The House of Favourite Newspapers

Insane (Mwendawazimu)-10

ILIPOISHIA

Kila kona shuleni huko, alikuwa gumzo kubwa kitu kilichomfanya kupendwa na kila mtu. Ndiyo kwanza alikuwa na miaka sita kipindi hicho. Aliwahi sana kuanza darasa la kwanza kutokana na uwezo wake mkubwa.

SONGA NAYO

Walimuona kama mtoto wao wa kumzaa, walimpenda kwa sababu hawakuwa na mtoto mwingine zaidi ya huyo ambaye waliamua kumpa jina na kumuona Theofil, ila wakawa wakimkatisha na kumuita Theo.

Walimpenda kutoka mioyoni mwao, alikuwa mtoto mzuri ambaye aliwafanya wote wawili kuwa na furaha kubwa. Hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba mtoto yule hakuwa wao, walikaa naye ndani tu na ni mara chache watu waliruhusiwa kumuona.

Kutokana na utajiri mkubwa waliokuwa nao, wakaahidi kumpa malezi bora, elimu bora na mambo mengine ambayo mtoto yeyote kutoka katika familia ya matajiri alitakiwa kupata.

Walimjali na kumlinda, Theo alikuwa kama yai, kila alipokuwa, walikuwa karibu yake, mfanyakazi wa ndani hakutakiwa kumgusa, muda mwingi walikuwa pamoja naye, walishinda naye chumbani na mara chache sana walitoka na kukaa katika bustani ya maua.

Siku zikakatika, miaka ikakatika, hawakutaka kutafuta mtoto mwingine, kwao, Theo alitosha, walipata mrithi ambaye waliamini kwamba baada ya miaka kadhaa watakapofariki basi mali zingebaki katika mikono halali na zisingeweza kupotea kama  ilivyotakiwa kuwa.

Mwaka wa tatu ilipoingia, Theo akachukuliwa na kupelekwa katika shule ya chekechea ya St. Mathew ambayo ilikuwa ikifundishwa na walimu wengi kutoka nchini Uingereza, shule hii ilikuwa Masaki jijini Dar es Salaam.

Mbali na Theo shuleni hapo, pia kulikuwa na watoto kutoka kwa mabilionea wengine, watoto wa mawaziri ambao wote hao walikuwa wakisoma hapo. Kila siku Edson alikuwa na kazi ya kumpeleka Theo shuleni hapo na kumfuata jioni tena akitangulizana na mkewe.

Kila walipomuona mioyo yao ilijawa faraja kiasi kwamba wakati mwingine wakasahau kwamba mtoto huyo hakuwa mtoto wao wa kumzaa.

Siku zikakatika, miezi ikakatika na miaka kwenda mbele. Baada ya miaka saba kupita, Theo akaanza shule ya msingi. Hakutakiwa kusomea nchini Tanzania, alichokifanya Edson ni kumchukua na kumpeleka nchini Marekani.

Huko akaanza kusoma katika Shule ya Msingi ya Forest Park. Hakutakiwa kurudi nchini Tanzania, maisha yake yalikuwa huko na wazazi hao walikuwa na kazi ya kumtembelea kila mwisho wa mwezi.

Walihakikisha mtoto huyo anapata malezi mazuri, hawakutaka kuona akipata mateso yoyote yale katika maisha yake na ndiyo maana walijitahidi kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba anakuwa na maisha mazuri kama walivyokuwa watoto wengine wa matajiri.

Baada ya miaka kadhaa, akamaliza elimu ya msingi na kuingia sekondari. Katika kipindi chote alichokuwa akikua, Theo alikuwa na sura nzuri, alikuwa muongeaji, mtundu na mgomvi kuliko wanafunzi wote.

Hilo lilimpa wakati mgumu shuleni, kila siku alikuwa akizungumziwa yeye. Alikuwa na hasira za karibu kiasi kwamba wanafunzi wote wakaonywa kwamba hawakutakiwa kumchokoza Theo kwani kwa jinsi alivyokuwa, alikuwua na uwezo wa kumfanya kitu chochote kile mtu yeyote.

“I am Assassin…” (mimi ni muuaji) alisema Theo huku akijitamba mbele ya wanafunzi wengine.

