The House of Favourite Newspapers

Hii Ya Harmo Vs Van Boy Ni Utoto

0

SIKU za nyuma kulikuwa na upinzani mkubwa wa kimuziki kati ya Diamond Platinumz na Harmonize ‘Konde Boy’ au Harmo lakini sasa mambo yamebadilika.

 

Tumeshuhudia Harmo akichuana na Rayvanny ‘Van Boy’ kuhusiana mambo ambayo wakubwa akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameyaita ya kitoto.Picha ilianza hivi, kwa kipindi kifupi, watu waliaminishwa kuwa Harmo alikuwa katika mahaba mazito na msanii wa filamu Kajala.

 

Ghafla, Harmo akaonekana hadharani na Kajala na kinda lake Paula wakiwa Mlimani City wakila raha za dunia.Lakini kimuziki Harmo anaimba huku watu wakiamini kwamba Mondi yupo juu kuliko Harmo na mtu ambaye hataamini hivyo, ataonekana ni zuzu tu.

Hadi ninapoandika makala haya ni wazi kwamba Mondi bado yupo juu katika fani ya muziki wa Bongo Fleva.Wabongo wana tabia ya kumchoka msanii hata kama yupo vipi lakini sivyo kwa Mondi ambaye kila kukicha anabuni mambo ili azidi kuwa kileleni.Mondi aliwahi kupambanishwa na Ali Kiba katika muziki wao na zogo likawa kubwa sana, wapenzi wa muziki wakamtwisha Ali Kiba zigo la misumari ili apambane kimuziki na Mondi.

 

Lakini mara kadhaa Ali Kiba hakupenda kulinganishwa kimuziki na Mondi kwa madai kwamba kila mmoja anapitia njia yake kimuziki kuelekea kwenye mafanikio.Hii ilifanya baadhi ya watu wamuone Ali Kiba au King Kiba kama mtu mwenye dharau lakini ukweli ni kwamba waliokosea ni mashabiki waliokuwa wakiwalinganisha kana kwamba kuna siku waliwahi kushindanishwa jukwaani.

 

Katika mahojiano mbalimbali ambayo King Kiba aliwahi kuyafanya nikiwemo mimi alikuwa anakwepa kuzungumzia nani zaidi kimuziki kati yake na Mondi.

 

Hivyo ndivyo ilivyokuwa wakati wa kugombea nani zaidi kati ya King Kiba na Mond japokuwa wao wenyewe hawakuwa na ushindani rasmi wa jukwaani kuhusu muziki wao lakini nikiri kwamba bato hiyo ilikuza muziki wa Bongo Fleva na kuvutia mashabiki wengi wa muziki.Ukweli ni kwamba wakati wa bato hiyo hakukuwa na Konde Boy wala Van Boy hivyo Mondi alibaki peke yake kupambana na King Kiba.

 

Lakini picha inaanza baada ya Van Boy kudaiwa kufunguliwa ofisi ambayo ni ya kurekodi yaani lebo ya muziki iitwayo Next Level.

 

Inasemekana akaombwa amnyemelee mtoto wa Kajala, Paula! Inasemekana nia ilikuwa kumkera Harmo ambaye alishatangaza kwamba Kajala, mama wa Paula ni mpenzi wake anayempenda sana katika mtima wake kuliko wanawake wote.

 

Harmo akaingia ‘kichwakichwa’ kwenye gemu ya Van Boy na Paula na ikawa sasa ni Paula na Harmo.Mambo hayo yananikumbusha huko majuu kulikokuwa na bato kati ya wasanii DMX na Jah Rule ambapo Jah alifaidika zaidi na gemu hiyo.Lakini pia nakumbuka bato kati ya 50 Cent na Rick Ross pamoja na Kanye West. Yote hayo yaliwapandisha Kanye na Rick Ross The Boss na kumtuliza 50 Cent.

 

Sasa Mondi kwa upande wa Bongo hakutaka hayo machale yakampata kupitia ngoma yake kupitia Wasafi Classic Baby (WCB) kwa ngoma yake aliyoipa jina la Zilipendwa dhidi ya ngoma ya Ali Kiba aliyoiita Seduce Me.

 

Ukweli ni kwamba kitu chochote kikiwa na upinzani huwa kizuri sana na kupata mashabiki hii maana yake Harmo kwa kutoa ngoma ya ubishani na Mondi ingepata watazamaji wengi kwa sababu Mondi kiukweli hakuna ubishi kwamba ana mashabiki wengi.

 

Hii maana yake kama ushindani wa kimuziki wa Harmo na Mondi ukiendelea, anayefaidika ni Harmo kwa kuwa mashabiki wengi wa Mondi watambeba.Mondi alifanya kosa moja tu la kutoa ngoma ya Zilipendwa saa chache tu baada ya King Kiba kuachia ngoma ya Seduce Me.

 

Huruma ya wapenzi wa muziki ilifanya ngoma hiyo ife kifo cha asili (natural death)! Huku Seduce Me ikikimbiza anga za muziki mara mbili ya ubora wake.Haikuwa ngoma ya ajabu kwa Kiba ila watu waliisapoti kazi yake kwa nguvu kwa kuamini anapigwa vita sana na kuonewa na mwenzake.Ukweli ni kwamba siku hizi wasanii wana kiki zao katika kukuza muziki wao.

 

Hizi kiki zinaharibu sana wasanii wetu na sasa zimevuka mipaka kwani zinaumiza nafsi na niwaombe wasanii wadogo waache kiki za kijinga za kudhalilishana.Fanyeni kiki za kukuza muziki wenu kwa kuwa muziki ni kitega uchumi kikubwa katika dunia ya leo. Mkifanya ujinga kama tulioushuhudia hivi karibuni kati ya Harmo na Van Boy inakuwa mnajipiga ngwala wenyewe kwa sababu watu watawadharau na viongozi wa serikali wataona mnafanya mambo kitoto, hivyo kujishushia heshima badala ya kujijenga.

MAKALA na ELVAN STAMBULI | GPL

Leave A Reply