The House of Favourite Newspapers

Ishu ya Madawa ya Kulevya, Kamanda Shilla Awaonya Polisi Airport

0

KAMANDA wa Polisi wa Viwanja vya Ndege nchini, Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Jeremiah Shilla amewaagiza Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kudhibiti dawa za kulevya na ikibainika dawa hizo zimepita katika uwanja huo watachukuliwa hatua kali.

 

Akizungumza na askari katika uwanja huo leo Jumatatu Januari 3, 2022, Kamanda Shilla amesema nilazima polisi waongeze bidii katika kukabiliana na dawa za kulevya katika uwanja huo, kwani bado kuna dawa hizo mitaani.

 

“Muendelee kujipanga vizuri kukabiliana na madawa haya na yoyote ambaye anathubutu kutaka kupitisha madawa katika uwanja huu akamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” amesema.

 

Amesema ikibainika dawa zimepita katika uwanja huo, hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria. Kamanda Shilla amewataka polisi hao kuimarisha uhusiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na jamii ili kuhakikisha wahalifu wanadhibitiwa.

 

“Polisi katika uwanja huu mjuwe mpo katika uwanja wa kimkakati kwa Serikali hapa ni lango la utalii hivyo mtoe huduma bora kwa wateja,” amesema.

 

Awali Mkuu wa kituo kidogo cha polisi Kia, SP Edith Makweli amesema polisi katika uwanja huo kwa kushirikiana na vyombo vingine wamekuwa imara wakati wote kudhibiti uhalifu ikiwemo kudhibiti dawa za kulevya.

 

“Tuna kikosi imara cha askari na mbwa ambao wamekuwa wakifanya ukaguzi na doria usiku na mchana katika eneo hili,” amesema.

 

Kamanda Shilla alipata fursa ya kutembelea kikosi cha Mbwa, kukagua nyumba za wafanyakazi na kuzungumza na maafisa wa polisi katika kituo hicho.

Leave A Reply