The House of Favourite Newspapers

Hivi Ndivyo Sinema ya Faru John Inavyochezwa

faru-john

STORI: MWANDISHI WETU | Gaztei la Risasi Jumamosi, Toleo la Desemba 24, 2016

DAR ES SALAAM: Ile sinema ya kifo chenye maswali mengi cha mnyama Faru aliyepewa jina la John (38) sasa imefika patamu kufuatia sakata hilo kuashiria kuwepo kwa usiri mkubwa ndani yake na maswali mengi ambayo, waziri mwenye dhamana, Profesa Jumanne Maghembe ndiye anapaswa kujibu, Risasi Jumamosi linakupa.

Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kwamba ifikapo Desemba 8, umpelekee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha Faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo na kupelekwa katika eneo la Gurumeti, Serengeti, Desemba 17, 2015 na baadaye kusemekena amekufa.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Hapo ndipo Faru John alipoanza kujipatia umaarufu mkubwa nchini na kimataifa kwani kifo chake kilionekana kugubikwa na sintofahamu nyingi hasa ikizingatiwa kuwa, wakati wa uhamisho huo, Rais John Pombe Magufuli alikuwa akifanya uteuzi wa
baraza lake jipya la mawaziri baada ya kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

faru-johnAPELEKEWA NYARAKA

Desemba 8, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti kama alivyoamuru kwenye ziara yake.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, waziri mkuu alisema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.

Alisema: “Nimepokea taarifa yenu saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu,” alisema katika kikao hicho.

Akisoma taarifa hiyo mbele ya waziri mkuu, Profesa Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati Faru John anahamishwa, alikuwa tayari ana watoto 26 ya faru wote waliopo ndani ya kreta hiyo.

Alisema: “Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ (mazaliano) ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.

Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya Faru John ilianza kudorora na alikufa Agosti 18, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya kuwalinda tembo na faru. Kamati hiyo iliundwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

back-risasiiiiGaztei la Risasi Jumamosi, Toleo la Desemba 24, 2016

TAMKO LA WAZIRI MKUU BAADA YA TAARIFA

Waziri Mkuu alisema serikali imeunda tume kuchunguza taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Grumeti, Serengeti.

Tume hiyo pia itatafuta kaburi la faru huyo ambaye inadaiwa alikufa. Alisema timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Grumet kwa ajili ya kutafuta kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya faru huyo.

Alisema, baadaye tume hiyo itakwenda kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wa faru huyo na kuvilinganisha na pembe alizopelekewa ili kubaini kama kweli zilikuwa ni za Faru John au la! Waziri Majaliwa alisema wakati ‘John’ akiwa Grumet, taarifa zilidai ni mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza alibaini hakuwa na ugonjwa wowote.

“Daktari alimpima tena kwa mara ya pili, taarifa zikasema tena si mgonjwa, ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani,” alisema waziri mkuu.

HAKUNA KABURI LA FARU JOHN!!

Sakata hilo lilichukua sura mpya hivi karibuni baada ya wahifadhi wa eneo la Grumet kueleza kuwa, hakuna kaburi la marehemu huyo kwa kuwa hakuzikwa.

Walisema hayo baada ya waziri mkuu kutangaza kuunda timu kuchunguza mazingira ya kifo cha faru huyo huku akihoji mambo manne yaliyozua utata ambayo ni Faru John aliumwa lini?

Aliumwa nini? Daktari gani aliyemtibu?

Na zipo wapi taarifa za matibabu yake?

Pia Majaliwa aliagiza mwili wa faru huyo kufukuliwa na kutazama kama vinasaba vyake vinaendana na watoto wake 26 ambao bado wapo Ngorongoro.

Kwa mujibu wa mmoja wa wahifadhi aliyeomba kutotajwa jina, kitaalamu wanyama ambao wanakufa bila kuwa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya hifadhi hawazikwi.

