The House of Favourite Newspapers

Haya ni Mengi Ambayo Hukuyafahamu Kuhusu Filamu ya Titanic

0

JANA niliamua kuangalia tena na tena filamu ya Titanic, hakika sikuichoka na ninaweza kukiri kwamba ni filamu bora ya kimapenzi niliyowahi kuangalia maisha mwangu mbali na A Walk To Remember, The Notebook na Romeo And Juliet.

Nilitaka nifahamu mengi kuhusu filamu hii, lakini pia nilitaka nifahamu baadhi kuhusu mwandishi wa filamu hii au hata tukio zima, je, lilikuwa la kweli au ilikuwa ni filamu ya kutungwa.

James Cameron

Nimegundua mengi, yamenisisimua na kunifanya niipende zaidi filamu hii. Mtunzi na muongozaji wa filamu hii ni mzee fulani anaitwa James Cameron. Huyu ni mwandishi, wakati mwingine nilikuwa najisemea kwamba hakuna binadamu anayepewa vipaji viwili vinavyoendana, kama utunzi na uchoraji na kote ukawa mkali. Nilijiangalia mimi, hivi Nyemo Chilongani ninaweza kuwa mchoraji na wakati mimi pia ni mwandishi? Niliona haiwezekani kwani kama kujaribu kuchora, nilijaribu, nikafundishwa na watu wakali lakini nikaishi kujua kuchora makopa tu.

Tuanze na James Cameron.

Nilipofuatilia kuhusu James Cameron, niligundua kwamba huyu jamaa ana vipaji vyote, yeye ni mtunzi lakini pia ni mchoraji. Unaikumbuka ile picha ambayo Jack Dawson (Leonardo diCaprio) aliyomchora Rose DeWitt (Kate Winslet)? Ile picha hakuchora Jack bali aliyekuwa akiichora kwa kipindi kile alikuwa huyu mtunzi na muongozaji wa filamu hiyo, James Cameron.

Jamaa anatumia mkono wa kushoto, lakini wakati anamchora Rose, kwa kuwa Jack alikuwa akitumia mkono wa kulia, ilimbidi na yeye atumie mkono wa kulia kila ulipokuwa ukipigwa picha mkono wakati unachora.

Kumbe Leonardo Hakutakiwa kuwa Jack

Ndiyo ukweli huo. Wakati Cameron anatengeneza filamu hii kwenye maandishi kwanza, mtu aliyekuwa amemfikiria alikuwa ni Leonardo diCaprio ambaye aliigiza kama Jack ila alipowafikishia wenye kampuni yao, wakamwambia alitakiwa kumbadilisha, amuweke Brad Pitt au hata Tom Cruise kwa kuwa ndiyo walikuwa waigizaji wenye majina makubwa kipindi hicho.

Tom Cruise, Brad Pitt

Hebu jifikirie, hivi kweli Tom Cruise angeweza kuuvaa uhusika wa Jack kama ilivyokuwa kwa Leonardo? Au hata Brat Pitt angeweza kuuvaa? Hakika alipoigiza Leonardo, alipendeza zaidi.

Alichokifanya Cameron ni kuleta ubishi tu kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima Leonardo achukue nafasi na kuigiza kama Jack kitu ambacho alifanikiwa kwa asilimia zote.

Hata Kate Hakutakiwa Kuigiza Kama Rose

Huo ndiyo ukweli, Kate Winslet hakutakiwa kuigiza kama Rose, mtu aliyekuwa amepewa nafasi alikuwa Cameron Diaz, mwanamama hodari sana katika uigizaji. Pia alichaguliwa mwanamuziki Madonna, walichokuwa wakikifanya watayarishaji ni kuchukua mtu mwenye jina kubwa ili filamu iuze sana ila Cameron akakataa, akawachukua watu alioowapanga yeye, filamu ikauzwa na kuvunja rekodi duniani.

Madonna

Nafasi ya Jack Aliwekwa Mwingine

Kuna jamaa ambaye aliwekwa kucheza filamu hiyo kama Jack (Bahati mbaya nimemsahau jina). Jamaa alicheza scene ya kwanza, likatokea la kutokea akatolewa na kuwekwa Leonardo.

