The House of Favourite Newspapers

Hans Pluijm Amewakosea Nini Azam FC?

Kocha Hans van Der Pluijm.

HAKUNA kitu nakiheshimu duniani kama namba. Namba hazidanganyi kabisa, mchezo wa soka ni mchezo wa namba. Azam FC wana msimu wa 11 tangu wameanza kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara lakini wameshinda kikombe kimoja tu cha ligi! Hapa tatizo siyo Kocha Hans van Der Pluijm.

 

Hapa tatizo siyo kuwaondoa kina John Bocco, hapa tatizo siyo kuwaondoa kina Saad Kawemba wala Abdul Mohammed. Wiki iliyopita, Azam FC imemfukuza kocha wao mkuu, Hans van Der Pluijm na msaidizi wake, Juma Mwambusi.

Aliyekuwa kocha msaidizi wa Azam, Juma Mwambusi.

Unajiuliza, kosa la Pluijm ni lipi? Sipati jibu. Kwa mujibu wa mtandao wa soka Tanzania, Pluijm ameiongoza Azam FC kwenye jumla ya mechi 38, ameshinda 25, ametoka sare 10 na kupoteza 3 pekee. Kwa kocha ambaye yupo kazini kwenye msimu wake wa kwanza.

 

Kwa Kocha mwenye timu yake mpya, kwa kocha mwenye wachezaji wapya, bado kuna namna ambavyo wamiliki wa Azam FC walipaswa kulitazama vizuri jambo hili.

 

Baada ya kufungwa na Simba SC, kibarua cha kocha huyo kikaota mbawa! Kufungwa na Simba ni kosa? Jibu ni kwamba Simba ni timu iliyokamilika zaidi kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Simba kwa kipindi cha hivi karibuni, hakuna timu yoyote iliyofanikiwa kuwasumbua iwe ndani wala nje ya nchi. Wamempiga Al Ahly, wamempiga Yanga. Wamempiga African Lyon, wamempiga Lipuli. Hii timu haikamatiki kwa sasa.

 

Pluijm ni kocha aliyeipa mafanikio Azam FC. Ndiyo, kaipa mafanikio Azam wala hakuna ubishi. Katika kipindi chake cha nusu msimu, tayari amewapatia taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kwa jina la Kagame Cup.

 

Pluijm kawapatia pia taji la Mapinduzi, tena kwa kuwafunga mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC. Hans hakushindwa kabisa kuiongoza Azam FC! Bado Azam ipo kwenye mbio za ligi kuu na ina uwezo wa kutwaa.

 

Ni kweli Simba wako vizuri na wana mechi nyingi mkononi lakini bado kimahesabu Azam wanaweza kutwaa ubingwa. Ni kweli Yanga wako vizuri na ndiyo vinara kwenye ligi lakini bado Azam wanaweza kutwaa ubingwa.

 

Katika miaka mitatu ya hivi karibuni, Azam FC imekuwa na watendaji wakuu watatu, kimahesabu kila mwaka ni lazima wamfukuze mtendaji wao mkuu. Kwa miaka mitatu ya hivi karibuni, Azam FC imekuwa na makocha wakuu pia watatu, kimahesabu hakuna kocha aliyedumu na timu hata kwa misimu miwili! Timu ya soka haiendeshwi kwa aina hii ya maamuzi.

 

Azam FC watafukuza sana makocha, watafukuza sana wachezaji, watafukuza sana watendaji wao lakini bado wataendelea kusuasua tu.

 

Hakuna michuano yoyote ambayo Azam FC chini ya Pluijm wameshiriki na kukwama. Wamefaulu kote. Wako kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu, wako kwenye mbio za ubingwa wa Azam Sports Federation. Kosa la Hans van Der Pluijm ni lipi? Pengine hilo ni swali gumu, pengine majibu yake ndiyo magumu.

 

Azam FC hawajatolewa kwenye mashindano yoyote wakiwa chini yake. Kocha Hans alihitaji muda zaidi na kizuri zaidi bado ana kocha wake msaidizi, Juma Mwambusi ambaye anaufahamu sana mpira wa Tanzania.

Azam FC wanahitaji kuwa wavumilivu, timuatimua ya makocha haiwezi kuwapeleka kwenye ufalme wa soka la Tanzania. Bado kocha Pluijm alihitaji muda zaidi.

 

Kocha Pluijm ameanza kuisuka Azam kwa kusajili wachezaji wake ambao walihitaji pia muda kuweza kurejea kwenye ubora wao, mfano ni wachezaji Donald Ngoma na Obrey Chirwa. Hawa ni wachezaji wawili ambao alifanya nao kazi akiwa Yanga. Lazima wajifunze kuwapa muda waalimu wao.

 

Ni kweli makocha wote duniani hufukuzwa lakini kwa Pluijm wamemuonea bure. Kwa muda mfupi kawapa mataji mawili na bado timu yake ingeweza kimahesabu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na lile la Shirikisho.

 

Wamepita kina John Stewart Hall, Joseph Omog na wengine wengi sana. Hawa wote walikuwa miongoni mwa makocha bora sana, tatizo ni uongozi thabiti tu. Kuwatimua makocha na wachezaji bora kila mara ni kujirudisha nyuma wao wenyewe. Kucheza mechi 38 huku ukiwa umeshinda 25, sare 10 na kupoteza mara tatu tu, Hans alikuwa bado ni kocha sahihi Azam FC.

KIBANDA UNIZA NA OSCAR OSCAR

Comments are closed.