa masaa yote ishirini na nne, alikula chakula kwa kutumia mrija uliopitishwa puani na pia aliwekewa dripu la maji zilizokimbizana kuingia kwenye mishipa yake! Hali yake haikuwa ya kuleta matumaini kila mtu alikuwa amekata tamaa! Kwa tajiri Abdulwakil ilikuwa huzuni kubwa zaidi pengine kuzidi hata aliyokuwa nayo Manjit.

Abdulwakil alitaka Victoria apone ili wawe pamoja tena   naye afaidi maisha kama alivyokuwa akifaidi yeye, mara nyingi alimuuliza Mungu ni kwanini kama aliamua kumkutanisha na dada yake iwe hivyo akiwa katika hali mbaya? Kuna wakati alishindwa kuvumilia machozi yakamtoka.

************

Kwa siku ishirini na saba Victoria aliendelea kulala kitandani bila kujitambua, vipimo vyake vyote vilionyesha hali yake iliendelea vizuri, mapigo yake yalikuwa sawasawa! Hiyo ilimaanisha kilichokuwa kikiendelea ni kupona kwa ubongo wake kazi ambayo hufanyika taratibu sana, sehemu mbalimbali za mwisho wake zilianza kurejewa na fahamu zilizokuwa zimepotea.

Siku ya ishirini na nane alifumbua macho lakini hakuweza kuongea chochote na kwa sababu alikuwa kipofu hakuweza kumwona mtu yeyote chumbani.

Manjit, Abdulwakil  na ndugu wote waliokuwepo  wodini hawakuruhusiwa kumsemesha kitu chochote kwani kufanya hivyo kungeuingiza ubongo wake katika shughuli na kuufanya uchelewe kupona zaidi, walizuiliwa kumwona kila siku wakawa wanamwona siku mbili tu kwa wiki! Mwezi mmoja baadaye hali yake ilikuwa nzuri aliweza hata kuongea.

“Anti!” Manjit alimwita.

“Wewe nani?”

“Mimi Manjit!”

“Manjit mwanangu au?”

“Ndiyo Anti! Pole sana!”

“Ahsante mwanangu! Walinipiga mno tena bila kosa lolote, lakini hapa tuko wapi?”

“Baghdad!”

“Ahaa! Nimekumbuka tulikuja kwenye matatizo yako ya mafuta?”

“Ndiyo!”

“Si walikukamata? Sasa walikuachia lini na matatizo yamekwisha au la?”

“Yamekwisha!”

“Kwa hiyo tunarudi Canada?”

“Hatutarudi Canada tena!”

“Kwanini?” Aliuliza Victoria lakini badala ya Manjit kujibu swali hilo alikaa kimya na minong’ono ilisikika pembeni, alikuwa akiongea na Abdulwakil aliyekuwemo chumbani akisikiliza maongezi yao.

“Anti!”

“Naam!”

“Hebu ongea kwanza na Abdulwakil!”

“Abdulwakil? Ambaye  watu wake walinipiga?”

“Ndiyo lakini msikilize kwanza!”

Victoria alitii sauti ya Manjit na kukaa kimya.

“Kwini!”  Victotia alisikia sauti ya mtu akimwita kwa jina ambalo hakuna mtu mwingine yeyote angemwita! Lilikuwa jina ambalo mama yake alimwita alipokuwa mtoto sababu ya muonekano wa sura yake,  alishangaa kupita kiasi.

“Wewe ni nani unayeniita jina hilo?”

“Mimi?”

“Ndiyo!”

“Naitwa Nicholaus!”

“Nicholaus? Mbona nimeambiwa unaitwa Abdulwakil”

“Amini maneno yangu mimi ni pacha wako Nicholaus niliyekuacha miaka mingi nyumbani Tanzania!”

“Haiwezekani! Sogea nikupapase usoni, ingawa mimi ni kipofu lakini sura ya Nicholaus bado naikumbuka!”

Abdulwakil  hakubisha kitu, alichofanya ni kusogeza uso wake karibu na mahali alipolala Victoria, mkono wa Victoria ukaanza kupita usoni mwake taratibu ukimgusa kwa ulaini.

“Mh! Mbona sio wewe?”

“Ni mimi Nicholaus!”

