The House of Favourite Newspapers

Hawa Burundi Hawatoki Jumapili Taifa

JUMAPILI hawatoki Taifa. Inyeshe mvua au liwake jua, Burundi lazima wapigwe. Ndio msisitizo wa Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akisapotiwa na mastaa wenzie.

 

Stars ikicheza kwa kujiamini jijini hapa jana jioni, walilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.


Wenyeji walipachika bao lao dakika ya 81 kupitia kwa Cedrick Amissi ambaye alitumia makosa ya ukuta wa Stars. Cedrick alipigiwa mpira mrefu ambao uliwapita mabeki wa Stars ambao ni Shamte, Nyoni na Yondani na kupiga shuti kali ndani ya 18 ambalo lilimshinda Kaseja aliyeanza kucheza soka mwanzoni mwa miaka 2000.

 

Stars walionyesha ukomavu na utulivu wa aina yake chini ya Kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije na kuibana Burundi hadi waliposawazisha dakika ya 85 kupitia kwa Simon Msuva anayekipiga kwenye klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco.


Stars ilicheza kwa kujiamini muda mwingi wakitumia staili ya kujilinda kiumakini na mashambulizi ya kushtukiza ambayo ndiyo yaliyozaa bao la kusawazisha.

 

Burundi walijiachia na kushambulia muda mwingi ili kutengeneza mazingira ya kumaliza mchezo huo nyumbani lakini mbinu za Etienne na vijana wake ziliwazidi akili.

 

Stars inahitaji japo suluhu kwenye mechi ya marudiano Jumapili jioni Jijini Dar es Salaam kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwenye hatua ya makundi ambako ndiko inapotafutwa tiketi ya kwenda Kombe la Dunia.

 

STARS WAGOMA

Wakati wa mapumziko Stars waligoma kuingia vyumbani ili kuwavuruga kisaikolojia wenyeji. Stars waligoma kuingia vyumbani baada ya kuhisi harufu za ajabu ambazo walikuwa hawazielewi, hivyo viongozi wakashauri wabaki nje.

 

Katika mzozo huo, Watanzania watatu, walikamatwa na wanajeshi wa Burundi na kuwekwa kizuizini hadi tunakwenda mitamboni walikuwa hawajaachiwa.

 

Kikosi cha Stars: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Sure Boy, Himid Mao, Samatta, Msuva na Hassan Dilunga.

Comments are closed.