The House of Favourite Newspapers

‘Haydom Marathon’ Mbio Zinaookoa Maisha

0

HAYDOM Marathon ni moja ya mbio zinazojulikana nchini kutokana na kushirikisha watu wengi kila mwaka tangu zilipoanza mwaka 2018, lengo kuu ikiwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Hospital ya Kilutheri Haydom mkoani Manyara.

 

Kaulimbiu ya mbio hizi ikisema: ‘Kimbia kuokoa maisha.’

Mbio hizo zimekuwa na umaarufu mkubwa kutokana na kushirikisha wanariadha mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi hasa Norway, Uholanzi na Marekani ambao huja kukimbia kwa ajili ya kufanya changizo ili kuokoa maisha ya watu wengi hasa wagonjwa wa mikoa ya kanda ya kaskazini na kanda ya kati ambao hupata huduma ya matibabu ya kiafya katika hospital ya Haydom.

Haydom Marathon ambayo inaandaliwa na uongozi wa Hospital ya Kilutheri Haydom (HLH) kwa kushirikiana Christian Sport Contact (CHRISC) mwaka huu zimechelewa kufanyika kutokana na kuenea kwa virusi vya corona vilivyotikisha dunia na kusababisha mambo mengi kusuasua na hata kukwamisha vitu vingine visifanyike.


Mbio hizo hufanyika kila mwaka kwa kuanzia katika viwanja vya shule ya msingi Haydom ambapo lengo huwa linabadilika kutokana na mahitaji ya hospitali na hufanyika mwezi huu ambapo zilitakiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu, lakini kutokana na kuenea kwa virusi vya corona zilisitishwa na zimepangwa kufanyika Jumamosi ya Desemba 12 katika viwanja vya shule ya msingi Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara.

Dr Vickfarajaeli ambaye ni kaimu msaidizi, mkurugenzi wa Tiba Hospital ya Kilutheri Haydom, amesema wameamua kutumia mchezo wa riadha ili  kupata fedha kwa ajili ya kujenga wodi ya watoto wachanga na kununua vifaa kwani wanaamini kwa kupitia mashindano ya riadha lengo lao litafanikiwa.

Amesema maandalizi yanaendelea kushika kasi ambapo katika mbio hizo ambazo zitafanyika Jumamosi, wanategemea wanariadha na wadau wa michezo pamoja na wananchi wa mikoa ya Manyara, Arusha, Singida na mikoa mingine watashiriki na kujitokeza kwa wingi ili  kuwachangia.


Amesema hali ya usalama ni nzuri sana wameshirikiana na jeshi la Polisi Haydom kuhakisha ulinzi unaimarishwa Jumamosi lakini pia wameshirikiana na serikali ya vijijini ambayo mashindano yatapita na kuongeza kuwa ni msimu wa tatu sasa mbio hizo zinafanyika na zimeendelea kupata umaarufu mkubwa kutokana na namna ambavyo wamekuwa wakiyaboresha.

Alifafanua kuwa mbali na kuwa mbio zao zimekuwa zikifanyika kwa ajili ya kufanya changizo ili kuboresha huduma za afya,  pia zimekuwa ni chanzo cha ajira kwa vijana ambao ni wanariadha na zimekuwa pia zikiibua vipaji na kuongeza kuwa msimu wa kwanza mwaka 2018 lengo la mbio ilikuwa ni kufanya changizo ili kununua mashine mpya ya CT-Scan na hilo lilifanikiwa  ambapo msimu wa pili mwaka jana lengo ilikuwa ni kufanya changizo kupata fedha ya kujenga wodi ya watoto wachanga.

Amesema zoezi la uandikishaji wa wanariadha linafanyika katika duka la vitabu lililopo ndani ya hospitali ya Kilutheri Haydom ambapo usajili kwa kilomita 21, km 10, km 2 (fun run) na mita 100 fun run kwa watu wazima ni shilingi 10,000 na watoto pamoja na wanafunzi walio chini ya umri wa miaka 15 ni sh. 2,000,ambapo amewaomba wazazi kuleta watoto wao kushiriki,lakini pia wadau kujitokeza kwa wingi.

Mbio za Haydom Marathon km 10 zitaanzia shule ya msingi Haydom na kupitia kijiji cha Harar na Basonyangwe na kurudi kupitia kati kati ya mji wa Haydom na kumalizikia uwanja wa shule ya msingi Haydom ambapo kwa km 21 watazunguka mara mbili eneo hilo.

Washindi wa km 21 mbio za Haydom Marathon mwaka 2019, wanaume alikuwa ni mwanariadha Bernard Musa kutoka Kenya aliyeongoza kwa muda wa saa 1:17:08 akifuatiwa na Stephano Huche kutoka Arusha kwa saa 1:17:16 na nafasi ya tatu ikaenda kwa Ezekiel Jafari kwa muda saa 1:17: 21 .

Wanawake mshindi wa kwanza alikuwa ni Cheruto Isgah kutoka Kenya aliyemaliza kwa kutumia muda wa saa 1:25:42 akifutiwa na Failuna Abdi kwa muda wa saa 1:26:28 na nafasi ya tatu ikashikiliwa na Catherine Lange wa Magereza Arusha kwa muda wa 1:27:36.

Zawadi kwa mshindi wa kwanza km 21 wanawake na wanaume alipata sh. milioni moja, wa pili laki sita na wa tatu laki nne.

Kwa washindi kilomita 10, mshindi wa kwanza alipata sh. laki tano, na wa pili shilingi laki mbili na nusu huku wa tatu akiondoka na laki mbili, na medali zilitolewa kwa washiriki wote.

#Habari na Kennedy Lucas, GPL

Leave A Reply