The House of Favourite Newspapers

Insane (Mwendawazimu)-7

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI

ILIPOISHIA

“Bora nimuache huyu malaya Jesca, siwezi kumsaliti Miriam. Bora nimwambie ukweli kwamba kama mapenzi kufa, acha yafe sasa hivi nibaki nilee mimba na nisubiri mtoto,” alisema Boniface. Hakutaka kuchelewa, hapohapo akachukua simu yake na kumpigia simu Jesca.

SONGA NAYO

“Hallo Jesca…naomba unisikilize,” alisema Boniface mara baada ya kupiga simu.

“Mbona sauti yako haisikiki kikawaida, kuna nini baby?” ilisikika sauti ya Jesca upande wa pili.

“Nilikuwa nataka kusema hivi…”

“Kwamba hunitaki tena, si ndiyo?” aliingilia Jesca. Boniface akashusha pumzi nzito kwani hakujua msichana huyo alijua vipi kile kilichokuwa kikiendelea akilini mwake.

“Mbona unakuwa na presha…”

“Niambie tu! Wala usiogope kuniumiza Boniface. Niambie ukweli tu,” alisikika Jesca kwenye simu, tayari akaanza kulia.

“Hapana! Sikumaanisha hivyo!”
“Umemaanisha nini?”
“Kwamba ninataka nianze upya mapenzi na wewe. Najua kwamba nimekuumiza, sikutaka uwe hivyo, nimekuwa na mambo mengi ya kiofisi ambayo yamekuwa yakiniendesha puta. Nahisi huu ni muda sahihi wangu kuwa na wewe na kuanza upya,” alisema Boniface.

“Kweli mpenzi?”
“Ndiyo mamii!”
“Upo wapi?”
“Nyumbani!”
“Nakuja!”

“Sawa.”

Alipokata simu, akauma meno yake kwani hakuamini kama yeye ndiye aliyemwambia Jesca maneno yale. Hofu ilimuingia ndani ya moyo wake na mbaya zaidi akaanza kumuonea huruma msichana kwa jinsi alivyokuwa akilia.

Alikumbuka jinsi alivyokuwa akimpenda kipindi cha nyuma, alivyojitolea moyo wake kumpenda. Kumbukumbu hizo zote zilimfanya kumuona msichana huyo mkuwa muhimu katika maisha yake japokuwa alikuwa akimsaliti kwa kutembea na Miriam Mwendawazimu.

Wala hazikupita dakika nyingi, Jesca akafika nyumbani hapo. Kitu cha kwanza kabia kukifanya mara baada ya kumuona Boniface ni kumsogelea na kisha kumkumbatia. Hakuamini kile alichokuwa ameambiwa, alitaka kusikia huku akiangalia macho kwa macho na mwanaume huyo.

Boniface hakubadilika, alimwambia ukweli kwamba huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuanza upya kwani kulikuwa na mambo mengi yaliyokuwa yametokea kipindi cha nyumba na ndiyo maana alikuwa amebadilika.

“Ulinitia hofu moyoni mwangu, sikuamini kama kweli umeuona udhaifu wako na kuniambia ukweli,” alisema Jesca huku akimwangalia Boniface machoni mwake, moyo wake ukazidi kumpenda msichana huyo.

“Amini hilo mpenzi! Nimekuwa mtu mpya.”
Mapenzi yakawa kama yamerudi lakini ukweli ni kwamba Boniface hakutaka kumpenda msichana huyo tena. Alitamani kumwambia ukweli kwamba hakutaka kuwa naye kwa sababu alikuwa na mpenzi mwingine lakini hilo lilishindikana kabisa.

Usiku huo ukawa wa kupeana mapenzi, kila wakati Jesca alionekana kuwa na furaha, kipindi cha nyuma alikata tamaa na kuona kwamba isingekuwa kazi rahisi kuirudisha furaha ya mpenzi wake lakini mwisho wa siku alifanikiwa.

Wakati moyo wake ukiwa na furaha kubwa, moyo wa Boniface ulikuwa ukimfikiria Miriam tu. Alijilaumu kwa kufanya mapenzi na Jesca, usoni alionyesha tabasamu lakini moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali.

Siku iliyofuata, Boniface akaondoka na kuelekea kazini. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, alikumbuka kwamba Miriam alikuwa hospitalini akiumwa kutokana na ujauzito aliokuwa nao, ilikuwa ni lazima kuondoka mahali hapo na kwenda kumjulia hali.

Asingeweza kubaki ofisini na wakati mama mtarajiwa wa mtoto wake alikuwa hospitalini akiumwa. Alichokifanya ni kuondoka kuelekea hospitalini huko. Kwa sababu madaktari walimfahamu kama msamaria mwema aliyemleta Miriam, wakampa taarifa kwamba hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.

“Kwa hiyo anaruhusiwa kutoka?”

“Ndiyo! Ila inabidi aogeshwe na kubadilishwa nguo,” alisema daktari.

“Hilo halina tatizo!”

Boniface akaondoka hospitalini hapo na kwenda katika duka la nguo za kike ambapo huko akanunua suruali ya jinsi na blauzi kisha kuwapelekea madaktari. Walichokifanya ni kumuogesha, kumkata nywele zake na kisha kumbadilisha nguo zile.

