The House of Favourite Newspapers

Insane (Mwendawazimu)-09

ILIPOISHIA

Boniface akashtuka, hakutaka kubaki ndani ya ofisi yake, akateremka kwenye ngazi harakaharaka, alipofika chini, akaingia ndani ya gari lake na kuliondoa mahali hapo. Aliwaona watu hao kwa mbali lakini hakuweza kuwapata kwani kulikuwa na foleni kubwa ya magari, akajikuta akikwamishwa na magari hayo. Pikipiki hiyo ilipofika maeneo ya Stesheni, ikakata kulia na kutokomea huko kuelekea Mnazi Mmoja.

SONGA NAYO..

Boniface alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokiona kwamba mtoto wake, aliyemzaa kwa damu yake, alikuwa amechukuliwa na watu wasiojulikana na kuondoka naye. Moyo wake ulimuuma mno, alirudi ofisini huku akibubujikwa na machozi.

Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makubwa, ofisini, hakutulia, alichokifanya ni kuwapigia simu polisi na kuwaambia kilichokuwa kimetokea, polisi hao wakaahidi kufika mahali hapo ndani ya dakika tano tu.

Akabaki ofisini pale, alisimama dirishani huku akiangalia chini, zaidi ya watu kumi walikuwa wamemzunguka Miriam ambaye alikuwa akihuzunika tu, hakulia lakini kwa jinsi alivyoonekana, ilikuwa rahisi kugundua kwamba alikuwa na maumivu moyoni mwake.

Hakuwa na akili lakini hilo halikumfanya kutokuumia. Alimpenda mtoto wake kwa sababu ndiye aliyemfanya kuwa na furaha, ndiye aliyekuwa akizunguka naye huku na kule, ghafla, watu wenye roho mbaya wakamuiba mtoto wake kitu kilichomuumiza kupita kawaida.

Baada ya dakika tano, polisi wakafika mahali hapo, harakaharaka akateremka kutoka ghorofani na kwenda chini, akatoa maelezo yake juu ya kile alichokiona, polisi wakachukua maelezo yake kisha kuwataka watu wengine kuelezea kilichotokea.

Maelezo yalifanana, wakachukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi ambapo huko wakaanza kuelezea kwa kina kilichokuwa kimetokea. Moyo wa Boniface bado ulikuwa na huzuni mno kama mtu aliyefiwa, mbali na polisi hao kuwaambia kwamba wangefanya upelelezi kuhakikisha mtoto anapatikana, lakini naye akataka kufanya upelelezi wake mpaka atakapofanikiwa kumpata mtoto wake.

Huo ndiyo ulikuwa muda wa kuhuzunika kupita kawaida. Hakuwa na furaha, muda mwingi alikuwa na huzuni kupita kawaida. Nyumbani hakutaka kukaa kabisa, muda mwingi alikuwa akishinda baa.

Msichana wake, Jesca alipokuwa akimtafuta kwenye simu, alipoiona namba hiyo akawa anakata simu. Hakuwa sawa, akili yake ilivurugwa kwani alikuwa na hamu sana ya kuwa na mtoto, tena amlee kwa mikono yake lakini mwisho wa siku mtoto akaibwa.

Hali yake aliyokuwa nayo zamani ikarudi tena, Jesca aligundua kwamba mpenzi wake hakuwa sawa. Kila siku akawa anamuuliza tatizo lililokuwa likimsibu lakini hakutaka kumwambia ukweli zaidi ya kumdanganya kwamba kila kitu kilikuwa poa.

Jesca hakuishia kumuuliza, kwa sababu alijua kwamba kulikuwa na kitu hakijakaa sawa, akaanza kumpeleleza chini kwa chini ili ajue kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Alijitahidi kufanya upelelezi wake lakini majibu yalikuwa yaleyale kwamba hakukuwa na msichana yeyote yule.

“Ila tatizo nini mpenzi?” aliuliza Jesca.

“Naomba uniache kwanza. Nimevurugwa Jesca!” alimwambia mpenzi wake.

“Mpenzi! Haiwezekani! Niambie tatizo nini! Mbona kila kitu unakifanya kivyakovykao. Mimi na wewe tutafunga ndoa, tatizo lako ni langu pia, unapokuwa na tatizo, natakiwa kujua mpenzi,” alisema Jesca huku akimsogelea mpenzi wake huyo aliyekuwa kwenye kiti, alikiegemeza kichwa chake, kichwa akakiinua juu.

“Naomba uniambie tatizo nini!”

“Nimesema niacheeee…” alisema Boniface kwa sauti ya juu kabisa mpaka Jesca akaogopa.

Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea kwa mpenzi wake, moyo wake ulimuuma mno kwani hakutamani kumuona mwanaume huyo akiwa kwenye hali hiyo, alipenda kumuona akiwa na furaha katika maisha yake yote.