“Mbona uso wako umejaa makovu kiasi hicho? Nicholaus hakuwa na sura ya aina hiyo”

“Nilipatwa na ajali mbaya sana wakati nakuja hapa kutoka  Iran, nimekuwa na shida nyingi katika maisha yangu mpaka kufikia hapa nilipo nitakueleza tukipata nafasi ila maisha yangu yalijaa mateso mengi, kila mara nilikulilia nilitaka sana kukutana na wewe lakini sikujua mahali ulikokuwa! Namshukuru Mungu  hatimaye amekuleta, nakupenda sana Victoria miaka yote nimekuwa nikitamani kukuona  hatimaye Mungu ametukutanisha! Hakuna deni atakalodaiwa Manjit ila tangu sasa wewe utaishi na mimi hapa Baghdad mpaka mwisho wa maisha yetu na Patrick na Manjit watafanya biashara pamoja sisi sote ni ndugu!” Alisema Abdulwakil na kumbusu Victoria usoni.

“Ilikuwaje ukaitwa Abdulwakil?”

“Maisha!”

“Maisha? Kivipi?”

Nicholaus alilazimika kuanza kueleza yote yaliyompata maishani tangu waachane na dada yake  nchini Tanzania,  kilichotokea mpaka akabadili dini na kilichotokea mpaka akatajirika kiasi hicho! Muda wote Victoria aliendelea kumsikiliza na Manjit pamoja na Patrick walikuwa kimya maneno yote yakiwaingia vizuri mioyoni mwao. Nicholaus aliongea maneno ambayo hata mke wake hakuwahi kuyafahamu, alilazimika kufanya hivyo  kumshawishi Victoria  kuamini kuwa  yeye ndiye alikuwa Nicholaus.

“Pamoja na maelezo yako yote bado siamini!”

“Kwanini?”

“Mtu yeyote anaweza kusema kama ulivyosema wewe!”

“Nifanye nini ili Victoria uamini!”

“Kuna kitu kimoja tu ambacho ukikifanya nitaamini!”

“Kitu gani?”

“Subiri!” Alisema Victoria kisha akaita kwa sauti ya juu ili muuguzi aliyekuwa ofisini aje, sauti yake ilifika hadi katika ofisi ya wauguzi na mara moja muuguzi mmoja alikwenda mbio hadi kitandani.

“Vipi Victoria?”

“Hakuna tatizo!”

“Nikusaidie nini?”

“Nafikiri nilipoletwa hapa nililetwa na nguo zangu!”

“Ndiyo!”

“Ziko wapi?”

“Ziko stoo!”

“Naomba basi uniletee gauni langu!”

“Sawa nakuja sasa hivi!”

Abdulwakil alishindwa kuelewa ni kitu gani alichotaka kufanya Victoria, ilibidi abaki kimya kusubiri! Hakumlaumu Victoria kwa jambo lolote kwani ilikuwa imepita miaka mingi sana bila kuonana na kwa sababu alikuwa kipofu hakuiona sura yake ili kukubali kuwa kweli yeye ndiye alikuwa Nicholaus ukizingatia alishabadilisha jina na alikuwa tajiri kupita kiasi kwa wakati huo. Dakika chache baadaye muuguzi alirejea akiwa na gauni lililojaa damu na kumkabidhi Victoria mkononi.

Victoria alianza kulipapasa gauni lake  katika mapindo  kama mtu aliyekuwa akisaka chawa! Ghafla alishtuka na kuacha zoezi hilo, akageuza kichwa chake kuelekea mahali sauti ya muuguzi ilikotokea.

“Sista naomba mkasi au wembe!”

“Wa nini?”

“Nataka unichanie hapa!”

“Unataka kuchana nguo?”

“Hapana kuna kitu nataka kukitoa!”

“Subiri nije basi!”

Muuguzi aliondoka aliporejea badala ya kuwa na mkasi alikuwa na wembe wa hospitali na kuanza kufumua sehemu aliyoelekezwa na Victoria,  tajiri Abdulwakil bado alikuwa amesimama eneo hilo akishangaa kitu ambacho Victoria alikuwa akifanya! Muuguzi naye alishangaa kukuta sehemu aliyokuwa akifumua kuna kipande cha noti.

“Mbona noti yenyewe kipande?”

“Acha tu mwanangu kazi yake mimi naifahamu!” Alisema Victoria kisha kugeuza kichwa chake kuelekeza mahali ilikotokea sauti ya Abdulwakil.

