The House of Favourite Newspapers

HIVI NDIVYO ‘HAUSIBOI’ ALIVYOMCHINJA MTOTO WA BOSI WAKE

DAR ES SALAAM: “Mwanangu amechinjwa kikatili jamani, kwani kamkosea nini mpaka amuue kikatili, naumia jamani, moyo wangu umejeruhiwa, Prosper sitamuona tena mimiii… ameuawa kinyama bila hatia….” Hiyo ni sehemu ya maneno ya kuhuzunisha ya Paulina Mofuga, mama wa mtoto aitwaye Prosper Myovela ambaye hivi karibuni aliuawa kikatili.

AMECHINJWA, AMEKUFA!

Ni tukio la kusikitisha lililotokea katika Mtaa wa Mnazi Mmoja, Kata ya Kitwiru mkoani Iringa ambapo mtoto Prosper mwenye umri wa miaka 4 anadaiwa kuuawa kwa kuchinjwa na ‘hausiboi’ aitwaye Geofrey Joseph (29) kisha mwili wake kuuweka kwenye kiroba.

BIBI WA MAREHEMU ASIMULIA

Akizungumza na Uwazi kwa huzuni, bibi wa mtoto huyo, Maimuna Chang’a alisema siku ya tukio, saa nane mchana akiwa nje ya nyumba wanayoishi na mtoto huyo akifanya shughuli zake za kilimo, ‘hausiboi’ huyo alirejea nyumbani huku akiwa anakimbia kisha akapitiliza ndani.

“Baada ya Geofrey kuingia ndani, ghafla nikasikia mayowe, mtoto akawa analia sana, mara kimya kikatawala, baada ya kama robo saa hivi nikasema hapana, ngoja niende nikajue nini kimetokea. “Nilipofika ndani nilimuona kijana huyo akiwa na wasiwasi kuashiria kuwa kuna kitu amekifanya, nilipomuuliza kuna nini kimetokea, akaanza kuniomba msamaha na kuniambia eti amemuua mjukuu wangu kwa bahati mbaya.

“Kwanza niliishiwa nguvu kusikia maneno yale, sikuamini, nguvu zikanijia, nikambana nikimtaka anionyeshe alipo mjukuu wangu, akanionyeshea kiroba. Nikamuuliza unasemaje wewe? Akaniambia eti Prosper yuko kwenye kile kiroba na pembeni kulikuwa na kisu na panga.

“Nilishtuka sana, nikakimbilia kwenda kuchungulia kwenye kile kiroba, kweli nikamkuta mjukuu wangu akiwa anahema kwa tabu sana lakini hapo sikuwa nimejua kuwa, alikuwa amekatwa eneo la shingo. “Hapohapo nikajiwa na ujasiri wa hali ya juu, nikamshika yule kijana na kumsukumia kwenye moja ya vyumba, nikafunga mlango kisha kuanza kupiga mayowe, watu wakajaa na ndipo nikawaelezea kilichotokea.

“Wananchi walipatwa na hasira sana kusikia ukatili aliofanya kijana huyo, wakamkamata na kumpeleka katika kituo cha polisi na mtoto naye akapelekwa hospitalini kujaribu kuokoa uhai wake. Hata hivyo alikata roho njiani, nimeumia sana.

“Shingo ya mtoto ilikuwa imechinjwa na kisu au panga, nashindwa kuamini kama kweli ukatili huu ni kwa sababu eti ya kuombwa muwa tu kwani Prosper hakuwa na tabia ya kuombaomba na kijana mwenyewe sijawahi kumuona akinywa pombe wala kuvuta sigara, hata sijui ni nini kimemfanya amuue mjukuu wangu kinyama hivi,” alisimulia bibi huyo.

MSIKIE MAMA MZAZI

Mama wa marehemu, Paulina Mofuga alisema siku ya tukio yeye alitoka nyumbani na kwenda mjini kwenye mihangaiko yake huku akimuacha mwanaye salama na bibi yake lakini baadaye akaja kusikia taarifa hizo ambazo zilimuweka kwenye wakati mgumu sana. “Hata kama ni wewe, unasikia mwanao kauawa kinyama kiasi kile, hivi utajisikiaje? Inauma kwa kweli, inaumaaa….” alisema mama huyo ambaye alimaliza kwa kilio.

MSIKIE BABA WA MAREHEMU

Akizungumza na Uwazi huku uso wake ukiwa umejawa na simanzi, baba wa mtoto Prosper, Shaibu Myovela alisema: “Siwezi hata kusimulia, nina maumivu makali sana moyoni, mwanangu ameuawa, daah…”

Akimzungumzia mtuhumiwa wa mauaji hayo ya kutisha, baba huyo alisema, alikuwa akiishi naye nyumbani kwake akiwa anafanya kazi za kulima bustani na hakuwa akimlipa mshahara zaidi ya kumpa pesa ya kula, kulala na malazi. “Huyu kijana ni mwenyeji wa Kilolo na nimeishi naye hapa kwa muda kidogo ila sijui nini kimemsukuma afanye ukatili huu, sisi tunaviachia vyombo vya sheria vifanye kazi yao,” alisema baba huyo.

POLISI WATHIBITISHA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 4, saa nane mchana katika maeneo ya Kibwabwa B ndani ya Manispaa ya Iringa .

Bwire alisema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alikuwa nyumbani na marehemu, marehemu alimuomba mtuhumiwa kipande cha muwa alichokuwa anakula na mtuhumiwa alipokataa mtoto huyo alimtolea mtuhumiwa lugha ya kuudhi na ndipo alipomshambulia. Bwire alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwani bado haiwaingii akilini mtu mwenye akili timamu kumuua mtoto kisa kumuomba mua hivyo watampeleka akapimwe akili yake kama ni mzima ama laa.

Gazeti hili linawapa pole ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya marehemu Prosper na tunawaombea kwa Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu tukiamini kwamba sheria itachukua mkondo wake.

STORI: FRANCIS GODWIN, UWAZI

Comments are closed.