Alichokifanya ni kuondoka na kurudi nyumbani, njiani alikuwa na mawazo tele, hakutaka kuvumilia, hakutaka kuona akiumia zaidi, alichokifanya ni kuwaambia wazazi wake, wenyewe walishangaa kwani kesi kama hiyo ilikwishawahi kuletwa kabla.

“Hujagundua ni kitu gani kinamsumbua?” aliuliza baba yake.

“Hapana! Nimejitahidi sana kumfuatilia lakini sijagundua kitu chochote kile,” alisema Jesca.

“Haiwezekani! Ngoja nizungumze naye.”
“Baba…”

“Wewe acha nikazungumze naye. Unajua wakati mwingine sisi wanaume tunakuwa na matatizo ambayo hatutaki wanawake zetu wajue, kwa hiyo usijali Jesca,” alisema baba yake maneno ambayo kidogo yalimpa moyo msichana huyo.

****

“Ile kazi imefanyika?” alisikika akiuliza Edson.

“Imefanyika. Mtoto tupo naye na tunakuja naye huko,” alisikika kijana mmoja.

“Safi sana. Njooni naye.”
“Hakuna shida.”
Mpango uliokuwa umefanywa haukuwa wao peke yao bali walimshirikisha madaktari wawili ambao ndiyo waliotakiwa kuwafanya watu wote wajue kwamba mke wa Edson alikuwa amejifungua.

Hilo halikuwa tatizo, mpango huo ukafanyika kikamilifu na ndani ya dakika kadhaa, watu hao wakafika hospitalini hapo ambapo wakapitia katika milango ya dharura waliyokuwa wameelekezwa mpaka ndani ya chumba hicho.

Mtoto akawekwa katika sehemu husika, na Edson alipoambiwa kwamba mtoto tayari alikuwa ndani ya chumba hicho, akaingia na kwenda kumuona. Alikuwa mtoto mzuri wa kiume, moyo wake ukatokea kumpenda, kwa jinsi alivyokuwa akilia, moyo wake ukampa uhakika kwamba mtoto huyo alikuwa mzima kabisa.

“Mtoto wangu ataitwa Fabian,” alisema Edson huku akikenua kana kwamba mtoto aliyekuwa akimwangalia alikuwa wake.

Kwa kuwa Rachel hakuwa na tatizo lolote lile, siku hiyo akaruhusiwa kuondoka na kurudi nyumbani. Huko, marafiki na ndugu wakaanza kumpongeza kwa kazi kubwa aliyokuwa ameifanya.

Hakukuwa na mtu aliyelifahamu hilo, kila mtu akajua kwamba huyo mtoto alizaliwa na Rachel. Baada ya siku tatu, walichokifanya ni kumfanyia sherehe mtoto huyo, japokuwa moyo wa Rachel ulimuuma lakini hakuwa na jinsi, alijua kwamba mumewe aliamua kufanya vile kwa sababu tu walihitaji furaha na kuficha aibu kubwa.

“Huyu ndiye atakuwa mrithi wetu,” alisema Edson huku akimwangalia mkewe.

“Nimefurahi! Sitotaka kusingizia tena. Bora tuwe na mtoto huyuhuyu mpenzi,” alisema Rachel huku akimwangalia mtoto wake.

“Haina shida. Cha msingi ni kumpa malezi bora, huyu ndiye bilionea wetu wa baadaye,” alisema Edson huku akichia tabasamu pana. Kwa jinsi alivyokuwa na furaha, ilikuwa vigumu sana kugundua kwamba mtoto yule hakuwa wake.

****

Alichokifanya baba Jesca ni kumtafuta Boniface na kuzungumza naye, mwanaume huyo, kwa kumwangalia tu alionekana kuwa na majonzi tele, hakuwa sawa na muda mwingi alionekana kuwa na mawazo mno.

Mzee huyo alipomuona tu, akagundua kwamba kulikuwa na tatizo kubwa lililokuwa likiendelea, alitaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kimemsibu mkwe wake mtarajiwa mpaka kuwa kwenye hali hiyo.

Alijaribu kuzungumza naye lakini Boniface akamwambia kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile na kila kitu kilikuwa kama kawaida. Mzee huyo hakutaka kukubali, alipomwangalia mwanaume huyo, aliamini kwamba alikuwa na tatizo, alitaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake ili kama kungekuwa na uwezekano wa kumsaidia, basi amsaidie.

“Hakuna tatizo baba,” alisema Boniface.

“Una uhakika?”
“Ndiyo! Hakuna tatizo baba. Wakati mwingine nakuwa na mawazo na mambo yangu, ila kiukweli ni kwamba sina tatizo kabisa,” alisema Boniface huku akimwangalia mwanaume huyo aliyekuwa mbele yake.

