The House of Favourite Newspapers

Hili la Kidoa na Samatta, limewakuta pia Eto’o na Ngassa

0

IMG-20160112-WA0005Mshambuliaji nyota wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta akiwa na Kidoa.

KILA mpenda soka wa nchi hii analitambua jina la mshambuliaji nyota wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta, ingawa wapo wengi wengine ambao hawajawahi kumuona akicheza. Miongoni mwa waliowahi kumuona akifanya vitu vyake uwanjani, mimi ni miongoni mwao.

Nilimtazama pale uwanja wa Uhuru wakati huo akiitu mikia African Lyon iliyo badili jina kutoka Mbagala Market na baadaye akiichezea Simba, kabla ya kutimkia Tout Puissant Mazembe ya pale Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Uwanjani, ninamfahamu Samata kama mchezaji mpambanaji, sifa ambayo imempatia mafanikio makubwa tuliyoshuhudia hivi karibuni, alipopata heshima ya kuwa Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani.

Hii ndiyo sifa inayolitangaza jina la nchi yetu nje, kwani kabla ya hapo, alitwaa pia kiatu cha dhahabu kwa kuibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana ambako timu yake iliibuka kuwa bingwa.

Unapomuona uwanjani, kama shabiki, unajipa matumaini kuwa wakati wowote anaweza kubadili matokeo, kwani haogopi kuchezewa rafu na hakati tamaa. Nje ya uwanja, Samatta ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye misimamo kuhusu maisha yao.

Samatta sasa ni staa wa soka ngazi ya Afrika, kwa sababu popote atakapotua, watu wa mpira watamtambua na kumpa heshima anayostahili. Moja ya madhara ya kuwa staa mkubwa, ni kuwa chanzo muhimu cha habari, bila kujali ni wapi na lini na chombo gani.

Wiki chache zilizopita baada ya Samatta kuileta nyumbani tuzo yake hiyo, alikuwa mtu muhimu katika hafla nyingi, kila moja ikilenga kumpongeza.

Walijitokeza pia watu wengi, marafiki na jamaa wa familia ya soka, ambao kila mmoja kwa wakati wake, alipenda kujumuika naye, ili angalau kuonesha jinsi gani alifurahia mafanikio yake.
Miongoni mwa waliopata fursa ya kukutana na Samatta ni binti mmoja anayeitwa Asha Salum ‘Kidoa’, ambaye wiki kadhaa kabla, alipata ushindi wa shindano la msanii wa kike mwenye mvuto, linaloendeshwa na gazeti hili kwa jina la Ijumaa Sexiest Girl 2015.

Walionwa wakiwa pamoja katika Hoteli ya Giraffe, iliyopo jijini Dar. Kwa gazeti hili, picha ya wawili hao wakiwa pamoja ni habari, tena habari kubwa. Baada ya kuandikwa kunaswa kwao, Samatta alikuja juu na kutoa maneno yenye kuonesha kukerwa kwake, katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, akimshutumu binti huyo kuwa ‘alicheza’ mchezo na gazeti hili ili wakutwe pamoja.

Siwezi kumzuia Samatta kutoa maoni yake juu ya jambo lolote kama alivyofanya, lakini ninachopenda kumshauri, kwa hadhi aliyofikia ni muhimu sana kwake kuwa makini kama hataki mambo kama haya yamkute, iwe Tanzania au popote atakapokuwepo.

Gazeti hili pamoja na mengine ya Global Publishers linashughulika na mastaa, bila kujali ni wa aina gani, mradi wana majina makubwa kwa jamii yetu. Na Samatta siyo mwanasoka wa kwanza kuandikwa, kwani huko nyuma, tuliwahi kumnasa pia nyota mkubwa kuliko yeye, Samuel Eto’o wa Cameroon akiwa na mwanadada anayefahamika kwa jina la Mboni.

Tuliwahi pia kuandika kuhusu Mrisho Ngassa akifanya mambo yake na mrembo f’lani. Je, mabinti waliokutwa na mastaa hawa nao walitengeneza mchongo ili wanaswe?
Kama Samatta anasema Kidoa alifanya mchezo na sisi, basi nina hofu kubwa na usalama wake yeye binafsi. Anadai binti huyo ni shemeji yake (sijui kwa nani) na kwamba ndiye aliyepanga wakakutane katika hoteli hiyo.

Sasa Samatta, unaendaje kukutana na shemeji yako hotelini, tena usiku? Mimi ninavyojua, katika ahadi za kukutana na akina dada, mwanaume ndiyo hupanga sehemu na muda wa kukutana, siyo wao!

Hatukuandika habari za Samatta kwa sababu tunamuonea wivu, bali kwa sababu ndiyo kazi yetu, kama yeye mpira ilivyo kazi yake. Na hii haitakuwa Bongo tu, hata akienda pale Ubelgiji au kwingineko Ulaya magazeti kama yetu yapo na wao ndo hatari zaidi. Mbona mastaa wa Ulaya tunasoma kashfa zao kila siku, au nao wanachezeshewa michezo na ‘ma-Ijumaa’ ya huko?

Nikuambie tu Mbwana kwamba, Ijumaa ni gazeti linaloandika habari za kweli kuhusu mastaa na habari nyingine za kijamii hivyo kwa kuwa unakiri kufika hotelini pale na Kidoa ambaye unadai ni shemeji yako, huna sababu ya kuumia, ndiyo ustaa huo braza.

Leave A Reply