The House of Favourite Newspapers

Harmonize, Zungumza Na Fraga, Ngada Zitampoteza

Msanii  Harmonize.

 

YAWEZEKANA jina lake ni geni masikioni mwa wengi lakini tayari kazi alizozifanya ni kubwa na pengine ndiyo zinazompa jeuri ya kujiona tayari ameshakuwa supastaa.

 

Frank Mshumbushi au maarufu kwa jina la Fraga, pengine utajiuliza ni nani huyu? Unaujua wimbo wa Happy Birthday wa Harmonize? Basi huyu bwana mdogo ndiye aliyesuka biti mwanzo mwisho na kuufanya wimbo huo u-hit.

 

Ukiachilia mbali kazi hiyo, zipo kazi kibao za Wasafi, akiwemo hata Diamond Platnumz mwenyewe ambazo bado hazijatoka, zote zimepita kwenye mikono ya huyu bwana mdogo.

Lakini katika siku za hivi karibuni, zimeanza kuibuka taarifa zisizo za kufurahisha zinazomhusu kijana huyu ambaye kwangu mimi simuhesabii kwenye orodha ya watayarishaji muziki wenye majina makubwa Bongo, hata kama yeye ataendelea kutembea kifua mbele akiamini kwamba kila mtu anamjua.

 

Zipo taarifa kwamba Fraga ameanza kuandamana na watu wenye sifa mbaya kwenye jamii na kama wahenga walivyosema, ndege wa rangi moja huruka pamoja. Inadaiwa kwamba Fraga hakauki kwenye maskani za Kinondoni Manyanya na Magomeni Mapipa, wanakoshinda wale mapedeshee wanaosumbua kwenye klabu za usiku kwa kuwatuza wasanii ‘madolali’ kama hawana akili nzuri.

 

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba Fraga amekuwa kama mpambe wa vigogo hao ambao nyuma ya pazia tunaambiwa kwamba kazi yao ni kuwageuza wasanii hasa hawa wanaochipukia kuwa ‘punda’ wa kubeba madawa ya kulevya kupeleka Afrika Kusini na Brazil.

 

Namfahamu Fraga na mara ya mwisho nilipopata nafasi ya kubadilishana naye mawazo kwenye klabu moja iliyopo Mikocheni kulikokuwa na pati ya msanii mmoja maarufu wa Bongo Muvi, malalamiko yake yalikuwa ni kwamba kazi ya utayarishaji muziki Bongo hailipi.

 

Alisema wazi kwamba siku hizi maprodyuza wamejazana mpaka vichochoroni hivyo kazi hiyo haimlipi tena kwa hiyo na yeye anafikiria kuanza kuimba.

 

Siku chache baadaye, alisikika kwenye baadhi ya vyombo vya habari akitambulisha wimbo wake, ni hapo ndipo nikaamini maneno yake aliyoniambia kwamba ameamua kweli kuingia miguu miwili kwenye Bongo Fleva, kwamba badala ya kuendelea kuwasukia wenzake biti, ameamua kuimba mwenyewe.

Binafsi niliguswa na jitihada zake lakini kabla hata huo wimbo wake wenyewe aliouzindua haujaanza kuwa gumzo, tayari kashfa nyingine imeingilia kati.

 

Kazi ya Happy Birthday ya Harmonize ndiyo ambayo unaweza kuizungumzia mbele za watu na wakakuelewa kuhusu Fraga, kwa hiyo huwezi kumtaja Fraga bila kumtaja Harmonize. Hii maana yake ni kwamba bado Fraga hajafikia hatua ambayo mwenyewe anaweza kuwa anaamini kwamba amefikia, ya kuwa staa mkubwa Bongo.

 

Bado anahitaji kujifunza mengi kutoka kwa waliomtangulia, kama kweli ameamua kuanza kuimba, pia ni jambo la heri lakini hayo yote hayawezi kufanikiwa kama ataendelea kuchangamana na watu wenye sifa mbaya kwenye jamii, kwa sababu hata kama yeye hajihusishi kwa namna yoyote na ishu za ‘ngada’, iwe ni kuvuta au kuuza, ni rahisi watu kuamini kwamba na yeye ni walewale, wakampuuza na kuacha kumuunga mkono kwenye kazi zake.

 

Ipo mifano mingi ya wasanii wa Bongo Fleva ambao kwa kusaka njia za mkato kufikia mafanikio, walijikuta wakibebeshwa madawa kama punda na baadaye wakaishia kuwa watumiaji wakubwa na kupotea kabisa kwenye gemu, wengine hivi sasa hatunao tena duniani.

 

Nazungumza na Harmonize kwa sababu naambiwa ni miongoni mwa wasanii ambao Fraga anawaheshimu sana. Kwangu mimi Harmonize ni kama mlezi kwa Fraga kwa sababu kupitia yeye, jina lake limekuwa maarufu haraka. Kaa chini na huyu mdogo wako, mweleze kwamba hakuna aliyewahi kupita kwenye njia anayotaka kupita yeye akabaki salama!

 

Kama anaamini kipaji ndicho kitakachomtoa, basi awekeze nguvu kwenye utayarishaji wa muziki na kuimba kama mwenyewe alivyoamua, lakini kutaka mteremko kwa kuchangamana na wajanja wa mjini, hakutamuacha salama.

Comments are closed.