Hilo ndilo jina alilopenda kujiita kila siku. Hakutaka kumficha mwanafunzi yeyote, kila alipokuwa akichokozwa na kuwapiga wanafunzi hao, aliwaambia mara kwa mara kwamba yeye alikuwa muuaji.

Akaogopeka, mwili wake mkubwa ukawafanya wanafunzi wengi kumuogopa. Walimu walikuwa wakimuita mara kwa mara huku wakimtaka kubadilisha maisha yake lakini hakusikia, kila siku aliwaambia watu kwamba yeye alikuwa muuaji.

Jina hilo akakaa nalo mpaka alipomaliza masomo. Kutokana na kuwa mbali na wazazi wake, akawaambia wazi kwamba hakutaka kusoma nchini Marekani kwani kulimfanya kuwa mnyonge, wanafunzi hawakumpenda na muda wote aliwakumbuka hivyo alitaka kurudi nchini Tanzania kusoma.

“Unataka kuja kusoma huku?” aliuliza mzee Edson.

“Ndiyo dad. Siwezi kusoma huku na hawa Wazungu! Nataka nirudi Tanzania, nilipozaliwa na kukulia,” alisema Theo kwenye simu.

Mzee Edson hakutaka kuamua kitu peke yake hivyo akamshirikisha mkewe na kumwambia kile kilichokuwa kimetokea. Mkewe, Bi Rachel hakutaka kupinga, yeye mwenyewe hakupenda sana mtoto wake akae mbali naye, kila siku alipenda kumuona akiwa karibu naye hivyo akamwambia mumewe kwamba lingekuwa jambo jema kama kijana wao angerudi Tanzania.

“Hakuna tatizo! Si ametaka mwenyewe, mwache arudi,” alisema Bi Rachel.

Walikubaliana hivyo kitu kilichofanyika ni kufanya harakati ili mtoto wao aweze kurudi nchini Tanzania. Alipoambiwa kwamba anatakiwa kurudi Tanzania, moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kwamba hatimaye angeungana na familia yake.

Alipofika Tanzania, kitu cha kwanza kilikuwa ni kutawala na magari ya baba yake barabarani. Hakutaka kusikia kitu chochote kile, alitanua kadiri alivyotaka, alivunja sheria za nchi kadiri alivyotaka kiasi kwamba akawa kero.

Akawa mtu wa wanawake, wengi walimpenda kwa sababu alikuwa na fedha, baba yake alikuwa bilionea mkubwa. Akagawa fedha kadiri alivyotaka na hata alipoambiwa asimamie mali za wazazi wake, hakuwa tayari, aliona kama mtu aliyekuwa akibanwa.

Hakuwa na uwezo mkubwa darasani lakini akajikuta akiingia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuanza kusomea biashara. Alionekana kuwa na akili sana lakini ukweli ni kwamba hakuwa chochote kile.

Hakuwa mtu wa kusoma, hakuwa mtu wa kukaa darasani, muda mwingi alikuwa barabarani, alikuwa akiendesha magari huku ndoto zake zikiwa ni kuwa kama Lewis Hamilton, mwendesha magari aina ya langalanga.

Wakati akielekea shuleni hapo mara mojamoja ndipo alipomuona msichana mrembo, aliyetokea kuvutiwa naye, msichana mwenye figa matata, msichana huyu aliitwa Esther. Moyo wake ukatokea kumpenda msichana huyo, alikuwa mrembo wa sura na kila alipomuona, moyo wake ulikufa na kuoza, alimtaka, alijitahidi kumfanyia ucheshi wa kila namna lakini msichana huyo hakuwa na habari naye.

“Ni nani anamfanya huyu msichana kunichunia hata nikimsalimi? Au hajui kama mimi ni mtoto wa bilionea? Subiri! Nitamfuata tu na si kuishia kumsalimia,” alijisemea, wakati akizungumza hayo, miguu aliweka juu ya meza ambapo hapo kulikuwa na mabunda ya hela aliyokuwa ameyapanga. Kwa hesabu za harakaharaka zilikuwa kama milioni kumi na tano.

Wanafunzi wote wakawa wakimtolea macho, ila yeye hakujali.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa

Comments are closed.