The House of Favourite Newspapers

Haya Ndiyo Niliyoyaona Baharini-5

0

ILIPOISHIA KWENYE GAZETI LA IJUMAA:
Lakini kwa sababu tunaondoka kesho yake nilimwambia itakuwaje, Nurdin akamjibia.
“Tutachota maji ya bahari hakuna shaka.”
Nilimwangalia Nurdin kama niliyetaka kumuuliza itawezekanaje?
Yule mganga akadakia yeye: “Kaa chini nikuelekeze namna ya kuoga hayo maji ya baharini na siyo kama alivyosema huyo mwenzako.”
SASA ENDELEA:


Unatakiwa kuchota maji ya baharini kwa kutumia chombo cha chuma. Halafu unanawa uso, miguu na mikono sehemu isiyokuwa na maji ya bahari. Ina maana unaweza kuchota maji hayo halafu ukaenda kuogea hata utakapokwenda kulala, sawa?”
“Sawa.”
“Nimemaliza,” alisema huku akituangalia kwa macho kama anayesema tunasubiri nini.
Nilimwangalia Nurdin kwa macho ya kumuuliza inakuaje  kuhusu pesa ya ujira. Yule mzee akawa amejua nadhani, maana alisema:
“Nyie nendeni, mambo mengine yote niachieni mimi.”
Kwa sababu tulirudi bandarini, tulipofika mimi nilichukua kikombe cha chuma ambacho tunatumia kwa maji. Nikaenda chota maji ya baharini, nikarudi kwenye meli. Nilinawa uso, mikono na miguu muda huohuo kwenye kichumba cha kulala.
Nilipomaliza sasa, wakati narudisha kikombe kwenye vifaa vya kulia chakula, ghafla mbele yangu nikamwona msichana mrembo, mweupe, lakini nilipomtumbulia macho akatoweka.
Nilisimama kwa kusita kuendelea na safari. Nilianza kuhisi makubwa zaidi. Nilipojiwa na uamuzi wa kuendelea kutembea, nilisema niende kwa Nurdin ambaye alikuwa nje.
Nilipomsimulia Nurdin akasema kuwa, hiyo ni hali ya kawaida kwa bandari ambazo zinapakana na makazi yenye majini. Akasema:
“Kwanza mshukuru yule mtaalam, kwani bila yeye huyo mrembo lazima angekufuata na kukusukuma mpaka kuanguka chini kisha angekusonya ndipo angeondoka.”
“Ndivyo inavyokuwa Nurdin?”
“Bwana Tolu, utayaona mengi. Ilimradi umekingwa, sasa subiri. Unajua tatizo la baharini siyo majini tu, pia kuna roho za watu waliokufa kwa kuzama na meli. Wale wakishakufa, baadhi yao nafsi zao huelea majini na kufanya vituko.
“Unajua bwana Tolu, wengi wanasema roho ndiyo nafsi lakini mimi naamini kuna nafsi na kuna roho. Binadamu ana mambo matatu. Ana mwili halafu ana nafsi na ana roho. Japokuwa tafsiri inasema nafsi ndiyo roho. Nafsi ndiyo huleta tabu baada ya mtu kufa, lakini roho kuna sehemu huenda.”
Nilimwangalia Nurdin kwa hiyo simulizi yake na kuamini kwamba, ana mambo mengi sana kichwani mwake kuhusu matukio ya kwenye maji.

Na yeye alipomaliza kusema hayo, aliacha kutoa maelezo mengine, akawa ananiangalia tu. Nadhani alijua nitamuuliza swali lakini mimi sikumuuliza.
Nurdin alipoona nimekaa kimya akaniuliza kama niliishiwa maswali, nikamwambia kwa wakati ule sikuwa na swali.
“Mmh! Kweli unachosema?”
“Kwa sasa sina swali…”   Yeye akaendelea: “Kuna wakati tukiwa katikati ya bahari, huoni chochote pande zote, tunajikuta sisi wenyewe tukiwa kwenye barabara ya lami na meli inapita humo lakini si kwa kuburuzika bali kama inaendelea kuchanja maji.”
Nilishangaa sana maelezo ya Nurdin lakini safari hii sikumwonesha kwamba nimeshangaa kwa maelezo yake bali nilitulia tu.

Basi, jioni tuliingia melini kulala. Meli yetu ilikuwa ina huduma zote kama ndani ya nyumba. Tulilala mzigo ukiwa tayari, kesho yake asubuhi tulipoamka, hatukumuona nahodha licha ya kumtafuta kila kona ndani ya meli, tukaanza kuwa na wasiwasi.
Baada ya nusu saa tangu tuanze kumtafuta, tukamkuta kwenye dirisha lake la kazi amelala lakini hana nguo. Mzee mmoja, anaitwa Noroe ndiye aliyetangulia kumwona, akatwambia.
Nahodha alikuwa amelala, ikabidi tumwamshe. Tuliingiwa wasiwasi mkubwa sana kwa sababu wakati wa kumtafuta, tulifika mpaka kwenye hicho kichumba chake.

Ilibidi tumwamshe ili tumsikie nini kilimpata mwenzetu mpaka akawa vile alivyo, akasema eti alikuwa amelala juu ya meli usiku kwa sababu ya kutafuta hali ya hewa lakini ndiyo ameshtuka sasa.
Kwa hiyo kwa maneno yake ni kwamba, mle ndani ya chumba chake cha kazi aliingizwa bila ridhaa yake na aliingizwa muda huohuo kwani sisi tuliangalia hakuwepo.
Nurdin alipanda juu ya meli kufuata nguo za nahodha. Kweli alizikuta zimewekwa pamoja ikitangulia surauli chini kabisa, shati, singlendi na nguo ya ndani halafu ukachukuliwa mkanda wake wa suruali na kuzifunga nguo hizo kwa pamoja. Sendozi zilikuwa pembeni kabisa.

Kwa mujibu wa Nurdin wakati anachukua nguo hizo alisikia harufu ya pafyumu ingawa alijua ilitoka kwa mrembo ambaye ni jini na si ajabu alikuwa eneo hilohilo akimwangalia.
Nahodha alivaa nguo zake, akamshukuru Mungu kisha akatangaza kuanza safari. Safari hii tulitakiwa kwenda kisiwa kinaitwa Papua New Guinea, lakini safari yenyewe sasa, ndani ya dakika arobaini na tano tu baada ya kutoka bandarini, jambo kubwa sana likatutokea.
Je, ni jambo gani hilo? Usikose kusoma mkasa huu kwenye Gazeti la Ijumaa, kesho.

Leave A Reply