IJUE SIRI YA MASTAA HAWA BONGO KUTOBOA KIMATAIIFA

YAWEZEKANA kabisa wewe ni msanii chipukizi au msanii mkubwa Bongo unayetamani siku moja uweze kutambulika kimataifa, lakini hujui wapi pa kuanzia wala kuishia, tulia kwanza!  

 

Kwa zaidi ya miaka 25, muziki wa Bongo Fleva umekuwa ukitikisa Bongo, lakini ni mastaa wachache ambao wamepenya nje ya nchi. Mwanzoni mwa miaka ya 2000, msanii kama AY aliweza kufanya kolabo la kimataifa na Amani wa Kenya huku Prof Jay akifanya na Chameleone wa Uganda na Lady Jaydee akifanya na Kidumu na Juliana Kanyomozi kutoka Uganda.

Ukiachana na hicho kizazi, kizazi cha sasa, wapo wasanii wachache wanaoonesha kupasua kimataifa, lakini kolabo zao nyingi zinaishia Nigeria na Afrika Kusini, mfano Vee Money na K.O, Harmonize na Korede Bello au Joh Makini na Chidinma wa Nigeria. Muziki wa Bongo Fleva unaweza kuufikisha mbali, unaweza kufanya muziki huo kwenye lebo kubwa za kimataifa ikiwemo Sony Music hata kama ni msanii chipukizi.

Showbiz limekuandalia siri ya mastaa kutoboa kimataifa akiwemo Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye ana mkataba na Kampuni ya Universal Music Group (UMG) iliyomkutanisha na Ne-Yo wakati Alikiba akiwa na Sony Music. Sony Music ni moja ya kampuni kubwa duniani zinazosimamia muziki ikiwa na makazi yake nchini Marekani. Kampuni hii ina ‘connection’ kubwa ya wasanii katika mabara yote na mara kwa mara huwa wanapokea wasanii wengi bila kujali ni chipukizi au ana kajina f’lani.

 

Sony Music ipoje?

Unapoambiwa Sony Music jua kwamba ndani yake kuna makampuni makubwa wanayoyasimamia kama vile Sony Music (Uingereza), Columbia Records, ROC Nation, Epic Records, RCA Records, Arista Records, Sony Music Latin, Ariola Records, Flying Buddha pamoja na RCA Inspiration (hii ni kwa waimba Injili).

 

Sony Music ilianza na wasanii tofauti ambao leo hii ni mastaa wakubwa duniani, ilianza na Kundi la Backstreet Boys, marehemu B.I.G (Notorious), Jennifer Lopez na mfalme wa Pop, marehemu Michael Jackson.

Wasanii wake wengine wanapatikana Amerika ya Kusini, Ulaya, Asia, Australia na Afrika sanasana nchini Nigeria ndiyo wapo wengi kama vile Wizkid, YCee, Davido, D’Banj, Tekno na Tiwa Savage. Wengine ni Beyonce, Chris Brown, Britney Spears, Drake na Mariah Carey kutoka Marekani, AKA kutoka Afrika Kusini, Adele na Robbie Williams kutoka Uingereza, Cindi Yen wa Taiwan na Brian Joo wa Korea.

 

Jinsi ya kujiunga na Sony

Ingawa wasanii wengine walitengenezwa kabla ya kuingia Sony Music, lakini inawezekana hata kwa wewe ambaye hajatengenezwa. Kama wewe ni msanii chipukizi au msanii ambaye unayejulikana, lakini hujajua njia ya kutoboa kimataifa, kupitia Sony Music makala haya yatakusaidia kwa kiasi kikubwa.

ZINGATIA HAYA

Tengeneza muziki mzuri

Kwa kujali kipaji chako, ingia kwenye studio zenye kutoa muziki bora ambapo utatengeneza kazi ya mfano (demo) ambayo itakusaidia kuandaa kazi bora baadaye. Kwa hiyo kama bado hujatoa kibao chochote, tuliza akili yako, tunga nyimbo kadhaa kisha chagua ulio bora zaidi halafu nenda studio.

Tangaza nyimbo zako

Ulimwengu wa sasa upo kidijitali sana, tunaishi dunia ya kijiji kimoja. Njia iliyo bora ya kutangaza nyimbo zako ni kutumia mitandao ya kisasa ambayo ni bora katika kukutangazia kazi zako za muziki duniani.

 

Baadhi ya mitandao hiyo ni SoundCloud, iTunes, Spotify, YouTube na mingine mingi. Kumbuka kuna ambayo itakutoka chapaa kidogo sana hivyo usiwaze! Pia unaweza kushea ngoma zako kwa marafiki, familia, mitandao ya kijamii, radio na TV na lengo la hapa ni kujitengenezea kwanza mashabiki wakujue.

Njia nyingine simpo ya kujitengenezea mashabiki ni kuwa na akaunti, Twitter,  Instagram, YouTube, Facebook na kwingineko. Hudhuria semina mbalimbali za kimuziki pamoja na matamasha makubwa na madogo, jipenyeze tu! Tengeneza video yenye ubora hata kama ni kwa gharama lakini ukiwa na moja au mbili itakusaidia sana mbeleni niamini mimi.

 

Wasiliana nao sasa

Baada ya kuzingatia hayo, Sony Music ambayo ni kampuni kubwa kama nilivyokueleza hapo juu, hupokea barua pepe nyingi kwa siku, mfano wa kazi za wasanii (demo), simu, meseji na wengine hufika ofisini kwao kujaribu bahati yao, japo si ngumu sana kutoboa kuna asilimia kubwa kama umefuata vigezo hivyo nilivyokupa.Kwa kuituma kazi yako (demo), tembelea tovuti yao au tawi lao la Sony Music unalolifahamu karibu nawe.

Unaweza pia kuwasiliana na meneja wa Sony Music kupitia vipaji (A&R), John Doelp (e.mail- doelp@ sonymusic.com) kisha ambatanisha na demo yako. Kumbuka, usitume nyimbo za kundi bali ya wewe kama wewe na utajibiwa.

Mwandishi wa makala haya, ni mwandishi wa burudani anayeandikia Magazeti Pendwa ya Global Publishers. Unaweza wasiliana naye kwa; +255 713 133 633

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment