The House of Favourite Newspapers

Afande Sele: Ilibakia Hivi tu Nibebe Unga

STORI: NA OJUKU ABRAHAM | RISASI MCHANGANYIKO|

DAR ES SALAAM: Wakati joto la watu wanaohusishwa na madawa ya kulevya likizidi kupanda, Mfalme wa Rhymes nchini, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele, ameibuka na kutoa ushuhuda jinsi ilivyobakia kidogo tu, awe msafirishaji wa mihadarati, Risasi Mchanganyiko lina stori kamili.

Akizungumza kwa njia ya simu na Risasi Mchanganyiko, Afande Sele, mmoja wa wasanii wakongwe wa Muziki wa Kizazi Kipya, alisema enzi zao wakato wakiwika, aliwahi kushawishiwa abebe unga, lakini kwa kuwa ni mtu anayejitambua, alikataa kujihusisha na mchezo huo.

“Sisi wakati ule tulifanya muziki kama burudani, tuliandika mistari mizuri ambayo ilitupatia majina na mashabiki wengi, vijana wa sasa wanafanya biashara ya muziki, wanaingia studio wanafanya muziki halafu wanatoa fedha nyingi katika promo, matokeo yake muziki hauna lolote lakini unapata airtime kubwa.

“Halafu utaona baada ya promo kubwa, wanaenda Sauz (Afrika Kusini) kushuti video. Ninakuambia hivi asilimia kubwa ya wasanii wanaoenda kushuti video kule wanasafirisha madawa ya hao wanaowapa hela ya promo, mimi nilishawahi kutakiwa nibebe unga, nikakataa, ndiyo maana unaona tunapotea kwenye media.

“Enzi zetu gemu lilikuwa gumu, hakukuwa na video wala hela ya promo, lakini tulikuwa tunapata hela kidogo, tumeshapewa sana dili hizo. Madogo wengi siku hizi utasikia sijui China sijui wapi, hakuna lolote, hawana vipaji, wanatafuta pesa kwa njia yoyote ilimradi watoke,” alisema mwimbaji huyo kiongozi wa Kundi la Watu Pori.

Akizungumzia sakata hilo la madawa ya kulevya, alisema endapo vita hivyo vitapiganwa kwa haki, watu wengi wanaoonekana wasafi wanaweza kugeuka kuwa wachafu, kwani biashara hii inafanywa na kila kada, wakiwemo viongozi wa dini!

“Kuna watu wengi wanaojihusisha na hii biashara na wanajulikana, lakini tatizo hatupo siriasi na hili jambo, kama viongozi wakimaanisha, vita hivi ni rahisi, tutakutana na maaskofu, mashehe, mapadre na kila aina ya watu ambao tunawaona ni wasafi. Mabwana wadogo wengi sana wamepotea kwa sababu ya ishu hii, ninaunga mkono harakati za kukomesha biashara ya unga,” alisema.

Comments are closed.