The House of Favourite Newspapers

Ibrahim Ajibu alivyoweka rekodi Taifa

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu ameweka rekodi mpya Uwanja wa Taifa katika mchezo waliocheza juzi dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga akiwa amevaa kwa mara ya kwanza kitambaa cha unahodha. Mchezaji huyo alichukua cheo hicho cha unahodha kwa Kelvin Yondani aliyeporwa na kocha kutokana kwenda kinyume na maelekezo yake.

 

Ajibu ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba, alifunga bao la kwanza akiwa nahodha kwenye mchezo wake wa kwanza mzunguko wa pili akiwa umbali wa mita 35 kwa kupiga mpira wa faulo uliompoteza mbali mlinda mlango wa Mwadui FC, Anold Masawe.

 

Dakika ya 18 Ajibu aliweka rekodi kwa kukosa penalti yake ya kwanza mzunguko wa pili baada ya mchezaji Amissi Tambwe kuchezewa rafu eneo la hatari na penalti hiyo ilipigwa na Ajibu ikaokolewa na Masawe.

 

Dakika ya 39 Ajibu alilipa kisasi baada ya kutengeneza pasi ya bao lililofungwa na Tambwe, akafanya hivyo pia kipindi cha pili dakika ya 58 kwa kumpa pasi Fei Salum ‘Fei Toto’ ambaye alimaliza kwa kuachia shuti la mbali lililomshinda Masawe.

 

Mchezo wake wa kwanza Ajibu akiwa na cheo, anatengeneza pasi mbili za mabao na kufunga bao moja huku akikosa bao moja, rekodi ambayo bado haijawekwa na nahodha yoyote wa Bongo kwa mzunguko wa pili pamoja na ule wa kwanza ambao kuna timu bado hazijaumaliza ikiwa ni pamoja na Yanga wenyewe.

LUNYAMADZO MLYUKA Dar es Salaam

Comments are closed.