The House of Favourite Newspapers

Hush: Tapeli Hatari Duniani, Matukio na Utajiri Wake Usipime!

0

 

JINA la Ray Hushpuppi ‘Hush’ limekuwa maarufu mno masikioni mwa wengi duniani. Likitajwa jina hili, baadhi ya mabilionea wanashtuka. Wanadhani muda si mrefu ‘wanapigwa’.

Kuna baadhi ya watu wanatamani kuwa kama huyu mwamba! Huyu jamaa amekuwa maarufu mno mitandaoni. Ana wafuasi zaidi ya milioni 2 pale Instagram.

 

Wafuasi wake wamekuwa wakijifunza mambo mbalimbali kwenye maisha yake kama; maisha ya kifahari anayoishi kwenye mijengo yake iliyonakshiwa kwa dhahabu, magari ya kifahari na ya bei mbaya kama Maybach Exelero, Ferrari, Rolls Royce, Aston Martin, Bentley Bentayga na ndege yake binafsi (private jet). Jamaa anakula bata la hatari la kuondoa stresi za maisha haya magumu hapa duniani.

Staili hii ya maisha, imemfanya kufuatiliwa na wengi hususan mastaa wakubwa duniani kama; Don Jazz (Nigeria), Mick Mill (Marekani) na wengine wengi na hata wa Kibongo. Je, uliwahi kujiuliza utajiri wake umetokana na nini na kwa nini anakula bata hadi kuku wananuna?

 

Gazeti la IJUMAA limechimba mengi usiyoyajua kuhusu jamaa huyu ambaye anatajwa kuwa ni tapeli wa kimataifa (international scamer) anayeshikiliwa na FBI pale Marekani kwa utapeli wa kutisha sehemu mbalimbali duniani;

HUSHPUPPI NI NANI?

Raymond Olorunwa Abbass, ndilo jina alilopewa na wazazi wake, lakini jina la kutafutia ugali mjini (utapeli) ni Hushpuppi.

Huyu mwamba ni mzaliwa wa pale Lagos nchini Nigeria, lakini makazi yake ya kifahari yapo kule Dubai kwenye Falme za Kiarabu.

 

UTAJIRI WAKE

Hushpuppi anatajwa kuwa na utajiri wa zaidi ya shilingi trilioni moja.

Mbali na magari yake ya kifahari 13 ambayo amekuwa akiyabadilisha kuendana na mavazi yake ya Cucci, anamiliki mali zisizohamishika kama; mijengo ya kifahari, ofisi na ‘apartments’ anazopangisha sehemu mbalimbali duniani.

Kutokana na utajiri wake kuwa gumzo, ndipo akaanza kuhusishwa na utapeli wa kudukua barua pepe za makampuni makubwa duniani, kubadili namna ya utumaji wa pesa (hacking) na kuiba taarifa mbalimbali za kibenki Afrika na duniani kwa ujumla. Yaani kama unamtumia mtu shilingi milioni 10 za Kibongo, basi zote zinakwenda kwenye akaunti yake.

Kutokana na sababu hizo, ndipo Shirika la Operation Pex Hunt 202 likaingia kazini na kuanza kumchunguza.

KUKAMATWA KWAKE

Za mwizi ni arobaini! Ndivyo msemo wa Kiswahili usemavyo, kwani Juni 10, mwaka huu, jamaa alikamatwa.

 

Alipokamatwa, alikutwa na nyaraka za kugushi, fedha zaidi ya shilingi bilioni 94.7 zilikutwa ndani kwake Dubai. Pia alikutwa na kompyuta 21, simu 47, flashi 15, hard disk 5 zenye mafaili 119,580 za watu na kampuni zilizoibiwa.

 

Pia kulikuwa na dokumenti za utapeli wa Dola za Kimarekani milioni 35 zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa mashine za kupumulia (ventilators) zilizohitajika nchini kwao Nigeria kukabiliana na janga la Corona. Hivyo Hushpuppi na wenzake 11, walitiwa mbaroni.

 

MAONI YA WATU

Kutokana na kukutwa na tuhuma hizo, wapo wanaoona kama anaonewa na wengine wanasema ni haki yake kwani amekuwa akisakwa kwa muda mrefu na Polisi nchini Nigeria kwa tuhuma hizohizo za utapeli. Ujanja aliokuwa akiufanya ni kutokufanya uhalifu mahali alipokuwa akiishi, yaani Dubai.

 

USHAURI WA BURE

Si kila staa tunayemuona mitandaoni anakula bata, basi tuige maisha yake, kwani kuna wengine wanatumia njia zisizo halali na kujipatia utajiri mkubwa. Chamsingi ni kuiga yale yaliyo mema na mabaya tuwaachie wenyewe, kama ilivyo kwa Hushpuppi.

MAKALA: AMINA SAID, BONGO

Leave A Reply