“Mimi na kaka yangu tuligawana kipande cha noti kama kumbukumbu wakati anaondoka tukiwa tumeahidiana kuviunganisha vipande vya noti tutakapokutana! Nimekitunza kipande hiki miaka mingi ili siku nikikutana na Nicholaus tuviunganishe! KAMA WEWE NI NICHOLAUS TOA KIPANDE CHAKO HUU NDIO UTAKUWA MWISHO WA UBISHI”

“Mh! Ninacho kweli?” Aliwaza Abdulwakil, mara ya mwisho kukiona kipande hicho ilikuwa ni miaka mitano kabla wakati akisoma kitabu cha historia ya Iraq nyumbani kwake, hakuwa na uhakika kama kitabu hicho bado kilikuwepo.

“Bila kipande hicho?”

“Haiwezekani!”

“Basi acha nikajaribu kukitafuta!” Akiwa amekata tamaa kabisa Abdulwakil aliendesha gari hadi nyumbani kwake, alifuatana na mkewe pamoja na Patrick wakimwacha Manjit na Victoria wodini, masaa mawili walipekuwa vitabu vyote vilivyokuwa ndani ya nyumba yao wakikitafuta kipande hicho bila mafanikio lakini dakika za mwisho kabisa Patrick alisikika akipiga kelele kutokea stoo, alikuwa amekiona kipande hicho cha noti na kutoka nacho mbio hadi sebuleni!

Abdulwakil aliruka  juu  na kushangilia na bila kuchelewa waliondoka hadi hospitali ambako waliwakuta Victoria na Manjit wakiwasubiri, Manjit hakuamini alipoona kipande cha noti nyekundu ya Tanzania kikitolewa na kukabidhiwa kwa Victoria, alikipapasa kipande cha Nicholaus na kupapasa kipande chake kwa taratibu akavinyoosha na kujaribu kuvikutanisha ncha zake, kweli vikashabihiana!

“Manjit hebu weka gundi hapa!”

“Sina gundi hapa anti!”

“Nesi tusaidie gundi!Au plasta kama unayo”

uuguzi bila kuchelewa alikimbia hadi ofisini na kuchukua plasta akaja  nayo na kuvigundisha vipande  viwili vya noti, vilikuwa vipande vichafu lakini vilipounganishwa vilifanana! Ilikuwa si rahisi kuamini vilikuwa vimeunganisha baada ya kutenganisha kwa miaka zaidi ya ishirini. Victoria alilia kwa furaha baada ya kukutana na kaka yake.

“Nicholaus!”

“Naam!”

“Nibusu usoni tafadhali siamini kama nimekutana na wewe!” Alisema Victoria huku akilia na Nicholaus alifanya hivyo bila kuchelewa.

Ilikuwa ni kama ndoto lakini  huo ndio ulikuwa ukweli, Victoria na Nicholaus mapacha waliotengana miaka mingi walikuwa wamekutana na kuunganisha vipande vyao vya noti walivyogawana  miaka mingi  wakati wa kutengana.

“Victoria!”

“Naam!”

“Mtu akiwa na kipande cha noti anaweza kununua kitu?”

“Hapana!”

“Basi nakupa kipande hiki cha noti  kitunze ili siku tukikutana   tuunganishe vipande vyetu na kununua kitu chochote!” Victoria aliyakumbuka maneno ya mwisho ya Nicholaus  wakati wakiagana miaka mingi mjini Arusha.

“Siamini!” Victoria alisema

“Hata mimi pia!”

Ilikuwa furaha kubwa isiyo na kifani mioyoni mwao hatimaye watu hao wawili kukutana, ulikuwa ni kama muujiza na ilikuwa si rahisi kuamini.

Wiki moja baadaye Victoria alitoka hospitali, sherehe kubwa kuliko zote zilizowahi kufanyika katika nchi ya Iraq ilifanywa watu wote mashuhuri nchini humo walialikwa,  Nicholaus alitembea akiwa amemshika mkono dada yake Victoria na kumtambulisha kwa karibu kila mtu aliyekuwepo ukumbini humo! Ilikuwa siku ya furaha kuliko zote zilizowahi kutokea katika maisha ya Nicholaus.

“Inaonekana huu ndiyo mwisho wa machozi yangu!” Victoria alisema akiwa amemkumbatia kaka yake.

“Lakini tumepita katika dimbwi la damu acha tupumzike!” Alimaliza Nicholaus na maisha tangu siku hiyo yalikuwa raha mstarehe!

 

 

MWISHO

Comments are closed.