The House of Favourite Newspapers

Jaji Mkuu Kenya ashauri hali ya kisiasa Zanzibar

0

Mutunga2

Jaji Mkuu wa Kenya, Dk Willy Mutunga.

JAJI Mkuu wa Kenya, Dk Willy Mutunga amesema hali ya kisiasa inayoendelea Zanzibar inahitaji busara ya mazungumzo ili kupata mwafaka.

Aidha, amesema anaamini hakuna kitakachoshindikana kwa kuwa Tanzania ni walimu wazuri katika mambo mengi na kwamba nchi kama Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda zinajifunza kutoka kwa Tanzania.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kuzungumza na majaji wa Tanzania kuhusu mageuzi ya Mahakama ya Kenya.

“Tanzania ina kila cha kujivunia kwani hakuna ukabila, wanajivunia lugha yao, utamaduni na msimamo wa ujamaa. Sidhani kama mmeingia katika ubepari na ukabaila,’’ alisema Jaji huyo na kuongeza kuwa msimamo wa Mwalimu Julius Nyerere ulijali maslahi ya wengine katika masuala mbalimbali ikiwemo uchumi na siasa.

Aidha, alisema Tanzania inafanya vizuri kuliko Kenya katika masuala ya usikilizaji wa kesi. Alisema watajifunza namna ya kusikiliza kesi haraka ili kumaliza mashauri kwa muda.

“Kenya iliwahi kusikiliza kesi tatu kwa zaidi ya miaka 33 hivyo ni tofauti na wanavyofanya wenzetu Watanzania,’’ alisema Jaji Mutunga na kusisitiza kuwa katika Afrika Mashariki, majaji na mahakimu wengi hawachukui rushwa na kwamba njia nzuri ni kuwatoa wanaopokea rushwa.

Leave A Reply