Boniface hakuamini mara baada ya Miriam kuletwa kwake, alionekana kuwa msichana wa tofauti, siku hiyo ndiyo akagundua kwamba kweli alikuwa amempa mimba msichana aliyekuwa mrembo kupitiliza.

Moyo wake ukafa zaidi katika penzi la msichana huyo kwani siku hiyo alionekana kuwa mrembo haswa zaidi ya Alicia Keys. Akajisahau kabisa kama msichana huyo alikuwa kichaa, alitamani kuwaambia madaktari wamfungue kamba walizomfunga ili wakumbatiane. Aliduwaa tu huku akimwangalia Miriam.

“Mbona unamwangalia hivyo?” aliuliza nesi huku akimwangalia Boniface, uso wake ulikuwa na tabasamu pana.

“Kweli Mungu hakupi vyote. Huyu msichana ni mzuri kweli,” alisema Bonifacem, hakutaka kuficha.

“Si ndiyo umuoe sasa! Au unaogopa kwa sababu yeye ni kichaa?” aliuliza nesi huyo.

“Wala siogopi. Nimetokea kumpenda kweli jamani!” alisema Boniface. Manesi wote wakahisi kwamba alitania lakini ukweli wa moyo wake ni kwamba alimpenda haswa.

“Kwa hiyo unaondoka naye au?” aliuliza nesi.

“Hapana! Acha akae hapahapa hospitalini! Nitalipia kila kitu mpaka atakapojifungua,” alisema Boniface kwani alijua kwamba Miriam angepata tabu sana mitaani kwani hali aliyokuwa nayo, ilikuwa ni lazima awe karibu na madaktari.

Hilo halikuwa tatizo, walichokifanya madaktari ni kumchukua na kumpeleka katika kituo cha vichaa, huko, maisha yake yakaanza upya. Kila siku alikuwa akiamka asubuhi na mapema, anapumzika na vichaa wengine huku wakicheza michezo yao, walikuwa wakila na kufanya mambo mengine na muda wa kula walikuwa wakila pamoja kisha kulala.

Boniface alikuwa na kazi ya kufika hospitalini hapo kila siku. Alimpenda mno Miriam, alishindwa kujizuia kwani hata alipokuwa akifika hospitalini hapo, aliomba muda wa kuwa na msichana huyo na kisha kuzungumza naye.

Manesi walimshangaa, hawakusikia maneno aliyokuwa akizungumza naye lakini walijua dhahiri kwamba jamaa alikuwa amekufa na kuoza kwa msichana huyo kichaa.

“Miriam mpenzi. Najua hali uliyokuwa nayo, najua unateseka kiasi gani, najua nimefanya kosa kubwa kukubaka, lakini ukweli ni kwamba ninakupenda. Mungu anaujua moyo wangu, nina mapenzi makubwa juu yako. Ninahuzunika kwa hali uliyokuwa nayo lakini sina jinsi. Una mimba yangu, naomba uitunze na mtoto akizaliwa, nitampa jina na nitamlea mimi mwenyewe,” alisema Boniface huku akimwangalia Miriam, wakati yeye akizungumza hayo, mwenzake hakuwa na habari naye.

“U msichana mrembo sana, huwa sijutii kabisa kukupenda. Umeyabadilisha maisha yangu na kunifanya kuwa mwanaume bora, na ninajua utanifanya kuwa baba bora pia. Nakupenda mpenzi. Nitakuja kukuona kesho,” alimalizia Boniface na kisha kuinuka na kuondoka katika sehemu ile aliyokaa na Miriam.

Akazoeleka kwa manesi na madaktari, kila siku alipokuwa akifika hospitalini hapo, alikuwa akiachwa aongee na msichana huyo ambaye alionekana kutokuelewa kitu chochote kile.

Alianza kama utani lakini baadaye akawa anamshika mpaka mkono na kuzungumza naye waziwazi. Alishindwa kabisa kuzizuia hisia zake, manesi wakaligundua penzi kubwa alilokuwa nalo kwa msichana huyo. Mpaka siku ambayo Miriam alishikwa na uchungu, Boniface alikuwa akifika hospitalini hapo.

“Dokta…dokta…naomba mumsaidie Miriam…” alipiga kelele Boniface mara baada ya kumuona ameanguka chini huku akilishika tumbo lake na damu kuanza kumtoka.

Hrakaharaka manesi watatu wakatokea mahali hapo, wakamchukua Miriam na kuanza kuondoka naye. Vichaa wengine waliokuwa eneo hilo walibaki wakishangaa, hawakujua kitu gani kilikuwa kikiendelea.

Harakaharaka akapelekwa kwenye chumba kilichoandikwa Labour kwa nje na kumlaza kitandani. Boniface hakutakiwa kuingia ndani, walimwambia abaki nje kwani wao kama wauguzi walikuwa wakitakiwa kufanya kazi yao. Hilo wala halikuwa tatizo, akatulia na kuanza kusikilizia hapo nje, alichotaka kusikia ni sauti ya mtoto tu.

“Mungu! Siamini kama nakwenda kuwa baba! Naomba umsaidie Miriam ajifungue salama,” alisema Boniface huku akiwa ameikutanisha mikono yake huku akiwa amepiga magoti.

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane Jumanne mahali hapa.

Comments are closed.