The House of Favourite Newspapers

Huyu Naye..! Fuata Maelekezo 19

0

ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:
Nilimtazama baba Rehema kisha nikashusha pumzi kwa nguvu na kumuweka sawasawa kwa mchezo unaofuata…
“Baba…baba…babaa,” sauti ya Rehema iliita kutokea sebuleni kuja chumbani…

TAMBAA NAYO MWENYEWE SASA…
Baba alivaa akatoka mbio huku akiuliza…
“Kuna nini Rehema?”
“Geti linagongwa kwa nguvu sijui nani?”
Na mimi nilikuwa nyuma ya baba Rehema. Kweli geti lilikuwa likigongwa kwa nguvu sana bila mgongaji kusema lolote.
“Wewe nani?” aliuliza baba Rehema kwa sauti iliyojaa uzito wa uanaume…
“Ngo ngo ngo,” geti liliendelea kugongwa licha ya kuulizwa ni nani!
“Nakuuliza wewe nani hujibu siyo? Unanijua unanisikia?” alisema baba Rehema…
“Ngo ngo ngo,” mgongaji aliendelea kugonga bila kujali tahadhari ya kuulizwa.

Baba Rehema alirudi chumbani, akachukua bastola na kutoka tena mpaka getini…
“Nakuuliza tena wewe ni nani? Usipojitambulisha nikifungua geti nitakachokufanyia utajuta kuzaliwa binadamu.”
“Ngo ngo ngooo…”
Nilimwona baba Rehema akiachia tabasamu la hasira kisha akafungua geti…
“Nimemfuata mwanangu na wala sitaki ugomvi na mtu,” alikuwa ni mama Rehema akisema maneno hayo huku amesimama katikati ya geti.

Wakati huo, Rehema mwenyewe alisimama nyuma yangu akiwa amejing’ata kidole akisikiliza.
Nilijua baba Rehema atawaka lakini alichofanya ni kuwa mpole akasema…
“Katika maisha yangu sijawahi kufikiria kama kuna uwezekano wa kugombea mtoto. Tumuulize mwenyewe kama yupo tayari kuondoka na wewe ruksa, kama anataka kubaki na mimi pia ruksa.”
Mimi nikadakia…

“Eti Rehema unakwenda na mama au unabaki hapa?”
“We koma! Unamuuliza wewe kama nani?” mama Rehema alinijia juu huku midomo yake ikitetemeka…
“Nataka kubaki na baba na mama wewe,” alijibu Rehema huku akimwangalia mama yake kwa macho mang’avu kabisa…
“We’ nitakuachia laana Rehema…kavae tuondoke…huyo unayesema mama yako wa hapa mbona ni malaya tu,” alipayuka mama Rehema…

“Mimi sitaki mama nabaki na baba hapahapa nyumbani.”
Nilimwona mama Rehema akiingia kwa nguvu na kumshika mkono Rehema akazama naye ndani kabisa mpaka chumbani kwa mtoto huyo…
“Jamila kuwa mpole,” baba Rehema aliniambia huku akinishika mkono na kunikalisha kwenye kochi kubwa na yeye akakaa hapo pembeni yangu.

Nilijisikia nina amani sana kwa baba Rehema kuwa upande wangu na kumwonesha dharau mke wake.
Mara, mama Rehema alitoka akiwa amemshika mkono Rehema huku mkono mwingine ameshika begi la nguo.
Rehema alikuwa akilia kwa sauti ya juu…
“Babaa…babaa…mimi sitaki kwenda na mama.”
Nilijikuta nikiingiwa na uchungu. Uhuru unatakiwa sana, mtoto awe na amani ya kuishi popote anapotaka yeye. Sasa kama vile hata huko anakokwenda amani itatoka wapi? Nilijiuliza mwenyewe nikasimama aisee…

“Huyu mtoto huendi naye mama Rehema, kama ni kupigwa zipigwe mimi na wewe,” nilisema kwa sauti iliyojaa hasira huku nikienda kumshika mkono Rehema…
“Weee…weee! Weeeee! Jaribu kumgusa mwanangu uone jinsi uchungu wa mwana anavyoujua mzazi,” mama Rehema alinichimba mkwara, sikujali wala kumwogopa nikamshika Rehema na kumvutia kwangu…
“We Jamila unanitafuta, sasa nakuua,” alisema mama Rehema.

Rehema alipopata upenyo wa kutoka kwenye mikono ya mama yake alikimbilia kwenye miguu ya baba yake huku akiendelea kulia…
“Jaribu uone nitakachokufanyia, mbwa wewe,” nilimpasha mama Rehema nikimwangalia kwa macho makavu yaliyosheheni shari na uadui mkubwa. Nilikunja ngumi na kusimama katika pozi la kumsubiri aje sasa anivae aone…
“Unadhani ulivyokuwa unanionea siku zote ndiyo mpaka na sasa, njoo,” nilimwambia.
Nilimwona akiondoka na begi la nguo za mtoto huku akitukana kila aina ya tusi alilobahatika kulijua hapa duniani.
Niliongozana naye kwa ujasiri mpaka getini huku nikimwambia…

“Matusi hayaniumizi kichwa mimi, wewe njoo uniue uone kitakachokupata.”
Alipovuka geti akiwa nje jirani na Bajaj, kumbe alikuja na Bajaj alisema…

“We Jamila kama sitakuua kwa tindikali nitakuua kwa uchawi hilo litambue kuanzia sasa…”
“Na mimi kama sitakuua kwa kukuchoma kisu nitakuua kwa kukukaba kabali, lifahamu hilo kuanzia sekunde hii,” na mimi nilimwambia kwa sauti ya kumfokea mpaka majirani wakatushangaa mtu na bosi wake kulikoni.
Nilipogeuza tu nikakutana na baba Rehema akiwa ananifuata…
“Vipi baby? Anakusumbua eee?”
“Anisumbue wapi huyu! Eti ataniua kwa uchawi au…”
Ile sijamaliza kusema nikashtukia amenimwagia maji usoni, nikasikia maumivu makali sana, nikaanza kupiga kelele nikienda chini…
Je, unajua nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi ijayo.

Leave A Reply