HAWA WANAPIGA KOTEKOTE !

Zuwena Mohammed,

MUZIKI wa Bongo Fleva kwa sasa upo kwenye ubora wake na hilo halina ubishi. Kumekuwa na ushindani mkubwa kwa wasanii wa kike na wa kiume ambapo mara kwa mara wamekuwa wakitoa ngoma na video kali.  Lakini haohao wasanii mbali na kufanya muziki, wapo waliotoka kwenye filamu na wengine wakipiga kotekote yaani kwenye filamu wanajua na kwenye muziki wanajua pia. Katika makala haya maalum, tunakuletea baadhi ya mastaa ambao wanapiga kotekote, yaani si ajabu kumuona kwenye filamu au muziki.

SHILOLE

Nyumbani kwao Igunga mkoani Tabora wanamjua kwa jina la Zuwena Mohammed, lakini ukiulizia kwa wajanja wengi wa Dar, wanamjua kama Shilole wengine watakwambia Shishi Baby na ukifika katika mgahawa wake watakwambia anaitwa Shishi Trump.

Filamu ya Fair Decision ya mwaka 2010 ambayo ndani yake yupo Irene Uwoya, Vincent Kigosi ‘Ray’, Jacob Steven ‘JB’ na wengine kibao ndiyo iliyomfanya watu wengi kumjua. Baadaye aliibuka katika filamu nyingine ambazo ni Don’t Play, Chungu ya Nafsi, Curse of Marriage, Zawadi ya Birthday na Talaka Yangu.

Kuonesha kuwa na muziki anauweza, Shilole alifanya staili ya mduara kwa kuachia ngoma kadhaa ambazo ni Lawama, Dume Dada na Paka la Bar na baadaye aliamua kubadili aina ya uimbaji na kufanya Bongo Fleva kamili akaachia Ngoma ya Nakomaa na Jiji, Chuna Buzi, Namchukua, Malele, Nyang’anyang’a, Say My Name, Hatutoi Kiki na Kigori.

Ukiachilia mbali muziki na filamu, Shilole pia ni bonge la mjasiriamali ambaye anajishughulisha na biashara ndogondogo na za mama ntilie akiwa na mgahawa wake wa Shishi Food.

HEMED SULEIMAN

Kwa muda mrefu Hemed amekuwa akitamba kwenye filamu na miongoni mwa alizosumbua nazo ni Confusion, Bad Girl, World of Benefit, The Secret of Toy, The Dream, Gumzo na nyingine nyingi. Licha ya kufanya poa kwenye filamu na kwenye muziki, jamaa yupo vizuri sana ambapo huko anatumia jina la Hemed PHD akifanya Muziki wa R&B na hadi sasa anashikilia ngoma kibao kwapani ambazo ni Imebaki Stori, Far Away, Mkimbie, Rest of My Life na Ulisema.

SNURA

Kama ilivyokuwa kwa Shilole, Snura ambaye jina lake halisi ni Snura Mushi naye alianzia kazi ya usanii katika Filamu ya Mfalme Seuta, Zinduna na Hitimisho. Mwaka 2007 alijiunga na Tuesday Kihangala ‘Mr Chuz’ akaibukia katika Tamthilia ya Jumba la Dhahabu na baada ya hapo mashavu ya filamu yakaanza kumiminika ambapo hadi sasa ameshacheza filamu kibao kama vile Fundo la Karne, Wrong Touch, Nafsi, Mimba, Limbwata, Ni Kosa Langu, Dikteta, Sabra, Almasi ya Damu na Ikwizu.

Kuonesha kuwa anapiga kotekote, kwenye muziki napo aliingia akifanya mduara kwenye Majanga, Ushaharibu, Najibadua, Shindu, Chura na Zungusha

KIDOA

Asha Salum ‘Kidoa’ anasimama kwa upande wa muziki kama muuza nyago ‘video vixen’ japokuwa kuimba yupo vizuri, lakini bado hajatoa ngoma ya peke yake.

Kidoa alifahamika zaidi kwenye video ya Wimbo wa Akadumba wa Nay wa Mitego. Kama ilivyokuwa kwa wengine, kwa Kidoa upande wa filamu kwake ni damudamu na ameshiriki filamu chache ikiwemo ya Kifaacho Mtu akiwa na Riyama Ally pamoja na Tamthilia ya Huba.

MALAIKA

Kama ulidhani anaweza muziki pekee, basi ulikuwa ukijidanganya. Malaika ambaye jina lake halisi ni Diana Exavery ni miongoni mwa mastaa wanaopiga kotekote yaani filamu yupo poa na muziki yupo poa.

Malaika alianza kung’ara katika filamu ya Mtunis ya Best Wife, baadaye alishiriki katika Filamu ya Mrembo Kikojozi, Yatima Asiyestahili pamoja na Binti Yangu akiwa kama mhusika mkuu. Kuonesha kuwa hakosei, kwenye Bongo Fleva napo aliingia na kutisha ambapo hadi sasa ana ngoma kibao zilizomweka kwenye chati mbalimbali ndani na nje ya nchi zikiwemo Saresare na Rarua.

SABBY ANGEL

Wengi wanamtambua kama ni msanii wa filamu kutokana na kucheza filamu nyingi kama vile Siyo Riziki, Sura Siyo Roho, Hard Price, Siri ya Giningi, Moto wa Radi na nyingine nyingi.

Mbali na filamu, Sabby pia amehusika katika Tamthilia ya Talaka akiwa kama mhusika mkuu, Duty na Dr Ray. Kama ilivyokuwa kwa mastaa wengine, Sabby naye anapiga kotekote ambapo anafanya vizuri kwenye muziki akiwa tayari na ngoma kadhaa kwenye TV ikiwemo ya Inahusu.

Snura

Malaika

Sabby

MAKALA: ANDREW CARLOS

Toa comment