The House of Favourite Newspapers

Hans Poppe afunguka kuhusu mkataba wa Ajibu

Na Said Ally/CHAMPIONI/GPL
MWENYEKITI wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ameibuka na kuweka hadharani kwamba mkataba wa mshambuliaji wao Ibrahim Ajibu upo mikononi mwake na kilichobakia kwa sasa ni kwa mshambuliaji huyo kumwaga saini ambapo baadhi ya vipengele tayari washakubaliana.
Ajibu ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao na klabu hiyo inafika ukingoni mwishoni mwa msimu huu. Wengine ni Jonas Mkude pamoja na Abdi Banda.
Akizungumza na Championi Jumatano, Hans Poppe amesema kwamba kilichobakia kwa sasa ni kumpatia Ajibu kiasi ambacho anakihitaji kabla ya kusaini mkataba mpya baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano.
“Mkataba mpya wa Ajibu upo mikononi mwangu kwa sababu mimi ndiyo nashughulika na masuala ya mikataba ya wachezaji wote na sasa ambacho tunakisubiria ni yeye kuja kusaini mkataba huo mpya baada ya kumkabidhi kiasi cha fedha ambazo yeye amezitaka kwa ajili ya kusaini mkataba huo.
“Tayari kuna mazungumzo ya awali ambayo yamefanyika baina yetu kwa ajili ya yeye kuendelea kubakia nasi kwa msimu ujao na tunaamini hilo litafanikiwa kwa sababu hata yeye ameonyesha nia hiyo ya kubaki,” alisema Hans Poppe.

Comments are closed.