Scene ya Kwanza Jack na Rose Kuonana ni Kwenye Mchoro

Inaweza ikakushangaza lakini scene ya kwanza kabisa ya wawili hao kuonana ilikuwa ni pale Rose alipotaka kuchorwa na Jack. Wanasema ilikuwa ngumu sana kwa Kate kumvulia nguo Leonardo kwa kuwa hakuwa akimjua, walikutana hapo kwa mara ya kwanza, ilikuwaje akae uchi mbele yake? Hata kama walikuwa wakiigiza, aliona kungekuwa na ugumu.

Baada ya kujifikiria sana, hatimaye akakubali, ila kabla ya picha kuanza kupigwa, Kate akamvulia Leonardo nguo, akamwangalia ili asije kutetemeka mara watakapoanza kuigiza.

Hebu jifikirie, mtu umekutana naye kwa mara ya kwanza, halafu wanakwambia muigize kama mmefahamiana kwa kipindi kirefu, tena mkiwa wapenzi! Inahitaji kipaji cha hali ya juu.

Ukiangalia scene hiyo, ingawa ndiyo ilikuwa ya kwanza lakini upendo ulionekana machoni mwao kiasi kwamba hata ukiambiwa kwamba ndani ya chumba kile Rose alipochorwa ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa wawili hao kuonana na kuigiza, ungekataa.

Leonardo Alikosea kwa Bahati Mbaya, Cameron akapenda

Ukiangalia kipande hicho wakati Rose amevua nguo, Jack alimwambia “Over on the Bed. Coach” (Yaani akae kitandani. Kwenye kochi) Hapo Leonardo alikosea, ilibidi amwambie moja kwa moja kwamba akae kwenye kochi na si kitanda. Ila kwa jinsi alivyokosea, Cameron akapenda na kuruhusu kipande hicho kiende na kisikatwe.

Naye Rose Akaongezea Mstari Wake

Si kila kitu kilichozungumzwa kilipangwa. Kuna kipindi pale Jack alipokuwa na rafiki yake mbele ya meli, wakasimama kisha kusema “I am the King Of The World” mstari huo haukuwa umepangwa na hata Rose kule karibu na mwisho alivyomwambia Jack pale walipokuwa wakati meli inazama “Jack, this is where we first met’ (Jack, hapa ndipo tulipokutana mara ya kwanza) haukuwa umeandikwa, ila Rose alisema tu, kweli ukafaa.

Rose Alimtemea Mate Cal, Haikuwa Kwenye Script

Huo ndiyo ukweli. Kuna scene inaonyesha kwamba Rose alimtemea mate Cal, wengi wanahisi kwamba ilipangwa lakini haikuwa hivyo, wala haikuwekwa katika script, ilikubaliwa kwamba Rose amchome Cal na kibanio cha nywele lakini aliifanya tu na ikamfurahisha Cameron na ndiyo maana hata ukiuangalia uso wa Cal alivyotemewa mate alishangaa kwani hakuwa ameambiwa kufanyiwa hivyo.

Kate Alitaka Kuacha Kuigiza

Rose ana matatizo ya pumu. Wakati wakiigiza, pale mwishoni alipokuwa kwenye maji, alipewa nguo iliyolowanishwa, maji yalikuwa ya baridi sana na alitakiwa kukaa humo kwa dakika kadhaa wakati wakipiga picha za filamu hiyo.

Rose akaanza kupata matatizo, akatoka haraka sana, akakaa pembeni na kumwambia Cameron kwamba asingeweza kuigiza tena kwani alikuwa akiumwa. Cameron akambembeleza sana sana hatimaye akakubali na kumalizia.

Leonardo na Kate ni Wapenzi?

Walianza kuigiza kwenye filamu hiyo, ukweli ni kwamba wakatokea kupendana na kuwa wapenzi. Wakati wakiendelea kuigiza, Kate anasema kwamba wakati mwingine walikuwa wakijifungia chumbani wawili na kufanya mapenzi kikwelikweli.

 

Mbali na muvi, walipendana sana. Na juzijuzi tu Kate alihojiwa alipokuwa akiigiza filamu mpya ya The Mountain Between Us, anasema kwamba wakati mwingine alikuwa akimtumia Leonardo meseji na kumwambia jinsi walivyokuwa wakiigiza na meseji hizo alizisema kama “Mpenzi! Tunaigiza, kuna baridi sana huku kiasi kwamba natamani hata ungekuwa karibu nami.” Anasema Rose na Leonardo kujibu, yaani kwa kifupi, tangu walipoigiza filamu ile, mpaka leo watu hawa wanapendana sana japokuwa kila mtu ana familia yake.