Kile kilichokuwa kikiendelea kilikuwa siri kubwa, hakutaka mtu mwingine ajue na ndiyo maana kila kitu kikabaki moyoni mwake. Mzee huyo akaondoka na kupeleka taarifa kwamba Boniface hakuwa na tatizo lolote lile kwani alitumia dakika nyingi kuzungumza naye lakini msimamo wake ulikuwa uleule kwamba hakukuwa na kitu chochote kibaya.

Uhusiano uliendelea kama kawaida japokuwa Boniface hakuonekana kuwa na furaha. Kichwa chake kilikuwa kikimuuma na wakati mwingine alivyokuwa akimwangalia Miriam Mwendawazimu, alivyokuwa na huzuni, moyo wake ulimuuma mno.

Mara kwa mara alikuwa akiwasiliana na polisi kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Polisi hao hawakujua kitu chochote, hawakujua ni nani aliyekuwa amemuiba mtoto huyo.

Upelelezi ulikuwa ukifanyika lakini hawakuweza kumpata mtu huyo kitu kilichowachanganya hata polisi wenyewe. Upelelezi ulifanyika kwa mwaka mzima lakini hakukuwa na dalili za kumpata muhusika kitu kilichowaweka polisi hao katika wakati mgumu.

Boniface hakutaka kuishia hapo, kwa sababu yeye ndiye aliyempa mwendawazimu mimba hiyo, akaamua kumtafuta mtoto mwingine na msichana huyo. Hakutumia nguvu kubwa, Miriam alimfahamu mwanaume huyo na hata alipokuwa akimfuata na kumchukua nyakati za usiku, aliondoka naye na kwenda kufanya naye mapenzi na kisha kumrudisha.

“Ni lazima nimzalishe tena,” alisema Boniface huku akimaanisha alichokisema.

Hilo halikuwa tatizo, baada ya mwezi mmoja wa kufanya mapenzi na mwendawazimu huyo, akamuona mwanamke huyo akianza kubadilika na kuonyesha dalili zote kwamba alikuwa mjauzito.

Muda huo alikuwa makini, alikuwa akimfuatilia kwa karibu sana. Baada ya miezi mitatu, tumbo likaanza kuonekana vizuri kabisa. Kila mtu alishangaa, hawakujua mwanaume aliyekuwa akimfanyia mchezo huyo kichaa huyo.

Alichokifanya ni kuwatumia madaktari kumchukua na kumpeka hospitalini, awe chini ya uangalizi wao mpaka pale ambapo angejifungua mtoto huyo. Hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu alikuwa na fedha nyingi, alijitahidi kutumia kwa ajili ya kuhakikisha mwanamke huyo anajifungua salama.

“Nitatumia mpaka senti yangu ya mwisho,” alimwambia daktari.

“Najua. Nilisikia taarifa zile mbaya. Pole sana,” alisema Dk. Fabian.

“Asante sana.”

Baada ya miezi sita na kutimiza miezi tisa, Miriam akajifungua mtoto mwingine wa kiume. Hiyo ilikuwa furaha kwa Boniface na kwa sababu Dk. Fabian alikuwa amemsaidia katika kila hali, akaamua kumpa jina lake na kuitwa Fabian kama ukumbusho wa kile alichokuwa amekifanya.

Boniface hakutaka kumruhusu Miriam aondoke hospitalini hapo, alichokifanya ni kulipia fedha zaidi ili mwanamke huyo aendelee kuwa na mtoto wake hospitalini hapo. Siku zikakatika na mtoto alipofikisha mwaka mmoja huku mwanamke huyo akiwa kwenye kituo cha watoto, Boniface akaanza kumchukua na kwenda naye nyumbani kwake.

Hakutaka kuona Jesca akifahamu chochote kile, alichokifanya ni kumwambia ndugu yake, Rose aende kuishi hapo nyumbani huku akijifanye mtoto yule ni wake. Hilo likafanikiwa, Rose ambaye alikuwa akijulikana na Jesca kama dada wa Boniface akaanza kuishi hapo huku akimlea mtoto Fabian.

“Mtoto wako mzuri wifi,” alisema Jesca pasipo kujua juu ya mtoto yule.

“Nashukuru sana wifi. Namshukuru Mungu kwa baraka zake,” alisema Rose.

Hiyo ilikuwa siri, mtoto Fabian akaendelea kukua huku mara kwa mara Boniface akimchukua na kwenda hospitalini kwa ajili ya kumuonyeshea Miriam mtoto wake. Siku zikakatika mpaka unaingia mwaka wa tatu ambapo Fabian akaanza kusoma katika shule ya chekechea iliyokuwa Mikocheni.

