The House of Favourite Newspapers

Hakielimu, Chuo Kikuu HAMK Kuimarisha Elimu ya Undi na Mafunzo Tanzania

0

Mkuu wa Uchumi na Utawala Umoja wa Ulaya, Karina Dzialowska (wa pili kushoto) pamoja na Afisa wa Umoja wa Ulaya nchni Tanzania, Agnes Hano (wa pili kulia) wakizindua rasmi Mradi wa Kuimarisha Ushirikiano na Uendelezaji wa Sekta ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Tanzania (TVET) unaofadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU). Kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, Dk. John Kalage akishuhudia.

HAKIELIMU kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha HAMK cha nchini Finland, Taasisi ya Mafunzo na Uendelezaji Tekinolojia ya 3DBear na SCV, Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Zanzibar; imezindua Mradi wa Kuimarisha Ushirikiano na Uendelezaji wa Sekta ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Tanzania (TVET) unaofadhiliwa na na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU).

Mkuu wa Mahusiano Ubalozi wa Finland, Juhana Lehtimem akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kuimarisha Ushirikiano na Uendelezaji wa Sekta ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Tanzania (TVET) unaofadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa  Ulaya (EU)

 

Mradi huo wa miaka mitatu (2024 – 26), una lengo la kutatua changamoto na ombwe lililopo kati ya mahitaji ya soko la ajira na wataalamu hitajika kwa kuwajengea uwezo walimu na wakufunzi wa vyuo vya Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA), katika kutumia teknolojia kufundisha na kusambaza maarifa ili kutoa wahitimu wanaoendana na mahitaji ya soko la ajira katika karne hii ya sayansi na teknolojia.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, Dk. John Kalage amesema mradi huo utajikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo (TVET) nchini pamoja na sekta binafsi; ili kujenga uhusiano wenye nguvu na wenye faida baina ya taasisi hizi, wajasiriamali na mahitaji ya soko la ajira.

Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, Dk. John Kalage akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kuimarisha Ushirikiano na Uendelezaji wa Sekta ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Tanzania (TVET) unaofadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa  Ulaya (EU).

Alisema lengo ni kuwawezesha walimu na taasisi za elimu ya ufundi kuboresha mafunzo wanayotoa ili kuwafanya vijana waweze kupata ajira kwa urahisi au kuanzisha biashara zao wenyewe.

“Mradi unalenga kukuza uwezo wa walimu ili waweze kusaidia wanafunzi wao kujiajiri; hii pia inalenga kuwapa walimu maarifa na ujuzi wa kuwasaidia wanafunzi wao wajue fursa za ujasiriamali na jinsi ya kuanzisha biashara zao wenyewe” alisema Dr. Kalage, ambaye ni Mkurugenzi HakiElimu.

Naye Meneja Mradi kutoka Chuo Kikuu cha HAMK Bi. Carita Cruz, aliongeza kuwa

mradi pia utawajengea uwezo walimu wa vyuo vya ufundi na mafunzo wa kutumia teknolojia ya kidijitali katika kufundisha ili kurahisisha uelewa wa wanafunzi na kuwafanya waweze kukabiliana na dunia ya ajira ya kisasa.

Wageni mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kuimarisha Ushirikiano na Uendelezaji wa Sekta ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Tanzania (TVET) unaofadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa  Ulaya (EU).

Alisema program hiyo itawapa fursa walimu na vyuo vinavyoshirikiana, kufanya ziara za mafunzo nchini Finland kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu. Hii itaruhusu Taasisi za VETA kuona jinsi nchi nyingine zinavyotekeleza dhana hii ya ushirikishaji walimu wa ufundi na mafunzo katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika ufundishaji.

Maofisa mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kuimarisha Ushirikiano na Uendelezaji wa Sekta ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Tanzania (TVET) unaofadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa  Ulaya (EU).

Mradi huo unatarajia kuwanufaisha zaidi ya walimu – wanafunzi 660 wanaodahiliwa katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC, ambao wataongeza idadi ya walimu wanaofundisha katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo vya Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi nchini na kunufaisha wanafunzi 66,459 wanaodahiliwa katika vyuo hivyo ambao watafundishwa na walimu hao waliojengewa uwezo.

Mradi huu pia utanufaisha wajasiriamali katika sekta binafsi ambao wamekuwa na hitaji la kupata wafanyakazi na wasimamizi wa shughuli zao wenye ujuzi na stadi zinazokidhi mahitaji ya soko ili kuzalisha faida zaidi.

Leave A Reply