Alisema baada ya faru huyo kufa aliondolewa pembe zake na yeye kutupwa ili awe  hakula cha wanyama wengine wanaotegemea mizoga, lakini mifupa yake ipo.

Alisema faru huyo aliombwa na Grumet kwenda kupanda faru waliopo katika eneo hilo baada ya dume aliyekuwapo kuuawa na tembo.

WASOMAJI WA RISASI JUMAMOSI

Baadhi ya wasomaji wa Risasi Jumamosi walipozungumza kuhusu sakata hilo walisema kuwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe ndiye mwenye majibu ya maswali yote kuhusu kifo cha faru huyo.

“Kama si Maghembe basi mtangulizi wake (Lazaro Nyarandu). Lakini kwa kuwa naamini serikali ya Rais John Magufuli si ya mchezomchezo, ikibainika uzembe ulikuwepo tangu wakati wa waziri aliyepita, basi ataulizwa tu hata ikibidi kuitwa na dola husika, hakuna udhuru kwamba hayuko madarakani,” alisema msomaji aliyejitambulisha kwa jina la Isaya Makidonto, mkazi wa Mabibo Farasi, Dar.

Naye mfanyakazi mmoja wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye aliomba hifadhi ya jina lake alisema homa inapanda na kushuka kwa vigogo wa wizara hiyo kwani, hakuna anayejua kesho yake.

“Unajua hii sinema ni ndefu, ina watu wengi ndani yake. Juzi imesemwa kwamba, hakuna kaburi la Faru John. Sasa kwa nini wale waliokwenda nyumbani kwa waziri mkuu kumpa taarifa, akiwemo Waziri Maghembe wasiseme? Inaonekana hata waziri mpaka wanafika kwa Majaliwa alikuwa hajui kama kuna kaburi au la! Kama alijua, basi aliamua kukausha.

“Na kama ni hivyo, sasa kazi ya waziri mwenye dhamana ni ipi? Maghembe alikwenda pale kama kivuli tu? Wale aliofuatana nao wanajua kila kitu kama anavyojua waziri wao.”

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili katika bunge lililopita, James Lembeli alisema kwa namna yoyote nyaraka atakazopewa Majaliwa zinapaswa kutoa majibu juu ya sababu za kuwepo kwa dalili za usiri wa jambo hilo.

“Nimeshangaa kusikia Faru John ninayemfahamu kwa muda mrefu ameondolewa (Ngorongoro) japokuwa siyo jambo geni ikiwa linafanyika kwa uwazi, inapokuwa siri ndiyo tatizo kwani inaibua harufu ya rushwa,” alisema Lembeli.

Akifafanua zaidi kiongozi huyo aliyeongoza vema kamati yake alisema kama taratibu za kuhamishwa zilifuatwa ni lazima kamati ya bunge inayohusika na maliasili ingekuwa na taarifa “… ni lazima kufuatilia kwa undani kwa nini ilifanyika hivyo,” alimaliza.

 

WATAKA NGOMA APEWE MAGUFULI

Baadhi ya wasomaji walitaka sakata la Faru John apewe Rais Magufuli ambaye yeye kulimaliza si suala la kumuumiza kichwa hata kidogo.

“Kwa mfano ikibainika Waziri Maghembe alizembea, Majaliwa sidhani kama anaweza kumuwajibisha. Mpaka mwenye nchi ambaye ni Magufuli. Si ndiye aliyemchagua! Lakini Magufuli naye kwa mambo kama haya yenye harufu ya ufisadi ndiyo anayachukia sana. Alishasema atapiga vita ufisadi. Hata Majaliwa alisema amenusa ufisadi kwenye ishu ya Faru John. Basi amwachie Magufuli amalizie mpira ambao yeye ameuanza.”

ILIKUPITA HII?

Mpaka Home; Haya Ndo’ Maisha Halisi ya Darassa, Cheki Video Akipika Msosi Gheto

Comments are closed.