Katika kipindi hicho, Boniface alikuwa kwenye wakati mgumu zaidi kwani Rose hakutakiwa kuondoka nyumbani hapo na wakati Jesca wakati mwingine alimwambia mpenzi wake kwamba huo ulikuwa muda wa msichana huyo kuondoka ili yeye ahamie nyumbani hapo.

“Haiwezekani! Siwezi kumfukuza dada yangu!” alisema Boniface.

“Lakini…”
“Jesca. Ninampenda sana Rose. Ni dada yangu aliyeachwa akiwa mjauzito. Kichwa chake kimechanganyikiwa, iweje nimuache? Nilihangaika kwa ajili ya kupata fedha kwa ajili ya ndugu zangu, nimezipata, naanzaje kumfukuza?” aliuliza Boniface.

Hakutaka kuona dada yake akiondoka nyumbani hapo. Jesca hakutaka kuridhika, kila siku alikasirika, hakukubaliana na hilo lakini Boniface hakutaka kumuona dada yake akiondoka nyumbani hapo.

Fabian aliendelea kukua, shuleni alipokuwa akisoma, alikuwa tofauti, alikuwa mkimya lakini mwenye uwezo mkubwa darasani. Akawa mwanafunzi wa kwanza kujua kusoma, alikuwa na umri mdogo lakini kwa uwezo aliokuwa nao uliwafanya hata walimu kumshangaa.

Ilikuwa ni furaha kwa Boniface, mtoto alivyoendelea kukua ndivyuo ambavyo sura yake ilipoanza kufanana na baba yake hivyo alichokifanya ni kuzungumza na Rose na kumwambia aondoke nyumbani hapo kwa kumpangia nyumba nzima iliyokuwa Kijitonyama.

“Nenda kaishi huko! Huyu mtoto anavyoanza kufanana nami na kila mtu anajua ni mtoto wako, tunaweza kuchafua hali ya hewa siku moja,” alisema Boniface.

“Basi sawa. Hakuna tatizo hata kidogo,” alisema Rose na kuondoka nyumbani hapo.

Alichokifanya Boniface ni kumwambia ukweli Jesca kwamba kwa kipindi hicho hakuwa tayari kumuoa na hakutaka kabisa kufikiria kuoa hata siku moja. Ilimuumiza moyoni mwake lakini alitakiwa kukubaliana na ukweli kwamba Boniface hakutaka kumuoa, kama alitaka basi waishi kama wapenzi lakini si kufunga ndoa.

Hilo halikuwa tatizo, kwa sababu alikuwa akimpenda sana mwanaume huyo, akakubaliana naye na kuanza kuishi pamoja. Mawazo ya Boniface bado yalikuwa kwa mpenzi wake, Miriam.

Mara kwa mara alikuwa akienda kwenye kituo kile kumwangalia mpaka siku ambayo madaktari walipomshauri na kumwambia kwamba lingekuwa jambo zuri kama angempeleka mwanamke huyo katika Hospitali ya Vichaa ya Milembe iliyokuwa mkoano Dodoma.

“Haina tatizo! Nipo tayari kugharamia kila kitu,” alisema Boniface.

Baada ya wiki moja, safari ya kuelekea mkoani Dodoma ikaanza. Moyo wake uliuma mno kwani alijua kwamba asingeweza kuwa karibu na msichana huyo kwa kumjulia hali mara kwa mara kama ilivyokuwa zamani.

Pamoja na kukaa huko, hilo halikumzuia kuacha kumpenda, halikumzuia kumuona mwanamke huyo kuwa mzazi mwenzake. Japokuwa alikuwa mbali na uwepo wa moyo wake lakini alijiahidi kwamba ilikuwa ni lazima awe anasafiri na Fabian kwenda huko kwa ajili ya kumuona.

“Nitakuwa nikija mara kwa mara kumuona,” alisema Boniface, alikuwa akizungumza na daktari wa kituo hicho.

“Hakuna tatizo! Unakaribishwa sana.”
“Nashukuru.”

Wakati yote yakiendelea, bado Fabian aliendelea kuwashangaza walimu kutokana na akili kubwa alizokuwa nazo. Alionekana kuwa mtoto wa ajabu, uwezo wake kichwani uliwachanganya walimu wenyewe.

Hakuwa mzungumzaji, muda mwingi alikuwa mpole lakini darasani, uwezo wake uliwashangaza hata walimu wenyewe. Hata alipomaliza chekechea na kujiunga na shule ya msingi, bado alionekana kuwa mtoto asiye wa kawaida.

Kila kona shuleni huko, alikuwa gumzo kubwa kitu kilichomfanya kupendwa na kila mtu. Ndiyo kwanza alikuwa na miaka sita kipindi hicho. Aliwahi sana kuanza darasa la kwanza kutokana na uwezo wake mkubwa.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne hapahapa.

Comments are closed.