The House of Favourite Newspapers

Imefichuka… Aslay, Mbosso Tifu Zito!

0

DAR: Kama ulikuwa unatarajia kolabo kati ya mafahali wengine wawili wa Bongo Fleva; Aslay Isihaka Nassoro na Mbwana Yusuph Kilungi ‘Mbosso Khan’, sahau jambo hilo kwa sasa, IJUMAA linafichua siri.

 

NI ZAO LA YAMOTO

Aslay na Mbosso ni miongoni mwa wasanii wakali waliokuwa wakiunda Kundi la Yamoto Band ambalo lilikuwa gumzo ndani na nje ya Bongo kabla ya kuvunjika yapata miaka mitano iliyopita na sasa kila mmoja anapambana kivyake.

Wengine waliokuwa nao Yamoto Band ni Beka Flavour na Enock Bella chini ya Said Fela ‘Mkubwa na Wanawe’.

 

TIFU TANGU KUSAMBARATIKA

Gazeti la IJUMAA linafahamu kwamba, jamaa hao wapo kwenye mtifuano mzito kwa muda mrefu tangu waliposambaratika.

Mara baada ya kusambaratika, Aslay ndiye aliyekuwa wa kwanza kuachia nyimbo zake binafsi ambapo Mbosso aliamua kurejea kijijini kwao mkoani Pwani.

 

Kufuatia Aslay kuachia nyimbo mfululizo, baadaye yalisikika madai kutoka kwa wenzake hao kuwa, yeye (Aslay) ndiye chanzo cha kuvunjika kwa Yamoto Band, madai ambayo huwa hataki kuyajibu.

 

MBOSSO WASAFI, ASLAY AMPOTEZEA

Ilidaiwa kuwa, kabla ya kujiunga na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Mbosso alikuwa akilalamika kuwa kila alipompigia simu Aslay alikuwa akimpotezea.

 

Lakini baada ya Mbosso kuchukuliwa na Wasafi, ndipo hali ilipozidi kuwa mbaya juu ya uhusiano wao na sasa hata simu wakawa hawapigiani.

 

WIVU WATAJWA

Mara tu baada ya Mbosso kusainiwa na Wasafi, kumekuwa na tetesi za kuoneana wivu na kufikia hatua ya kushindanishwa wenyewe kwa wenyewe.

 

Kuhusu kushindanishwa, Mbosso aliliambia Gazeti la IJUMAA kuwa; “Mimi ninauheshimu muziki wa Aslay kwa sababu ni mtu ambaye nimemkuta kwenye industry, halafu kwangu mimi yule ni brother.”

Hata hivyo, mashabiki wao wamekuwa wakitofautiana, huku kila upande ukiamini msanii wake ni mkali kuliko mwingine.

 

KUJIMWAMBAFAI

Katika hali kama hiyo, hata wao wenyewe (Aslay na Mbosso), kila mmoja anadaiwa kujimwambafai na kujiona yupo juu kuliko mwenzake.

 

“Wale hawawezi kuelewana kwa sababu kila mmoja anajiona yupo juu kuliko mwenzake.

“Siyo vibaya mtu kujiamini sana, ushindani unaleta chachu kwenye gemu la Bongo Fleva.

“Mimi sioni kama mabifu yana ubaya kama lengo ni kushindana kimuziki, lakini wasijengeane chuki,” alisema mwigizaji wa Bongo Movies ambaye pia anafanya Bongo Fleva, Laurent Ngubilu.

 

Katika kuonesha kuwa bado hadi sasa hali si shwari, Mbosso aliliambia Gazeti la Ijumaa;

“Nilimsapoti sana (Aslay) kwa muda mrefu, lakini nilionekana ninajipendekeza,” alisema Mbosso alipoulizwa na gazeti hili juu ya uhusiano wake na Aslay na kuongeza;

“Baada ya kumsapoti Aslay kwa muda mrefu, watu wakawa wananiambia mbona wewe unamsapoti halafu yeye hakusapoti?

 

“Mtu umem-follow (kwenye Instagram), mwenzako ameku-unfollow. Jifunze kubalansi shobo, nikasema kumbe na mimi naonekana namshobokea… ngoja na mimi nim-unfollow.

“Kwa hiyo nisiwe mnafiki, kwa sasa hivi kila mtu hana urafiki na mwenzake.”

 

HUYU HAPA ASLAY

Kwa upande wake Aslay alipoulizwa na IJUMAA hivi karibuni juu ya uhusiano wake na Mbosso alikuwa na haya ya kusema;

“Kuna matatizo ambayo siwezi kuongea kwani mwisho wa siku kila kitu kinaendea freshi, tusiendelee tena kuleta kitu kingine.”

Alipoulizwa kama ana mpango wa kufanya kolabo na Mbosso, Aslay alisema hana la kusema.

 

BEKA VITA NA ASLAY

Ukimwacha Mbosso, msanii wa Yamoto, Beka Flavour naye anatajwa kutoivana na Aslay.

Katika maelezo yake, Beka alikanusha maelezo kuwa anamwogopa Aslay kutokana na kipaji chake kikubwa.

 

“Hakuna kitu kama hicho, wale wenye fikra kuwa ninamuogopa waendelee kufikiria hivyo, muziki wangu sija-focus kwake, nime-focus kwa watu wakubwa wengine,” alisema Beka akieleza uhusiano wake na Aslay.

 

MABIFU YA BONGO FLEVA

Kwenye Bongo Fleva kumekuwa na mabifu tangu enzi za Gangwe Mobb na TMK Wanaume, Jide na MwanaFA, Joh Makini na Fid Q, Diamond na Dimpoz, Diamond na Kiba, Diamond na Harmonize na mengine kibao. Hivyo, wanachokifanya Aslay na Mbosso siyo kitu kipya.

Stori: Neema Adrian, Ijumaa

Leave A Reply