The House of Favourite Newspapers

Okwi Naikumbuka Sana Yanga

Na Said Ally/CHAMPIONI/GPL
MSHAMBULIAJI wa timu ya SC Villa ya Uganda, Emmanuel Okwi ambaye aliwahi kutamba na Simba ya hapa nchini, ametamka kuwa bado anaukumbuka upinzani ambao alikuwa anakutana nao alipokuwa Tanzania kutoka kwa timu mbalimbali ikiwemo Yanga wakati yeye akiichezea Simba.
Okwi kwa sasa anakipiga kwenye klabu hiyo ambayo inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uganda ikiwa na pointi 14, inadaiwa kwamba mkataba wake wa miezi sita ukimalizika anaweza kujiunga na timu nyingine ikiwemo Simba.
Mganda huyo aliyewahi pia kuitumikia Yanga, amesema ligi anayocheza kwa sasa ina upinzani wa hali ya juu, lakini hauwezi kuufikia ule uliopo Tanzania hali inayomfanya kuwa na hamu ya kurudi kucheza Bongo.
“Kokote pale kuna ushindani, huwezi kusema sehemu fulani hakuna ushindani, bali kuna tofauti ya huo ushindani.
“Kwa mfano ligi ya huku Uganda ni ngumu asikwambie mtu, mchezaji unatakiwa kupambana kisawasawa kuhakikisha unafanikiwa, lakini ugumu huu hauwezi kuufikia ule wa Tanzania.
“Tanzania kila timu ukikutana nayo unatakiwa kujipanga kisawasawa kitu ambacho kinanifanya niwe natamani nije kucheza huko japo mpaka sasa sijafanya mazungumzo na timu yoyote ile lakini nakumbuka upinzani mkubwa wa Yanga na Simba,” alisema Okwi ambaye mpaka sasa amefunga mabao matano katika ligi hiyo ya Uganda.

Comments are closed.