Na Vipi Kuhusu Ile Couple ya Wazee Iliyokufa?

Kama umeiangalia filamu hiyo utakuwa umekiona kile kipande babu na bibi wamelala kitandani wamekumbatiana huku maji yakianza kuingia kwenye chumba chao.

Hicho kipande kiliwekwa kwa ajili ya kuwaenzi Ida na Isidor Strauss ambao walikuwa mume na mke wazee waliokufa katika ajali hiyo ya meli mwaka 1912 huku wakiwa wamiliki wa duka la Macy nchini Uingereza.

Je, Ni Kweli Kilichoigizwa Ndicho Kilichotokea?

Si kweli! Kilichoigizwa si kilichotokea bali baadhi ya majina ya wahusika walikuwepo. Kwa mfano, Rose DeWitt. Katika meli hiyo iliyozama mwaka 1912, kulikuwa na abiria aliyekuwa na jina hilo lakini pia kulikuwa na mwanaume aliyeitwa Joseph Dawson.

Huyo alikuwa mwanajeshi, kaburini kwake kuliandikwa J Dawson. Cameron hakulifahamu hilo ila baada ya filamu kutolewa, akagundua kwamba kulikuwa na mtu aliyeitwa J Dawson na aliliona hata kaburi lake.

Je! Ni kweli Wawili Hao Walikuwa na Uhusiano?

Hapana! Walikuwa ni abiria ambao hawakuwa wakijuana kabisa, alichokifanya Cameron ni kutengeneza muvi na kuwafanya kama watu waliokuwa wakijuana, kupitia wao, akatengeneza filamu.

Na Vipi Kuhusu Cal, Alikuwepo?

Cal ni yule mchumba wa Rose ambaye alikuwa tajiri, alikuwa akisafiri naye kuelekea Marekani. Ni kweli mwanaume huyo alikuwepo ndani ya meli, alikuwa tajiri, alikuwa miongoni mwa watu waliopona kwenye ajali hiyo.

Cal (kulia) wa ukweli wa miaka hiyo aliyenusurika kwenye ajali ya Titanic

Mwanaume huyo alijiua mwaka 1929 baada ya hali ya uchumi kubadilika na biashara zake kuanza kuyumba. Ili kutengeneza uhalisia, Cameron akamuingiza mwanaume huyo kwenye filamu hiyo na kumfanya kama alikuwa mpenzi wa Rose.

Cha Kushangaza

Filamu ya Titanic ilitumia kiasi kikubwa cha pesa kuitengeneza kuliko hata meli halisi gharama iliyotumia mwaka 1912. Meli hiyo ilitumia dola 7.5 milioni ambazo kwa sasa ingekuwa dola 150 milioni na wakati filamu ilitumia dola milioni 200 kuitengeneza.

Muvi Ilikuwa Ndefu kwa saa 36

Wakati filamu ikiwa imekwishatengenezwa na kupelekewa James Horner kwa ajili ya kuikata, anasema ilikuwa ndefu kwa saa 36 hivyo kuipunguza mpaka kuwa saa 3 na dakika 6.

Scene ya Mwisho Ilikuwa ni saa 2:20

Wakati Jack anamsubiri Rose katika scene ya mwisho kisha kukumbatiana, kwa nyuma saa ilikuwa ikionyesha ni saa 2:20, ndio muda huohuo ambao meli halisi ya Titanic ilizama.

Waigizaji Walipewa saa Tatu Kufundishwa

Cameron hakutaka kukurupuka muvi iishe haraka, alijua kwamba waigizaji walitakiwa kuigiza kama watu wa mwaka 1912 hivyo walikuwa wakitumia saa tatu kuwafundisha jinsi watu wa kipindi hicho walivyokuwa, tabia zao na mambo mbalimbali waliyokuwa wakiyafanya ili muvi kubeba uhalisia.

Makala imeandikwa na Nyemo Chilongani, (GPL)

Leave A Reply